• Tidak ada hasil yang ditemukan

Kazi Zinazofafanua Dhana ya Tondozi

Finnegan (1970), anaeleza kwa jumla kuhusu tondozi katika jamii za Kiafrika. Anasema tondozi ni aina ya ushairi inayotumika kusifu watu, hususani watawala, wanyama, vitu au mafanikio fulani ya kivita. Anasema kuwa, msingi mkuu wa tondozi ni majina ya kusifu. Finnegan (k.h.j) anasema, tondozi huweza ‘kutondozwa’ katika shughuli maalumu za kijamii, na huendana na maadili ya jamii hiyo. Pia tondozi hizo huweza kutondozwa kwenye sherehe za jando na unyago, harusi, na wakati mwingine, kwenye muktadha wa mazishi ingawa si nyingi. Finnegan (1970) akimnukuu Bowers (1965) anasema, katika jamii ya watu wa kaskazini mwa Sierra Leone na maeneo mengine ya Afrika Magharibi, tondozi ziliambatana na ngoma na marimba, Bowers (k.h.j) anasema kuwa,zilikuwapo tondozi zilizoghanwa na wanawake na nyingine zilighanwa na wanaume, ingawa nyingi zilighanwa na

wanaume. Finnegan (1970) anasema, tondozi nyingi zina sifa ya Kiistiara na kuwa ni tungo zilizoenea sana Afrika na ndizo zinazotumia ishara nyingi zaidi kuliko aina zote za tungo za kishairi.

Maelezo ya Finnegan yamesaidia, kutupa mwanga kuhusu asili ya tondozi na muktadha wa matumizi ya tondozi.Ingawa maelezo yake ni ya jumla mno, yanatoa mwelekeo mzima kuhusu tondozi. Maelezo hayo yametoa mwanga kwa ajili ya utafiti wetu. Hata hivyo, maelezo hayo hayatatui tatizo la utafiti huu ambalo lilijikita katika kuchunguza mabadiliko ya tondozi za Wanyakyusa.

Ndamugoba (1987) anazungumzia utanzu wa sifo. Anasema kuwa, sifo ni utungo wa kishairi unaoelezea sifa. Sifo za Kihaya zilikuwa za aina mbili, sifo zisizoimbwa (zinaghanwa) na sifo zinazoimbwa (zisizoghanwa). Sifo zisizoimbwa zimegawanyika katika makundi mawili yaani majigambo, sifo za kujisifia mwenyewe na tondozi, sifo za kumsifia mtu au kitu kingine. Kwa ujumla andiko la Ndamugoba limetunufaisha sana katika utafiti wetu kwa kutusaidia kubaini utofauti wa kimaudhui na kifani wa tondozi. Hata hivyo Ndamugoba (1987) hakushughulikia mabadiliko yanayojitokeza katika sifo, kwahiyo utafiti huu umeziba pengo hilo lililoachwa na Ndamugoba.

Mulokozi (1996), anaelezea utanzu wa sifo kuwa ni masimulizi ya kishairi na huhusu matukio muhimu kihistoria, au jamii, huelezea habari za ushujaa na mashujaa, huwasilishwa kwa kughanwa na ala ya muziki, hutungwa papo kwa hapo na huambatana na wahusika. Kwa upande wa tondozi, ambazo pia, ameziita pembezi, Mulokozi anasema, kuwa ni kitanzu cha sifo ambacho husifia mtu mwingine.

Anasema, kitu chochote chaweza kusifiwa na sifa zake, mara nyingi ni za kiistiara (allegorical) zilizokusudiwa binadamu. Kama ilivyo kwa Finnegan (1970) ametoa picha ya jumla kuhusu tondozi tena kwa ufupi. Ni wazi kabisa kuwa, alichokizungumza Mulokozi hakijatatua tatizo letu katika utafiti huu lakini kimetupa picha kuhusu dhana ya tondozi na dhima zake.

Groenewald (2001) anasema kuwa, sifo za kijadi zina dhima ya kuonesha umuhimu wa mshairi juu ya mambo ya zamani. Anasema, sifo ziliunganisha kizazi kilicho hai na kile cha wahenga, anatolea mfano sifo za kikabila huko Afrika ya Kusini, zilizokuwa zinaghanwa katika harusi na matambiko. Sifo hizo zilikuwa na dhima ya kuwaunganisha wanajamii walio hai na mizimu ya mababu zao (wahenga). Wazo hilo la kuunganisha vizazi, lilikuwa linadhihirika katika ulimwengu wa kidini zaidi. Sifo hizo zilitumika pia wakati wa vipindi vya hatari katika kabila la Wazulu ili kuleta muunganiko wa kizazi kilichoishi na kile cha mizimu, ambao ulikuwa ni muhimu sana. Sifo zilighanwa pia wakati wa mabadiliko, hasa kupevuka au katika ndoa, wakati huo mizimu ilifanywa kifamilia, hata wakati wa kupotelewa na watu (kifo) au mali, wakati mtu akitaka kusafiri au msichana akiwa kwenye maandalizi ya kuolewa.

Katika nyakati hizo, sifo zilikuwa na umuhimu sana kama daraja la mawasiliano kati ya jamii inayoishi na ile ya mizimu. Njia ya kuwasiliana mizimu na wahenga ilikuwa ni kutongoa sifa zao hasa wakati kafara imetolewa. Mizimu na machifu (watawala) walikuwa na kazi ya kulinda maslahi ya jamii kiroho na kimwili. Kwa hakika maelezo haya ya Groenewald yametufaa sana katika utafiti huu kwa sababu yanaeleza namna ambavyo sifo na tondozi zikiwemo zinavyojitokeza katika

miktadha mbalimbali ya kijamii. Maelezo yake pia yanatupa mwanga kuwa sifo ni zaidi ya kuburudisha. Sifo zimebeba amali za jamii za awamu zinazohusika.

