• Tidak ada hasil yang ditemukan

2.6 Kiunzi cha Nadharia

2.6.2 Nadharia ya Uhistoria Mpya

Nadharia hii inahusishwa na athari za akina Raymond William (mfuasi wa Kimaksi) na Michel Foucalt. Uhistoria mpya unahusishwa na Wamarekani. Waingereza wameiita, Uyakinifu wa Kitamaduni, wakirejelea kitu kilekile. Wana Uhistoria Mpya wanaitambua nafasi kubwa na muhimu, inayochukuliwa na muktadha wa kihistoria katika kazi za fasihi. Nadharia hii imesaidia kutoa maelezo madhubuti ya miktadha ya fasihi kihistoria.

Ni nadharia ya kisasa na kimaendeleo inayohusishwa na tapo la wasomi wenye mwelekeo wa kilimbwende na ufufuo wa elimu na maarifa katika kazi ya sanaa, (Murfin, 1991 na Rice, 1993). Nadharia hii ni ya kimaendeleo inachangiwa na nadharia za hivi karibuni kama vile uchambuzi nafsia, mwitikio wa msomaji, ufeministi (Mc Gann, 1985). Nadharia hii ina mikabala mingi ndani yake. Mikabala hiiina mawazo ya kimsingi yanayounganisha mikabala hiyo ambayo ni:

Kwanza, kila tukio la kisimulizi, hutegemezwa kwenye hali changamano ya matukio ya Kiyakinifu. Pili, tukio lolote la kufichua, kuhakiki, kukosoa na hata kupinga huishia kuzitumia mbinu inazozipinga. Tukio hilo, huweza kutumbukia katika hali inayotaka kuzifichua au kukosoa. Tatu, kazi za fasihi na zisizo za fasihi huingiliana kimzunguko. Nne, hamna usemi wowote wa kibunifu au Kiyakinifu, unaoweza kuelekeza kwenye ukweli usiobadilika au unaoelekeza kazi ya binadamu isiyoweza kubadilishwa. Tano, mtindo wa kuhakiki na lugha inayokifu, kuuelezea utamaduni, unaopatikana katika jamii ya kibepari, huhusika katika uchumi wa kibepari unaouelezea. Mkazo mkubwa wa nadharia hiyo haupo kwenye tendo au kitendo cha kuisawiri historia au wakati uliopita, bali njia zinazoweza kutumiwa kuijenga au kuisawiri tena jana au historia (Wamitila, 2002).

Nadharia hiyo inashikilia kuwa, kazi za kifasihi zinaweza kusomwa kwa njia ifaayo, zikiwa na kani za kihistoria, zinazosababisha au zinazotawala hali fulani pamoja na kuangaza mazingira yanayobadilika, ingawa ni vigumu kuyajua mambo yote tupasayo kuyajua na tunayohitaji kuyajua kuihusu awamu hiyo, aghalabu mazingira tuliyomo au hali ya jamii ya leo inavyoathiri kwa kiasi kikubwa, tunavyosawiri tamaduni za wakati uliopita.

Dhana ya pili ni uyakinifu wa kiutamaduni ambao ni muundo unaogeukageuka. Hii ni dhana inayoiangalia fasihi kwa jicho la matukio fulani ya kiutamaduni. Dhana nyingine ni mabadilishano, dhana hii inahusishwa zaidi na mwanadharia Stephene Greenblatt (1988), na dhana ya mwisho ni mzunguko unaoyarejelea mageuzi au matukio, itikadi za kiutamaduni, jinsi zinavyotoka sehemu moja hadi nyingine, kwa mbadilishano.

Kutokana na vipengele na misingi ya nadharia hii ni wazi kwamba vimesaidia kwa yale ambayo yalidhamiriwa na utafiti huu, Kwa kuwa mawazo mengi yanayojadiliwa katika nadharia hii, yana mlandano na madhumuni ya utafiti wetu, mawazo hayo ndiyo yametusaidia sana katika uchambuzi na uchanganuzi wa data na kisha kubaini kile tulichonuia katika utafiti huu.

Pia nadharia hii ina uwezo wa kueleza yale ya kidesturi na kimila na mambo mengi kadha wa kadha yanayohusika nayo. Kwa mujibu wa mawazo na misingi uhistoria mpya tumeweza kubaini haya;

(a) Ni muhimu kufanya uchunguzi juu ya jamii halisi inayozalisha fasihi katika mazingira na wakati maalum (Butler, 1987). Utafiti wetu umefanyika katika jamii ya Wanyakyusa kwa kuchunguza tondozi zao, katika utafiti huu tumegundua kuwa tondozi za nyakati mbalimbali zimeyasawiri matukio ya awamu husika, hivyo hata maudhui yaliyojitokeza katika tondozi hizo ni yale yaliyokuwa yakitendeka katika jamii kwa uhalisi wake.

(b) Matakwa ya kijamii na kisiasa huathiri utoaji na upokezi wa kazi ya fasihi (Greenblatt, 1980). Kila mtunzi huwa ameathiriwa na mazingira, na athari hizi hazina budi kujitokeza katika utunzi wake. Katika utafiti huu tumegundua

kuwa wasanii wengi wa tondozi wameathiriwa sana na mazingira ndipo sasa nyimbo zao huwa na michomozo ya kijamii na kisiasa ya awamu hiyo.

