• Tidak ada hasil yang ditemukan

4.3 Falsafa ya Washairi Teule Juu ya Mwanamke

4.3.1 Falsafa ya Shaaban Robert juu ya Mwanamke

Shaaban Robert anamuona mwanamke kuwa na nafasi kubwa katika kuyafanya maisha ya duniani kuwa mazuri au mabaya. Mwanaume aliyejaaliwa kupata mke mzuri huishi maisha kama ya peponi. Yule aliyejaaliwa kupata mke mwovu na msumbufu huishi maisha mabaya ya shida na taabu kama aliye motoni. Falsafa hii inatokana na mafundisho ya dini ya Kiislamu kwamba mwanamke ni kiumbe wa kumtumikia mume kwa kumstarehesha kwa starehe mbalimbali za Kibailojia, kijamii

na kiutamaduni. Katika shairi la “Dunia Njema” katika kitabu cha Ashiki Kitabu Hiki anasema:

Dunia nzuri na mambo yake, Yana fahari ya peke yake, Juu sayari ni taa zake, Chini Johari ardhi yake. Zulia lake nyasi kijani,

Na maji yake mvua mbinguni, Kushuka kwake milele shani, Sifa ni zake Mola Manani (uk. 28).

Hii inamaanisha kuwa dunia ni mahali pazuri pa kuishi na kupata starehe za aina kwa aina kutokana na mambo ya dunia. Msitari wa kwanza wa ubeti huu unajenga ishara kuwa kinachoifanya dunia kuwa mahali pazuri pa kuishi ni mambo yake. Mambo haya ni pamoja na kuwa na mke mwema na mwadilifu. Tumeihusianisha ishara hii na shairi la “Kuoa” katika diwani hiyohiyo ambalo linaeleza kuwa:

Kuoa mke si kufu, Atakuliza machozi, Kwa mambo yake dhaifu, Ukonde ubaki ngozi, Huwezi kumsarifu, Cheo chako hakiwazi, Kwake kama upuuzi,

Yafahamu yasemwayo (uk. 6).

Hii inamaanisha kuwa kuoa mwanamke ambaye ni muovu na asiye na adabu ni dhiki kubwa katika maisha ya mwanaume. Kumbe starehe kubwa katika maisha ya mwanaume ni kuwa na mke mwema. Ili kuepukana na dhiki hii Shaaban Robert anawataka wanaume kuomba dua kwa Mwenyezi Mungu kuomba kupatiwa mke mwema. Mwanamke watakaye muomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu awe amepambika kwa sifa nzuri. Miongoni mwa sifa hizo ni zile zilizopo katika shairi la “Urafiki” katika kitabu cha Pambo la Lugha. Anasema;

Umbo la kupendeza, kama la malaika Sura ya kufurahisha, kama ile ya pepo Umbo la takaso, kama mbingu na mwezi Hulingani na mkadi, labda luli bahari (uk. 32).

Huyu ndiye mwanamke ambaye Shaaban Robert anamuona kuwa ataweza kumpatia mwanaume starehe ya duniani. Momanyi (2001) anaziona sifa alizopambwa mwanamke katika ubeti huu ni za kumfanya kuwa ni kifaa cha kutumiwa na mwanaume kama chombo cha starehe. Momanyi (ameshatajwa) amesahau kuwa Falsafa ya Shaaban Robert kumhusu mwanamke ni kuwa, ni kazi na wajibu wa mwanamke kumpatia mumewe starehe zote anazohitaji katika maisha. Hata hivyo, tunapingana na mawazo ya shaaban Robert hapo juu kuwa sifa alizompamba nazo mwanamke katika ubeti hapo juu hazitoshi kumfanya mwanamke kuwa kiumbe anayeweza kumpatia mwanaume starehe zote anazohitaji katika maisha. Sifa muhimu aliyoisahau katika ubeti huu ni tabia njema ya mwanamke. Mwanamke muovu atamfanya mumewe kuwa mtu wa shida na taabu katika maisha yake yote.

Katika kuendeleza falsafa yake kuhusu nafasi ya mwanamke katika maisha ya mume na jamii kwa jumla, Shaaban Robert anaonya kuwa starehe hizo huwa zina mwisho wake. Katika Shairi la “Maswali na Majibu” katika Ashiki Kitabu Hiki anasema:

Dunia imetubana, Imetuvika masombo, Tulikwenda kwa mapana, Tukapiga watu fimbo. Ngoma ikivuma sana, Ni kupasuka kiwambo, Roho zimejaa mambo,

Radha ziko wapi tena? (uk. 105).

Hii inaonesha kuwa starehe anazopata mwanadamu hapa duniani ikiwamo ile ya kuwa na mke mwema na kushiriki naye katika starehe za kingono, hufika mahali

zikaisha. Kwa sababu starehe hizo huwa zinakwisha mwanadamu anaaswa kutoziabudu na kuziendekeza starehe hizo. Kutokana na kuendekeza starehe hizo baadhi ya watu hutoka nje ya ndoa zao na kujisababishia madhara makubwa ya kupata maradhi. Pamoja na Shaaban Robert kuonesha falsafa yake juu ya mwanamke kuwa na nafasi kubwa katika kumpatia mwanaume starehe za dunia ametoa pia hadhari muhimu kwa wanaume kutoendekeza starehe hizo na kufikia kufanya maasi. Hadhari hii ni sahihi na inapendeza ikifuatwa na wanajamii katika maisha yao ya kila siku. Baadhi ya wanaume wanapoona wake zao wamezeeka hutafuta watoto wadogo wa kike na kuwa na mahusiano nao.

Kwa upande wa pili falsafa ya Shaaban Robert kumhusu mwanamke inaona kuwa mwanamke anapaswa kupata stahili sawa na zile anazopata mwanaume katika maslahi ya kazi. Haiwezekani mwanamke na mwanaume wakafanya kazi iliyo sawasawa halafu mwanamke akapata ujira kidogo na mwanaume ujira mkubwa. Kwa mfano, wakati mwanaume anakwenda kazini asubuhi mwanamke hubaki nyumbani kulea watoto wao na kufanya kazi za ndani kama kufua nguo, kuosha vyombo, kusafisha nyumba, kuandaa chakula na kuwahudumia watu wote waliopo katika nyumba yao. Kazi hizi huwa hazina malipo kwa mwanamke na hata akiwa na shida yoyote ile inayohitaji kutatuliwa kwa fedha inakuwa vigumu kuitatua. Mwanaume ambaye amemwachia mke mzigo mzito wa shughuli nyumbani hulipwa mshahara na hathubutu hata mara moja kumkumbuka mke ambaye ndio anayeandaa mazingira mazuri ya mume kufanya kazi. Katika shairi la “Nani Atakutendea” anaeleza:

Kazi bila manufaa, Nani atakutendea, Sinifanyie hadaa, Kungwi hakunihusia.

Sinifanyie hamaki, Shetani wangu hataki, Sharti unipe haki,

Ndipo ataputulia (uk. 13).

Shairi hili linaonya kuwatumikisha wanawake kwa kazi nyingi bila ya kuwapatia malipo stahiki au hata kutambua mchango wao. Usawa wa malipo baina ya mwanaume na mwanamke katika kazi ni kitu muhimu kitakacholeta ustawi wa maisha ya wanaadamu wote katika maisha yao ya duniani.