• Tidak ada hasil yang ditemukan

Kwa kuwa data za utafiti ziliwasilishwa, kuchambuliwa na kujadiliwa kwa mujibu wa malengo mahususi na muhtasari wa sura hii pia umetolewa kwa kuzingatia malengo mahususi ya utafiti.

5.1.1 Dhamira za Kijamii katika Riwaya ya Kiu

Dhamira za kijamii kama tulieleza hapo awali kuwa hizi ni dhamira ambazo zinahusu maisha ya kila siku ya wanadamu. Ni dhamira ambazo zinatokana na shughuli mbalimbali za jamii katika harakati za kudumisha maisha yao. Katika riwaya ya Kiu kuna utajiri mkubwa wa dhamira za kijamii lakini katika utafiti huu ni 5 tu ndizo zilizowasilishwa, kuchambuliwa na kufanyiwa mjadala. Dhamira hizo ni usafi wa mazingira, mapenzi katika jamii, wizi na magendo, umaskini katika jamii na ujasiriamali. Tukieleza kwa muhtasari kuhusu dhamira ya usafi wa mazingira kama ilivyosawiriwa katika riwaya ya Kiu mwandishi anabainisha kuwa jamii usafi wa mazingira bado ni changamoto kubwa katika jamii. Jamii hafanyi jitihada kubwa katika usafi wa mazingira licha ya kuwa wao ndio watumiaji wa mazingira na ndio

wanaosababisha uchafuzi wa mazingira. Pia, serikali nayo bado haikufanya jitihada kubwa katika usafi wa mazingira jambo linalosababisha miji kuwa michafu na kuibuka kwa magonjwa ya kuambukiza kama kipindupindu na homa za matumbo.

Dhamira nyingine ambayo tunaweza kuieleza kwa muhtasari ni ile ya wizi na magendo ambayo imesawiriwa vizuri katika riwaya ya Kiu ya Mohamed Suleiman. Mtunzi anathibitisha kuwa wizi na magendo ni vitu ambavyo kwa sasa vimetawala katika jamii kwani watu wengi hupata utajiri wa mali kutokana na njia za wizi na magendo. Tabia hii imezoeleka katika jamii kiasi cha kufanya wanajamii kuamini kuwa wanaweza kupata utajiri kwa njia za wizi na magendo na utajiri wao ukawa ni wa uhalali. Kashifa za rushwa na ufisadi zimekuwa nyingi katika jamii ya Watanzania kiasi cha kufanya kila idara na taasisi za serikali na za binafsi kuhusishwa na rushwa. Jambo hili si jema hata kidogo na linapaswa kukomeshwa ili likome kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi ya Tanzania.

Ujasiriamali ni dhamira nyingine ambayo imejitokeza kwa kiasi kikubwa katika riwaya ya Kiu. Kama tulivyosema mahali fulani katika tasinifu hii ni kuwa katika jamii ya leo kila kitu kimekuwa ni bidhaa kiasi kwamba kama mtu hana fedha hawezi kuishi maisha mazuri. Ujishughulishaji wa akina mama hasa kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo za kijasiriamali kumesaidia kuwawezesha akina mama kumudu gharama za maisha hata pale wanapofiwa na waume zao. Mfano mzuri ni Cheusi ambaye alifiwa na mumewe na kisha kuachwa na mtoto ambaye alikuwa ni mwanafunzi. Kwa kufanya shughuli ya kusukuma maandazi na mikate aliweza kupata fedha ambazo zilimsaidia kuendesha maisha yake na mtoto wake ingawa

fedha hizo hazikuwa za kutosheleza. Huu ni mfano mzuri ambao unafaa kuigwa na akina mama wengine kwa kuwa ni kitu ambacho kinawezekana.

Dhamira nyingine zilizowasilishwa, kuchambuliwa na kujadiliwa ni pamoja mapenzi katika jamii na umaskini. Matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa ipo dhana kuwa mwanamke maskini anaweza kumkubali mwanaume yeyote tu alimradi anao uwezo wa kifedha. Dhana hii alikuwa nayo Iddi ambaye ni dereva wa Mzee Mwinyi kwa miaka mingi. Iddi aliamini kuwa Mwinyi anaweza kumpata Bahati kwa sababu yeye alikuwa ni tajiri na Bahati alitoka katika familia ya kimaskini. Mawazo haya yanaweza kuwa na ukweli fulani lakini pia yasiwe na ukweli katika baadhi ya mazingira. Hata hivyo, mapenzi yanayosabishwa na watu kupenda fedha ni mengi zaidi kuliko yale ya mtu kumkataa mtu kutokana na utajiri wake.

