• Tidak ada hasil yang ditemukan

4.4 Dhima ya Tamathali za Usemi katika Kujenga Dhamira

4.4.1 Dhima za Kimaudhui

4.4.1.3 Kufafanua Jambo

Tamathali za usemi katika mashairi ya magazetini zina dhima ya kufafanua masuala mbalimbali yenye masilahi kwa wananchi na taifa lao. Kufafanua jambo ni kulitolea maelezo ya kina ili liweze kufahamika vizuri mbele ya wale wanaopaswa kulifahamu jambo hilo kwa nia na makusudio yaliyolengwa na mtunzi wa shairi. Katika utafiti huu tunaona kwamba, tamathali za usemi zina dhima ya kufafanua njia ambazo

zinaweza kumfanya mtu akaambukizwa UKIMWI. Mshairi Yusuf R. R. Mfalme kupitia shairi lake la “Kuenea kwa UKIMWI,” anaeleza kwamba:

Wale wapenda zinaa, kondomu wanotumia Wakizoea kuvaa, siku zikisha titia

Hatima wanazitwaa, mbali wanaziachia

Wenyewe huwa wasema, kwamba wamezoweana Zile mila za kigeni, ndizo zinatusumbua

Ushamba uafukani, mila zetu hutibua

Wazazi nambari mbili, lawama kwenu natua Ati mwaishi uzunguni, watoto kuvaa uchi! (UHURU, Mei 14, 2003. Yusuf R. R. Mfalme).

Katika beti hizi mbili za shairi tunamuona mshairi akifafanua kwa kutumia tamathali ya usemi ya taswira baadhi ya mambo ambayo yanachangia maambukizi ya UKIMWI katika jamii zetu. Katika ubeti wa pili msitari wa tatu anaeleza kwamba, “watoto kuvaa uchi,” katika hali ya kawaida mtu hawezi kuvaa uchi, ni hali ya mtu kuwa utupu pasipo kuvaa nguo. Mtu anapokuwa hajavaa nguo ndio anakuwa yupo uchi na anapovaa nguo anakuwa amejisitiri. Kwa hakika, matumizi ya taswira hii yanatoa ufafanuzi kwamba, uvaaji wa nguo ambazo zinaonesha maungo na mapambo ya mwili hasa ule wa mwanamke basi huwatamanisha wanaume na kuwataka wanawake hao kimapenzi, jambo ambalo, huchangia maambukizi ya UKIMWI. Tulifanya usaili na Mzee John Mwasakija, mkazi wa Ilala Sharifu Shamba kuhusiana na suala hili naye akatueleza kwamba:

Siku hizi dunia imeharibika sana mwanangu. Siku hizi mwanamke anavaa nguo ambazo zinamwacha uchi bila ya kuona haya yoyote mbele za wanaume na hata wanawake wenzake. Hali hii kwa kiasi kikubwa inachangia kuongeza maambukizi ya UKIMWI kwa jamii. Kama inavyofahamika, mwili wa mwanamke hasa wa Kiafrika umeumbwa na Mwenyezi Mungu kwa namna ambayo humvutia mwanamume yeyote rijali, anapoona maungo ya mwanamke hasa mapaja na makalio. Baadhi ya wanaume wanapoona maungo hayo huchanganyikiwa na kufanya kila wanaloweza mpaka ampate

mwanamke huyo. Kwa kufanya hivyo, mwanamke huyo anaweza kukutana na vishawishi mbalimbali vya wanaume ambao tayari wameshaambukizwa UKIMWI. Vilevile, wanaume wote ambao pia watavutiwa na mwanamke huyo na kufanya nae mapenzi wanakuwa katika hatari ya kuambukizwa UKIMWI.