(c) Kila utungo wa fasihi ni zao la jumuiya fulani, ambapo kiwango cha utamaduni wake, maendeleo ya fasihi yake kwa jumla na miongoni mwa mambo mengine yote, huchangamana na kuupa utungo fulani mfumo wake maalum. (Davis, 1986) yeyé anasema, Maendeleo ya historia hufafanua mahusiano ya watu katika awamu maalum kwa mujibu wa mipaka ya yale yanayotiliwa maanani na utamaduni.

(d) Fasihi haiwezi kutengwa na historia inayohusika nayo kwani inarejelea vitu vilivyomo kwenye mazingira. Foucalt (1972) akiunga mkono hoja hii anaeleza kuwa umuhimu wa yale yanayosemwa katika awamu fulani huwa tofauti na yale ya awamu nyingine. Hii ni kusema kuwa maudhui ya awamu fulani ni tofauti na yale ya awamu nyingine.

Nadharia hii imeuwezesha utafiti kubainisha misingi ambamo maudhui fulani yamejikita, kwasababukazi fulani ya fasihi ni zao la amali za wakati na mahali fulani katika maendeleo ya kihistoria. Utafiti huu umechambua maudhui kwa kuzingatia aina za tondozi na namna zilivyosawiri matukio ya awamu hiyo kulingana na mahitaji ya jamii ya wakati huo. Hii ni kwasababu katika kila jamii utoaji wa ujumbe husimamiwa, kuteuliwa na kupangwa kulingana na utaratibu fulani (Foucalt, 1972). Utafiti huu umechukulia fasihi kama tendo la kijamii linalosimamiwa kwa mujibu wa wakati. Hivyo imebainika kwamba tondozi ni kazi ya sanaa inayotolewa na kuhifadhiwa chini ya masharti maalum ya kijamii, na maudhui yake yanajikita katika muktadha maalum wa kihistoria.

Nadharia hii pia imesaidia uibushaji wa dhana ya mabadiliko kwa kuwa uhakiki wa kihistoria huelezea yale yaliyo bayana na ambayo yana athari kuu katika mazingira na wakati maalum. Hivyo tumegundua kuwa maudhui yaliyokuwa yanajitokeza yalikuwa yanajikita katika awamu fulani maalumu ya kihistoria. Utafiti huu umechunguza tondozi za awamu mbalimbali zinavyosawiri maisha halisi ya Wanyakyusa katika tondozi za wakati husika na mazingira ya kihistoria. Mathalani katika mkabala kama huu baadhi ya tondozi zilieleza matukio muhimu kama vile uhuru, Azimio la Arusha na vita vya Kagera.

Hii ni kwasababu fasihi huathiriwa na uhalisi uliopo, pia ufafanuzi wa kazi fulani ya fasihi hauna budi kuwa na mwelekeo na maendeleo, sambamba na vipengele vingine vya maisha ya jamii. Hivyo katika utafiti huu tumegundua kuwa katika uelewaji wa kazi ya fasihi inampasa mtu kuelewa muktadha wa kihistoria ambamo kazi ya fasihi hutokea.

Wanauhistoria mpya wanadahili kuwa, kazi za kifasihi ni matokeo ya uhusiano changamano za kimwingiliano matini na wala siyo kazi zinazotokana na ubunifu wa msanii peke yake. Wanasema kuwa, mwingiliano matini uliopo unapatikana kwa kuiangalia jamii pamoja na utamaduni. Kwa hiyo ni kosa kuitenga fasihi na miktadha ya kijamii kwa kuwa maingiliano kati ya muktadha huo na kazi ile ni muhimu katika kuipa sura na uhai kazi inayohusika, (Wamitila: 2002). Dhana za kimsingi za nadharia hii ni, “Usukaji, ambayo hutumia kurejelea hali ya kuyachukua matukio na

matendo ya kihistoria na kufanya sehemu ya matukio ya hadithi au kazi ya kifasihi kama ilivyojitokeza katika baadhi ya tondozi kama vile vita vya Kagera, Idi Amin dada nakadhalika ukisoma ukurasa wa 146-148.

Nadharia hii imemsaidia mtafiti katika malengo yote mawili yaliyonuiwa na utafiti huu. Kwanza imeeleza taathira za kijamii na kihistoria zinazoleta mikinzano katika hatua za ukuaji kimaudhui. Pili katika vipengele vya fani, nadharia hii, imemsaidia mtafiti kueleza dhana ya utendaji hususani katika mavazi, lugha inavyofungamana na utamaduni na kipengele cha mtindo kimefafanuliwa kwa kutumia nadharia hii.

Udhaifu wa nadharia hii ni kuwa inakuwa ni kazi ngumu labda isiyowezekana kuusaka ukweli kwa usomaji wa kihistoria, kwa kuwa uchunguzi wowote unaathiriwa na sababu za kiuchunguzi, haiwezekani kuwa na sifa za ubaki, za kimwingiliano matini, ambao unapatikana kwa kuangalia jamii pamoja na utamaduni. Muktadha wa kijamii huweza kuzipuuza sifa za kiujumi za kazi fulani za kifasihi, na huu ni udhaifu wa nadharia za kisoloshojia kwa jumla. Kwahiyo haiwezekani tukayajua mambo yote tuyapasayo na tunayohitaji kuyajua kuhusu awamu hiyo, aghalabu mazingira tuliyomo au hali ya jamii ya leo inaathiri kwa kiasi kikubwa jinsi tunavyozisawiri tamaduni za wakati uliopita.