5.1.2 Mbinu za Kifani katika Riwaya ya Kiu

Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa Riwaya ya Kiu ya Mohamed Suleiman inasheheni utajiri mkubwa wa mbinu za kifani lakini katika utafiti huu tumeshughulikia vipengele vya matumizi ya mbinu ya barua, misemo, sitiari, tashihisi na taharuki tu. Sababu hasa ya kuteua mbinu hizi 5 ni kuwa zinatosheleza mahitaji ya malengo ya utafiti huu. Mbinu ya matumizi ya barua imetumiwa kwa lengo la kukuza na kuendeleza dhamira ya mapenzi ambapo Bahati alitaka kujua kama Iddi anampenda kwa dhati. Bahati aliandika barua ya kumweleza Iddi kuwa sasa yeye bahati yupo katika mapenzi ya dhati na Mwinyi na anamuomba Iddi asimsumbue kwani hivi sasa wapo katika mipango ya harusi yao. Barua hiyo ilimtesa Iddi hata asijuwe ni jambo gani atafanya kwa sababu tayari alikwishafahamu

kwamba mipango yote aliyoipanga yeye na Bahati sasa imekufa. Hata hivyo, yaliyosemwa katika barua hiyo yalilenga kumpima Iddi kama kweli anampenda Bahati. Bahati alifahamu kuwa Iddi anampenda kwa sababu alikasirika baada ya kuisoma barua aliyomtumia. Kumbe Iddi hakukasirika kwa sababu alimpenda sana Bahati bali aliona dhahiri kuwa mipango ya kupata utajiri wa Mwinyi kupitia kwa Bahati ilikuwa ni ndoto tu isiyotekelezeka tena.

Taharuki ni mbinu nyingine ya kifani ambayo imetumika katika kuibua dhamira za kijamii katika riwaya ya Kiu ya Mohamed Suleiman. Mbinu hii imetumika katika upangaji wa visa na matukio ambapo mwanzo tu wa riwaya hii pameanza kitaharuki. Hali ya kumchelewesha msomaji kupata suluhisho la kile ambacho kinaelezwa katika riwaya kinamfanya msoamji kuwa na hamu ya kusoma zaidi kwani atataka kusoma zaidi ili apate mwisho wa tukio lake. Kwa mfano, mwanzoni mwa riwaya kunaelezwa kuwa Mwinyi anaishi kwa shida na kukosa raha licha ya kuwa yeye ni mtu tajiri. Jambo linaloezwa kuwa ndilo linalomnyima Mwinyi raha ni mapenzi yake kwa Bahati jambo ambalo aliona kuwa haliwezi kufanikiwa kutokana na yeye kuwa na ni Mzee na Bahati ni binti mdogo.

Mbinu nyingine za kifani zilizotumika katika kujenga dhamira za kijamii katika riwaya ya Kiu ni misemo, sitiari na tashihisi. Mbinu hizi za kifani zimetumika katika kusisitiza masuala mbalimbali yanayohusiana na dhamira za kijamii katika riwaya ya Kiu.

5.3 Hitimisho

Riwaya ya Kiu licha ya kuandikwa zaidi ya miaka 44 iliyopita lakini bado dhamira zinazoelezwa katika riwaya hii ni zimejaa uhalisia wa mambo ulivyo katika jamii ya leo ya Watanzania. Dhamira za usafi wa mazingira, mapenzi, wizi na magendo, umaskini na ujasiriamali ni dhamira zilizopamba moto katika Tanzania ya leo. Kwa mfano, kuhusu usafi wa mazingira, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania daktari John Pombe Joseph Magufuli alifuta sherehe za uhuru za tarehe 9 mwezi wa 12 mwaka 2015 na kuifanya siku hiyo kuwa ni siku ya usafi wa mazingira nchi nzima. Aliamua kuchukua uamuzi huo kwa sababu nchi ilikuwa imekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu unaosababishwa na uchafu wa mazingira.

Riwaya ya Kiu imesheheni dhamira ambazo zina uhalisia katika maisha ya leo ya jamii. Dhamira hizo ni pamoja ujasiriamali ambapo tunaona kundi la wanawake likijitokeza na kushiriki katika uzalishaji mali na kufanya biashara. Shughuli za uzalishaji mali husaidia katika kukuza kipato na kupunguza umaskini uliopo katika jamii. Dhamira hizi zimewasilishwa kupitia mbinu za matumizi ya barua, misemo, sitiari, tashihisi na taharuki.

Dokumen terkait