• Tidak ada hasil yang ditemukan

Utafiti huu ulihusu mada ya utafiti isemayo: Kutathmini mabadiliko ya usawiri wa mwanamke katika riwaya ya Utengano na Kamwe si mbali tena. Huu ni Utafiti Linganishi. Utafiti huu uligawanywa katika sura tano zifuatazo: Sura ya kwanza ilihusu Utangulizi wa jumla. Vipengele vilivyojadiliwa ni pamoja na; Utangulizi, usuli wa mada, tatizo la utafiti, Malengo ya utafiti (Lengo kuu na malengo mahsusi), Maswali ya utafiti, Umuhimu wa utafiti, Vikwazo vya Utafiti na utatuzi wake, Mipaka ya utafiti, Muundo wa tasnifu na Hitimisho.

Katika Utafiti, huu mtafiti aliongozwa na malengo ya aina mbili; Lengo kuu na malengo mahsusi. Lengo kuu lilikuwa ni: Kutathmini mabadiliko ya usawiri wa mwanamke katika riwaya ya Utengano na Kamwe si mbali tena. Malengo Mahsusi yalikuwa matatu: (i) Kufafanua usawiri wa mwanamke katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena. (ii) Kufananisha usawiri wa mwanamke katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena (iii) Kutofautisha usawiri wa

mwanamke katika riwaya za Utengano na Kamwe si mbali tena. Sambamba na hilo utafiti huu uliambatana na maswali matatu ya msingi: (i) Ni kwa vipi usawiri wa mwanamke umejitokeza katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena? (ii) Ni kwa namna gani usawiri wa mwanamke umefanana katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena (iii) Ni kwa tofauti gani usawiri wa mwanamke umejitokeza katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena?

Sura ya pili ilihusu Mapitio ya Kazi Tangulizi na Mkabala wa Kinadharia. Kwa upande wa sura hii ilijumuisha mada ndogo ndogo zifuatazo; Utangulizi, Ufafanuzi wa Istilahi muhimu (mfano, Dhana ya Wahusika), Mapitio ya kazi tangulizi, Nadharia zilizotumika ni Ufeministi wa Kiafrika na Nadharia ya Fasihi Linganishi. Mwisho ni Hitimisho.

Sura ya tatu ilihusu Mbinu za utafiti. Katika sura hii vipengele vifuatavyo vilijadiliwa: Utangulizi, Maana ya mbinu za utafiti, Eneo la utafiti, na sababu za uteuzi wa eneo la Utafiti, Mbinu ya usampulishaji, Ukusanyaji wa data na Mbinu za ukusanyaji wa data, Mbinu za uchambuzi wa data zilitumika ambayo ni mkabala wa Kimaelezo, Zana / vifaa vya utafiti na mwisho ni Hitimisho.

Sura ya nne ilihusu Uwasilishaji, Uchambuzi na mjadala wa data za utafiti. Vipengele vilivyojadiliwa: Utangulizi, Usuli wa mwandishi – Said A. Mohamed, muhtasari wa riwaya ya Utengano na Kamwe si mbali tena, Uchambuzi wa usawiri wa mwanamke katika riwaya za Utengano na Kamwe si mbali tena.

Kwa ujumla kulingana na mada husika ambayo ni: Kutathmini mabadiliko ya usawiri wa mwanamke katika riwaya ya Utengano na Kamwe si mbali tena: Utafiti Linganishi. Mtafiti kwa kurejelea data zilizokusanywa na uchambuzi wake, riwaya hizi zimefanana kidogo (wastani wa asilimia thelathini) ukilinganisha na kutofautiana kwake (wastani wa asilimia sabiini) katika usawiri wa mwanamke. Hali hii imechangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo za kimazingira, kiwakati, hisoria, dini, siasa, uchumi na utamaduni. Sambamba na hilo uchambuzi wa utafiti huu uliongozwa na malengo mahsusi ya utafiti. Kwa muhtasari ufafanuzi wa malengo mahsusi hayo ni kama ifuatavyo:

5.2.1 Lengo Mahsusi La Kwanza

Lengo mahsusi la kwanza la Utafiti huu ilikuwa ni: Kufafanua usawiri wa mwanamke katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena. Lengo hili liliongozwa na swali la msingi la kwanza lisemalo: Ni kwa vipi usawiri wa mwanamke umejitokeza katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena?

