• Tidak ada hasil yang ditemukan

Miiko ni kama sheria, kwa hali hiyo sheria ni nyingi kulingana na shughuli za wanajamii. Katika jamii ya Wabungu, licha ya makundi mengi ya miiko yaliyobainishwa na mtafiti, hapa mtafiti anajumuisha miiko mingine mchanganyiko ambayo aliikusanya na kuijadili kidogo.

5.30.1 Ni Mwiko Kujinyonga

Wabungu wanaamini kuwa kujinyonga kunarithiwa. Mtu akijinyonga, hali hii itaendelea kuwapata hata watoto, wajukuu na vitukuu. Ili kuleta hali bora ya maisha ya watu. Kijiuwa kwa kutumia njia yoyote ile kama kunywa sumu kujitundika kwa kamba au kujihatarishia maisha ili mtu afe ilihesabiwa kuwa ni mwiko mkubwa katika jamii. Kila mtu ana haki ya kuishi. (Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977). Watafitiwa walieleza kuwa mwiko huu ulikusudia kujenga maadili yanayothamini utu na uhai wa mtu mmoja mmoja au jamii nzima ya Wabungu.

5.30.2 Ni Mwiko kupakaa Mafuta Kuanzia Miguuni Kwenda Kichwani

Jamii ya Wabungu iliamini kuwa miguu ingawa ni sehemu ya mwili, ni michafu hata kama umeoga. Wakati huo watu hawakuwa wakitumia viatu kama sasa na kwa hali hiyo mara baada ya kuoga bado waliendelea kukanyaga chini. Kwa hali hiyo, kama mtu alianza kupakaa mafuta kuanzia miguuni, basi uchafu kutoka miguuni ulipandishwa hadi usoni ambako ilikuwa ni rahisi kwa mtu huyu kusogeza taka hadi kuingia kinywani bila kujua na kusababisha maradhi ya kuharisha. Kwa hali hiyo watu walipaswa kujipakaa mafuta kuanzia kichwani hadi miguuni.

5.30.3 Ni Mwiko Kushona Nguo Mwilini Ukiwa Umevaa, Unajitabiria Kifo Wabungu waliamini kuwa maiti hushonewa sanda na kufunika mwili wote.. Kushona nguo mwilini ni sawa na mtu kujifananisha na maiti, wakati anaposhonewa sanda kwa mazishi. Kwa hivyo, ingawa kifo ni amri ya Mungu, lakini si vyema kwa aliye hai kujifananisha na maiti. Pia ni wazi kuwa nguo inayoshonwa mwilini haiwezi ikashoneka vizuri. Kushona nguo mwilini kunaweza kusababisha kujishona au

kujichoma na sindani na kuleta madhara makubwa mwilini. Mwiko huu una umuhimu kutekelezwa ili kuepuka madhara kwa mshonaji na nguo inayoshonwa.

5.30.4 Ni Mwiko Kukoroga Chakula kwa Kisu, Walaji Wataumwa Tumbo la Kukata na Kuharisha Damu

Watafitiwa walieleza kuwa ni mwiko kukoroga chakula kinachopikwa kwa kisu au kitu chenye ncha kali. Wabungu walitumia vyungu kupika chakula. Kwa maana hii kukorogea kisu ilikuwa ni sawa na kunoa kisu kwa kutumia udongo wa chungu. Unaponoa kisu vipande vidogo vya madini yaliyotumika kutengenezea kisu, huchanganyika na chakula na hivyo kuleta madhara kwa mlaji wa chakula hicho. Pia ilikuwa ni hadhari kwa uharibifu wa vyombo vya kupikia kama sufuria na vyungu. Wakati wa kukoroga chakula kilichomo katika sufuria au chungu kikiwa cha moto ni rahisi kutoboa. Mwiko huu unaweza kukubalika kwa vile kisu sio kifaa halisi cha kukorogea chakula.

Mtafitiwa Zazi alifafanua kwa kutoa mfano wa upembuaji wa mchele. Mtu anapopembua mchele mawe yote huzama na kutuama chini ya sufuria. Kama mtu atatumiya kisu au kitu chenye ncha kali kukoroga, mawe na mchanga hauwezi kupata msukosuko wa kutosha kuzamisha. Hali hii inaweza kusababisha chakula kuliwa kikiwa na mawe na kusababisha matatizo ya kidole tumbo kujaa mawe au mchanga.

