• Tidak ada hasil yang ditemukan

Mzee Prof. Dkt. Sheikh Sengo, alimweleza mtafiti kuwa, dhanna au chimbuko la nadharia yoyote ile ni matatizo. Kwanza kunakuwa na tatizo. Tatizo linapowasumbua wanajamii kwa muda, mwanajamii mmoja au jopo la wanajamii wakakaa na kuanza kusugua vichwa kwa kutafuta ufumbuzi wa tatizo hadi wakapata ufumbuzi wake. Njia ya kutatua tatizo hilo inapotumika mara ya kwanza na kuleta mafanikio na mara ya pili, na mara ya tatu, na kuendelea, basi hii huitwa NADHARIA (Sengo, 2012 mazungumzo).

Utatuzi wa tatizo hili hauwezi kuwa ni wa jumla. Utatuzi huu utategemea mazingira halisi na wakati halisi. Mzee Sengo alifafanua kuwa tatizo linalotatulika masika, si sawa na linalotatulika wakati wa kiangazi. Tatizo la jangwani haliwezi kutatulika sawa na lile la misitu ya Kongo (Berry, 2009).

Katika taalimu ya mitishamba, mizizi ya mitishamba ya Ubunguni haiwezi kutibu ugonjwa ule ule Ukwereni. Mizizi ya Ubunguni itatumika kutibu Ubunguni na mizizi ya Ukwereni itatumika kutibu Ukwereni. Ulimbe wa taalimu hii unakwenda ndani zaidi ya miti hiyo. Chumvi chumvi za udongo wa Ubunguni si sawa na zile za Ukwereni. Ukwereni kuna chumvi chumvi zaidi. Je, taalimu hii unahitaji Mzungu kumfundisha Mbungu? Huu ni ukweli.

Dhanna ya nadharia imejadiliwa na kufafanuliwa kijuu juu na wanazuoni wengi. Kati yao ni kama (Kiango na Wenzake 2006; Ogechi na wenzake 2008; Wamitila 2002; Wamitila 2008). Katika ujumla wao wanakubaliana kuwa nadharia ni jumla ya dhanna, nyenzo, kauli, ushauri, mapendekezo, mawazo, maelezo au mwongozo mkuu uliopangwa ili kusaidia kueleza, kutatua au kuelekeza jambo fulani. Wanazuoni wote wanakubaliana kuwa nadharia ni nyenzo katika kumwongoza mtafiti. Mtafiti katika utafiti huu, pamoja na maelezo yake hapo juu amepiga mbizi kilindini, hivyo, katika utafiti wa kufuwawa kwa miiko na kupotoka kwa maadili, mtafiti ametumia nadharia katika kupambanua na kueleza nia kuu ya utafiti ambayo ndiyo tatizo la msingi lililotafitiwa.

Nadharia si imani wala maelezo ya kawaida. Haya ni maelezo kuntu juu ya vipengele muhimu vya sanaajadiiya vinavyopaswa kuzingatiwa na kila mwanasanaajadiiya wakati wa kuhakiki, kuandika, kuzungumza, kusikiliza au kutafiti kazi za sanaajadiiya. Hili ni zao la tafakuri nzito, utafiti, uchunguzi, utazamaji na upembuzi wa kina na wa muda mrefu (Ogechi, 2008) na kwa mujibu wa mtandao wa wikipedia (imepakuliwa 1/2/2011). Nadharia ni mwavuli wa wanataalim katika kukabili kusikiliza, kusoma au kuandika kara mbalimbali za sanaajadiiya kwa kuzingatia njia

mbalimbali muhimu za kifalsafa na jinsi mtafiti au msemaji atakavyotafsiri maana za dhanna mbalimbali.

2.2.1 Mawazo ya Jumla Kuhusu Nadharia

Musau (2002) anasisitiza kuwa nadharia huchochea uhakiki wa kitaalimu kwa kuibua maswali ya kisayansi ambayo huimarisha tabia ya udadisi ya kusaka ukweli. Mtafiti anaona na kukubaliana na Musau kuwa, miiko katika sanaajadiiya inahitaji maelezo kuntu ambayo kwayo yatawasaidia Wabungu na wanajamii wengine Watanzania na Afrika kwa ujumla wake kuweza kutalii kwa mzamo athari chanya za kusaka ukweli wa miiko uliomo katika jamii husika. Athari ambazo zitaifanya jamii ya Wabungu kuweza kuulinda utu wao dhidi ya kukengeuka kwa maadili ya watu wazima, vijana na watoto katika malezi na vita dhidi ya uguberi, ufisidi na ufisadi unaoikabili jamii ya Wabungu. Maadili mema ni utu wa mtu.