Mphande (2004) anasema, ushairi wa sifo ni kati ya njia zinazoifafanua fasihi ya Afrika ya kusini kwa sababu, sifo zina umuhimu katika kutoa ufafanuzi wa siasa na fasihi ya watu wake. Utanzu wa sifo za kijadi unaoitwa Izibongo kwa Wazulu, ni sanaa ya kisiasa inayopatikana katika jamii za Afrika ya Kusini, katika uchunguzi wake alitaka kuelewa namna sifo za Wangoni wa Afrika ya kusini zinavyoeleza historia ya Wangoni hao chini ya utawala wa Zwangedaba. Kwao, dhima kuu, ya sifo ni kuhifadhi na kurithisha utambulishi wa jamii, wakati huo huo, zikiburudisha hadhira. Katika kazi hii ya Mphande tumepata mawazo ambayo Wazulu wanayaamini na ambayo yamejitokeza katika sifo zao yakielezea ujumi wao. Hivyo kazi hii imekuwa ni mwongozo mzuri wa kile tulichokuwa tunakitafuta katika utafiti wetu.

Linden (2010), anasema, ushairi wa sifo na nyimbo, ni kigezo cha kupima kuaminika kwa vizazi visivyo rasmi na vilivyopita kwa sababu, ushairi wa sifo ni wa kuaminika na unatunza historia halisi kwa muda mrefu. Linden anasema kuwa, ndani ya ushairi wa sifo tunapata yale mambo ambayo jamii inayaona kuwa ni ya msingi na inayakubali. Maelezo haya ya Linden yametusaidia sana tulipokuwa tunachunguza tondozi za miaka ya zamani kwa kuwa ndani ya tondozi hizo tumeelewa, maudhui ya jamii za nyakati tofauti ambayo pia ni lengo mojawapo la utafiti huu.

Samwel (2011) akizungumzia utanzu wa sifo, akirejelea kabila la Wahaya, anazungumzia dhana ya Ebizina akiwa na maana kuwa, ni tondozi ambazo huweza

kuambatana na ngoma. Anasema kuwa, lengo kuu lilikiwa ni kuonya, kuelekeza na kusifia. Anasema, tondozi za Ebizina, hutendwa na wanawake, wakisifia waume zao. Wanaume nao wana tondozi zao, zinazojulikana kama, (Ebishambagizo). Samweli (k.h.j) anasema, utungo huo unafanana na majigambo (Ebyebugo) kwa maana ya kuwa, zote mbili hutumia sauti za kughanwa, ingawa tondozi humsifia mtu mwingine, majigambo mtu hujisifia mwenyewe. Samweli, akimnukuu Ndamugoba (1987:4) anatoa maelezo tofauti kidogo, kuhusu tondozi, anaposema kuwa, Ebizina hazikughanwa bali ziliimbwa, hivyo anamaanisha kuwa kitanzu hiki kinaimbwa ili kusifia mtu kuonya, kukosoa, kuburudisha na kutoa elimu ya jumla ya maisha.

Katika maelezo yake, Samweli ametaja tondozi za Mukama, ambapo, anayesifiwa, ni mukama, kutokana na matendo makuu ya kishujaa aliyoyafanya na tondozi za ng`ombe kinachosifiwa ni ngo`mbe. Akimnukuu Rubanza (1994) na Hodza na Fortune (1979) anasema, ingawa kinachosifiwa ni wanyama, huwa ni kiwakilishi cha tabia za binadamu, hivyo ng`ombe huchukuliwa kama ishara tu. Maelezo hayo ya Samweli, katika utafiti wake uliozungumzia majigambo yametufaa sana kwa sababu yametupa mwanga kuhusu sifo za kijadi. Pia utafiti wake umekuwa msaada na mwongozo katika utafiti huu. Hata hivyo maelezo yake, yamekuwa msaada hata kututofautishia kati ya majigambo na tondozi ingawa haikuwa lengo lake kuzungumzia tondozi. Kwa maelezo ya Samweli, tondozi huwa zinaimbwa na wakati huo pia huwa zinaghanwa. Maelezo haya yametusaidia pia kujua kuwa tondozi huwa zinaghanwa na kuimbwa.

Herman (2012) ameshughulikia sifo za kijadi za sherehe za harusi za jamii ya Wahaya, alisema, sifo ni tungo za kishairi ambazo husifu watu, wanyama, mimea au

hata vitu vingine. Baadhi ya sifo, huwa zinakashifu na kukejeli. Anasema, sifo nyingi za kijadi, hurejelea sana watu maarufu katika jamii inayohusika, anasema kuwa shida anazokutana nazo mtu, ndizo huibua sifo hizo. Akielezea zaidi ushairi wa majigambo ameeleza dhima ya sifo hizo za kijadi kuwa ni kuendeleza ushujaa, kuendeleza mfumo dume, kutunza kumbukumbu ya mambo ya jamii, kuwezesha mazungumzo ya kijadi, kuburudisha hadhira, ishara ya kuridhika, kuonesha moyo wa shukrani na kujitambulisha kinasaba. Herman (k.h.j), yeye anatupa mwanga kuhusu sifo za kijadi, ingawa yeye kajikita katika majigambo, lakini tondozi na majigambo ni kama mapacha wa mifuko tofauti, kwa hiyo kupitia majigambo, tunapata picha kuhusu tondozi.