Maelezo haya yanathibitisha ufafanuzi unaoelezwa na mshairi juu ya mambo yanayochangia maambukizi ya UKIMWI katika jamii. Suala la wanawake na wasichana kuvaa mavazi ambayo yanaonesha maungo yao si utamaduni wa Mwafrika bali ni wa wageni hasa Wazungu. Kuiga utamaduni wa kigeni na kuufanya kama sehemu ya utamaduni wa jamii yetu hasa hili la mavazi limechangia katika kuongeza maambukizi ya UKIMWI katika jamii hasa katika kipindi kile ambacho jamii ilikuwa haina ufahamu mkubwa kuhusu UKIMWI.

4.4.1.4 Kufanikisha Mawasiliano

Tamathali za usemi katika mashairi ya magazetini zina dhima ya kufanya mawasiliano katika jamii juu ya jambo au mambo ambayo mshairi anataka yaifikie jamii yake. Mawasiliano ni hali au kitendo cha kupashana habari kati ya mtu na mtu, mtu na kikundi, kikundi na kikundi, taasisi na mtu, jamii na jamii na kadhalika. Tamathali za usemi katika mashairi ya magazetini zina dhima ya kufanya mawasiliano kati ya mtunzi wa shairi na wadau wa masuala ya UKIMWI kwa nia na makusudio tafautitafauti. Kwa mfano, mshairi Camdulla Msimbe kupitia shairi lake la “Kitumbua,” Anaeleza kuwa:

Hata kwa kunywea chai, Sasa hakitamaniki Kula tena hakifai, na wala hakiuziki

Mdomoni hakikai, mkononi hakishikiki Kitumbua hakiliki, kimeingia mchanga Afadhali ya chapati, bajia, donati na keki Nile kwa huu wakati, roho juu siiweki

Kitumbua hakiliki, kimeingia mchanga Nikikute kitumbua, nakipiga ovateki Kisije kuniumbua, nikawa sieleweki Watu nikawasumbua, shida kwao sipeleki Kitumbua hakiliki, kimeingia mchanga

Katika beti tatu za shairi hapo juu, mshairi anatumia tamathali za usemi kwa nia ya kufanya mawasiliano na jamii kuhusu UKIMWI. Kitumbua ni neno ambalo limetumika kiishara kuashiria tendo la ngono ambalo utamu wake unafananishwa na ladha ya kitumbua. Kwa kawaida kitumbua kinapoanguka chini na kupatwa na mchanga basi hupoteza thamani na ladha yake kwa mlaji, atakula kitumbua hicho kwa hofu na mashaka asije akaumiza meno yake. Matumizi ya tamathali hii ya usemi yana dhima ya kuipasha jamii kuwa, tendo la ngono ambalo lina utamu sawa na kitumbua na pengine zaidi yake sasa ni hatari kufanywa hovyo hovyo bila ndoa na kuaminiana baina ya wapenzi wawili, kwa sababu mwisho wake ni kupata UKIMWI. Msomaji yeyote atakayekutana na shairi hilo atakuwa amepata taarifa, kwamba UKIMWI ni hatari na hivyo ajiepushe kufanya ngono zembe ambazo ni hatari kwa afya na maisha yake kwa jumla.

Katika ubeti wa tatu mshairi anajenga taswira kwamba, mwanamke wa barabarani yaani mwanamke asiyekuwa wa kwake anamuona kama mtu hatari. Akikutana naye barabarani atampita kwa kasi kubwa na kamwe hataki kuwa karibu na mwanamke huyo. Dhima ya ishara hii ni kuitaka jamii kutokuwa na mahusiano na wanawake au wanaume ambao wanakutana nao barabarani kwa sababu wanaweza kuambukizwa UKIMWI na kisha kuyaweka maisha yao rehani. Ishara hii pia inajenga picha kwamba, si jambo jema kwa mtu yeyote awe mwanaume au mwanamke kujenga

mazoea yanayoweza kumsababishia kuwa na uhusiano wa kingono na mtu huyo, jambo ambalo linaweza kumfanya apate UKIMWI.

4.5 Dhima za Tamathali za Usemi Kifani