Kama ilivyo kwa wanasanaajadiiya watangulizi (Nchimbi, 1979; P’Bitek, 1972; Sengo, 2007), pia mtafiti ana wasiwasi kuwa Waafrika wanaiacha miiko yao kwa kutabii utamaduni wa wageni, huu ni ugonjwa mbaya sana. (Nchimbi, 1979) anasema;

“Humpumbaza Mwafrika, hata akaacha kutumia akili yake; akaacha kuuthamini utu wake; Uafrika na hata weusi wake; Badala yake, Anajichukia mwenyewe, Utu wake, Uafrika na hata rangi yake” (Nchimbi, 1979).

Utu wa Mwafrika, utu wa Mbungu unakabiliwa na ugonjwa wa kutabii mila, tamaduni, maadili, ustaarabu, miiko na falsafa za Wazungu na kuukana UTU wa Mbungu.

Kama ada, miiko katika sanaajadiiya inahitaji maelezo kuntu ambayo kwayo yatawasaidia Wabungu na wanajamii wengine Watanzania na Afrika kwa ujumla wake, kuweza kutalii kwa mzamo athari chanya za miiko. Athari chanya ni athari ambazo zitaifanya jamii ya Wabungu na ya Watanzania kwa jumla kuweza kuulinda utu wao dhidi ya kukengeuka kwa maadili ya watu wazima, vijana na watoto katika malezi na vita dhidi ya uguberi, ufisidi na ufisadi unaoikabili jamii ya Wabungu. Maadili mema ni utu wa mtu.

Nchimbi (1979) katika shairi lake anashadidia matatizo ambayo Waafrika wengi wanakabiliana nayo ambayo anayaita ni ugonjwa mbaya sana. Katika beti hizi anasema:

“Ugonjwa unawanasa Waafrika wengi, Ndani na nje ya Afrika;

Ni ugonjwa uambukizao sana.

Unamshambulia Mwafrika, alikotoka, Makuu aliyofanya,

Na vikubwa alivyovivumbua! Humpumbaza Mwafrika

Hata akaacha kutumia akili yake; Akaacha kuuthamini utu wake; Uafrika na hata weusi wake; Badala yake,

Anajichukia mwenyewe, Utu wake,

Mtafiti anashadidia mawazo ambayo (Nchimbi, 1979) anawakumbusha Wabungu wote. “UTU wa Mwafrika”. Mbungu kama Waafrika wengine, ana ugonjwa mbaya sana na huu si mwingine, bali ni ugonjwa wa kutabii mila, tamaduni, maadili, ustaarabu, miiko na falsafa za Wazungu na kuukana UTU wetu kama Waafrika, Watanzania – Wabungu, (P’Bitek, 1972) naye anashadidia maneno haya na anasikitishwa kuona kuwa Waafrika hawapendi Uafrika wao na wanataka kujibadili kuwa kama Wazungu. Wanaukana Uafrika wao na kusahaku kuwa, Kila Jamii ina Ujumi Wake.

2.2.2 Matatizo ya Nadharia

Mtafiti anaona kuwa, kuna nadharia nyingi sana ambazo zinafafanua mambo mengi yanayofanana. Kwa mfano nadharia za Marx zinatumika katika kuelezea masuala ya uchumi, utawala, utamaduni n.k. Wingi wa nadharia ni hatari sana hasa kwa watafiti na watumiaji kama wanataalimu wachanga katika nyanja ya utafiti. Hali hii inapigiwa mbizi na (Ogechi, 2008; Musau, 2002; Berry, 2009). Kwa upande mwingine, kuna shida ya kuwa na nadharia kuu chache zinazofafanua vipengele vingi. Hali hii inaleta ugiligili ambao unaweza kumchanganya mtafiti wakati wa uchambuzi wa data.

Nadharia nyingi zina asili ya nchi za kimagharibi. Kwa hali hiyo zinaendana na mazingira, utamaduni, uchumi na hisia za kimagharibi. Kwa hiyo mtafiti anaona bila shaka yoyote, nadharia za aina hii haziwezi kukidhi mahitaji ya kujadili na kufafanua athari za kufuwawa kwa miiko ya jamii ya Wabungu, kauli hii inakubaliana na kauli ya (Musau, 2002; Sengo, 1978; Sengo, 2009) pamoja na mazungumzo ya mtafiti na Mzee, Prof. Dkt Sheikh. Sengo yanayohusu dhana ya nadharia.

2.2.3 Hitimisho

Mtafiti anahitimisha kwa kusema kuwa, nadharia zina nafasi muhimu sana katika kubainisha ukweli na utu wa Mbungu. Nadharia zitapembuwa na kupepeta ili kubaki na kilicho bora kwa matumizi ya jamii ya Wabungu. Kutokana na maelezo juu ya dhana ya Nadharia mtafiti amezama na kuangalia kwa undani nadharia zifuatazo;