Katika Utafiti huu, mtafiti alibaini kuwa riwaya mbili hizi teule zimemsawiri mwanamke katika hali mbili (chanya na hasi). Kwa mfano katika riwaya ya Utengano; Mwanamke amesawiriwa kama muhusika Mshauri mwema, Jasiri na mwenye kujitoa mhanga, Mwenye msimamo thabiti, Mlezi wa familiya, Mapenzi ya dhati, Muwajibikaji, Tabibu na daktari wa kienyeji, Ushawishi na Uchochezi, Mipango na Hadaa, Mlevi na Mgomvi / Mshari, Dhaifu na Masikini, Chombo cha starehe na Mtenda rushwa.

Kwa upande wa riwaya ya Kamwe si mbali tena, mtafiti aligundua mwanamke amesawiriwa katika hali / tabia zile zile mbili (chanya na hasi). Kwa mfano, Mwanamke amesawiriwa kama muhusika Muwajibikaji, Mtambuzi na Mwanahistoria, Mpenda dini, Huruma na mwenye Imani thabiti, Mwanamabadiliko, Msamehevu, Tabibu / daktari wa kienyeji, Mlezi wa familiya, Chombo cha starehe, Yatima na anayehitaji msaada, Jeuri, Kiburi na mwenye tama. Ni vyema mema yakafuwatwa na maovu yakaachwa.

5.2.2 Lengo Mahsusi la Pili

Lengo mahsusi la pili la utafiti huu ilikuwa ni: Kufananisha usawiri wa mwanamke katika riwaya za Utengano na Kamwe si mbali tena. Lengo hili lilikitwa katika swali la msingi lisemalo: Ni kwa namna gani usawiri wa mwanamke umefanana katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena.

Utafiti huu ulibaini kuwa, riwaya hizi teule katika kufanana kwa usawiri wa mwanamke umejitokeza kama ifuatavyo: Mwanamke amesawiriwa kama muhusika mwenye Mapenzi ya dhati, Msimamo thabiti, Muwajibikaji, Mlezi wa familiya, Tabibu / daktari wa kienyeji na Chombo cha starehe kwa mwanamume. Kwa makusudio hayo riwaya hizi pamoja na kwamba zimetofautiana kwa miaka (34) lakini bado kuna baadhi ya tabia chache zimeonekana kufanana kwa wastani wa asilimia thelathini (30%).

5.2.3 Lengo Mahsusi la Tatu

Katika utafiti huu, lengo mahsusi la tatu lilikuwa ni: Kutofautisha usawiri wa mwanamke katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena. Lengo mahsusi

hili liliongozwa na swali la msingi la tatu lisemalo: Ni kwa tofauti gani usawiri wa mwanamke umejitokeza katika riwaya teule za Utengano na Kamwe si mbali tena?

Kwa ujumla riwaya hizi zimetofautiana kwa wastani wa asilimia sabiini (70%) kaika kumsawiri mwanamke. Kwa mfano katika Utengano mwanamke amesawiriwa kama muhusika mshauri mwema, jasiri na mwenye kujitolea mhanga, ushawishi na uchochezi, mipango na hadaa, dhaifu na masikini, mtenda rushwa, mlevi, na mgomvi (mshari). Kwa upande wa riwaya ya Kamwe si mbali tena mwanamke amesawiriwa kama muhusika mtambuzi na mwanahistoria, mpenda dini, mwenye huruma na imani thabiti, mwanamabadiliko / mageuzi, yatima anayehitaji msaada, msamehevu, msomi (mwenye elimu), mwenye tama, jeuri na kiburi.

5.3 Hitimisho

Kwa kuhitimishia, tunaweza kusisitiza kuwa mwanamke ni muhusika binaadamu kama walivyo wanaadamu wengineo. Ni muhusika mwenye uwezo mkubwa wa kutenda matendo mbalimbali ambayo hugawanywa katika sehemu mbili kuu. Matendo mema (chanya) na matendo maovu (hasi). Mtafiti amegundua kuwa kuna tofauti baina ya usawiri wa mwanamke katika maisha ya zamani (riwaya ya Utengano ya mwaka 1980) na usawiri wa mwanamke katika maisha ya sasa (riwaya ya Kamwe si mbali tena, ya mwaka 2014) hadi sasa (2016). Kwa udhati kabisa tathmini ya tofauti ya usawiri huo katika riwaya hizi mbili yanaakisi na maisha ya sasa kwa kuhusisha na matendo ya jamii ya leo na kumfanya mwanamke aonekane amebadilika zaidi tofauti na zamani. Hii inamaanisha kuwa mwanamke ni muhusika anayekwenda sambamba na mabadiliko ya wakati, historia, imani na ushiriki au

ushirikishwaji wake, kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hali hii humfanya aendelee kuonekana ni mwenye thamani na kuhitajika.