5.30.5 Ni Mwiko Kwenda Usiku Kisimani au Mtoni Kuchota Maji

Mwiko huu umechukulia maeneo ya kisimani kuwa mara nyingi huwepo mabondeni, mbali na makazi ya watu. Watafitiwa walieleza kuwa kwa vile wakati wa usiku huwa

hakuna nuru si rahisi mtu kuweza kuona kijacho na kirudicho. Kwa mfano, mtu anaweza kukanyaga nyoka na wadudu wengine ambao ni hatari na wanaweza wakaleta madhara kwa afya ya mtu. Pia kama mtu ataangukia majini usiku ingekuwa ni vigumu kupata msaada kwani watu wengi hawapiti au kwenda kisimani. Wabungu waliamini kuwa chemchem zinatoa maji mengi usiku kwa hiyo kama mtu atakwenda kisimani atafanya maji yasitoke ya kutosha.

Kwenda kisimani usiku pia kulikuwa na mchango mkubwa juu ya usafi wa maji kisimani. Kama mtu atakwenda kisimani usiku angeweza kuyachafua maji kwa urahisi kwa sababu ya uhafifu wa mwanga. Pia inawezekana watu waovu wakamvamia mtu na kumhujumu pasi na kupata msaada kwa vile eneo la kisima limejitenga na nyumba. Inawezekana pia mtu akaingia shimoni au kukanyaga miiba . Aidha imeelezwa kuwa upo uhusiano kati ya eneo la vianzio vya maji na mashetani wanapenda kukaa maeneo hayo hasa nyakati za usiku. Maelezo hayo kwa kiasi yanakubalika ingawaje sio mara zote kuwa mtu akaenda kisimani atakutana na shetani, bali kuna madhara mengine kama yalivyoelezwa na watafitiwa kuwa yanaweza kumpata mtu. Mwiko huu unachangia harakati za utunzaji wa ikolojia ya vyanzo vya maji, chemchem, visima au mito.

5.30.6 Ni Mwiko Kwenda Dukani Kununua Chumvi Usiku

Kwa asili shughuli za Wabungu ni kilimo, uvuvi na uwindaji. Kutokana na shughuli hizi, Wabungu walikula mara baada ya kurudi nyumbani. Chakula kililiwa jioni kabla ya giza. Kwa hali hiyo maandalizi ya kupika chakula yalifanywa mapema zaidi. Maandalizi ya mapema ya chakula yaliendana na kuwepo kwa viungo kama chumvi. Ilikuwa ni tabia mbaya kwa mtu kwenda kwa jirani kuomba chumvi au

kwenda dukani kununua chumvi usiku. Watafitiwa walieleza kuwa mwiko huu ulilenga kuifanya jamii hasa ya Wabungu wanawake ambao ndio walioandaa chakula, wafanye maandalizi ya upishi mapema.

5.30.7 Ni Mwiko kuinamisha Kichwa na Kunywa Maji Mtoni, Utapigwa na Mkia wa Mamba

Mwiko huu ni onyo kwa Wabungu kuwa wasinywe maji mtoni au ziwani kwa kuinamisha kichwa. Hii ni kwa sababu ziwa Rukwa pamoja na mito yote inayoingia ziwani, ina mamba wengi ambao ni hatari kwa maisha ya wanadamu. Pia maji yana mchanganyiko wa mambo mengi ambayo yanaweza kuleta madhara kwa binadamu. Kama ilivyoelezwa kabla kuwa watu hufuwa nguo zenye kinyesi au wengine kwenda haja ndogo mtoni. Mtu kuinamisha kichwa na kunywa maji anaweza kuidhuru afya yake kwani hatajuwa ni kitu gani atakachokinywa. Vile vile msukumo wa maji unaweza kuongezeka na maji yakampalia mnywaji. Wabungu wanaamini kuwa kama mtu ana ugonjwa wa kifafa akianguka ndani ya maji, basi, maisha yake yanaweza kuishia hapo.

5.30.8 Ni Mwiko kuitika Wito Bila Kumwona Mtu Anayeita

Wabungu waliamini kuwa kama mtu ataitika wito bila kumwona mtu ambaye anamwita, basi sauti yake itachukuliwa. Mtu huyu atakuwa zuzu. Wabungu waliamini kuwa kuna uchawi, na kwa uchawi watu waliweza kurogwa kwa njia ya kuchukuliwa sauti zao. Aidha mwituni ni sehemu ambayo kuna usalama mdogo kwa vile si mara nyingi kuweko na watu isipokuwa kwa wale wanaofanya shughuli maalum kama vile kulima na kukata kuni.

Eneo hilo pia liliaminika kukaliwa na viumbe wengine kama mashetani na majini. Aidha ni eneo la maficho ya watu waovu kama majambazi na waasi wengine. Maelezo ya wasailiwa juu ya kuwekwa mwiko huu yameeleza kuwa inawezekana watu waovu waliojificha mwituni wakamwita mtu kwa mwito mmoja ili wathibitishe kama huyo wanayemwita ndiye. Ili waweze kutekeleza uovu wao pale watakapobaini kuwa wanayemtaka ndiye aliyeitika.

SURA YA SITA