• Tidak ada hasil yang ditemukan

Nadharia ya Kila Jamii ina Ujumi Wake

Jamii za Kiafrika na watu wa bara lake lote wamekuwa kama kichwa cha mwendawazimu. Watu kutoka ughaibuni wanakuja katika bara la Afrika na hata katika jamii ya Wabungu na kuwabeza wazawa. Wazawa wamekubaliana na hali hii. Wabungu wamekuwa watu wa kupokea mila na desturi kutoka Uzunguni na kusahau kuwa na wao wana mila, utamaduni, nyimbo, mashairi, tambo mbali mbali na miiko kwa kulinda maadili ya jamii ya Wabungu. Suala la kulinda sanaajadiiya linashadidiwa na wanataalimu wa sanaajadiiya wengi (Dickinson, 1972; Sithole, 2006; Chisenga, 2002).

Wageni walikuja wakawabeza Waafrika na utamaduni wao na wao Waafrika wakakubali na sasa wanajidharau wenyewe. Wabungu walisalimu amri na kuacha hata mlima wenye dhahabu nyingi Ubunguni kuitwa jina la mlima Elizabeti badala ya kuuita mlima Ilonga, Kapala, Zunda, au Sigonda. Utu wa Mwafrika umepotea kabisa, badala ya kukataa utamaduni mpya, Wabungu wamelewa usasa na kuukana utu wao ambao ndio utamaduni wao wa asili. Utamaduni uliowakuza baba na mama zao, babu na bibi zao. Wabungu wamesahau kuwa Mwafrika ndiye chimbuko la ustaarabu na elimu duniani.

Chimbuko la Kila Jamii ina Ujumi Wake

Nadharia hii imetokana na mawazo ya John Frederick Dewey (1850 - 1952) mwanafalsafa na mwanasaikolojia Mmarekani. Dewey aliamini kuwa ujumi ni wazo la maadili na tabia ya mwanadamu inayoongozwa na kupenda (Alexander, 1987). Wafuasi wa nadharia hii ni wengi. Katika Afrika nadharia ya Kila Jamii ina Ujumi Wake iliyoanzishwa na Leopold Sedar Senghor katika miaka ya 1930. Msenegali huyu shujaa wa sanaajadiiya tangu miaka ya sitini na kuzama zaidi mwanzoni mwa miaka ya sabini. Nyota ya mwanasanaajaadiiya huyu ilizimikia mwaka 2001.

Kuzimika kwa nyota hii, ndiko kunakoendeleya kutuunganisha wanasanaajadiiya wote pamoja na mtafiti, kuyabetua mawazo yake na kuyaweka mahali peupe ili uzuri wa miiko, thamani ya miiko, kazi za miiko, ulimbe uliokuwamo ndani ya miiko na maadili yaliyolimo katika jamii ya Wabungu ambayo sasa yamefuwawa kuanza kuenziwa upya. Kwa kutumia nadharia hii, Wabungu wote wanakumbushwa, wanaamshwa kutoka katika lepe la usingizi na kuanza kuuenzi Ubungu, Uafrika na Utanzania wao na tunu zilizomo ndani ya miiko, (Sengo, 2008; Sengo, 1978). Aidha

nadharia ya Kila Jamii ina Ujumi Wake, inasaidia kuamsha ari ya watafiti wengine wa sanaajadiiya katika nyanja ya miiko, kuondoa fikra, hisia za kimagharibi na kuurejelea utu wa mtu mweusi utu wa Mbungu.

Katika jamii ya Wabungu, mwingiliano wa wageni ambao walileta dini na elimu ya kufisha lugha na fikra za Wabungu, kulisababisha jamii ya Wabungu kuanza kujikana yenyewe. Kuukana utu wao, Kukana ukweli wao (Thiong’o, 2009; Zimunya, 1982; Zirimu, 1971). Wabungu wakajiona wao si kitu mbele ya watu kutoka Uzunguni au ughaibuni. Wabungu wakatawaliwa na wakoloni na kutozwa kodi kwa nguvu. Kodi zikapewa majina kama, koda ya kichwa, kodi ya miguu, kodi ya mali uliyonayo, kodi ya maendeleo na nyingine nyingi. Mwili wako unaulipia kodi, kwa manufaa ya nani? Mbungu akajengewa woga wa kuinua kichwa mbele ya Masinjala (makarani wa kukusanya kodi wakati huo) na kukimbia baada ya kushindwa kulipa kodi. Wabungu wakaacha hata kutumia lugha yao. Lugha ni kasiki la kumbukumbu ya kila jambo katika jamii. Kuacha kutumia lugha ni sawa na kupoteza kumbukumbu zote za sanaajadiiya. Sasa Mbungu amebaki kuwa mtumwa wa usasa.

2.5.1 Umuhimu wa Nadharia ya Kila Jamii ina Ujumi Wake

Nadharia ya Kila Jamii ina Ujumi Wake inalenga kuurejesha Utu wa Mbungu uliopotea kabisa. Kila Jamii ina Ujumi Wake ni nadharia inayomfanya Mbungu kuurejesha utu wake ulioporwa na wageni hawa kutoka Uzunguni. Kila Jamii ina Ujumi Wake inatusisitiza kuurejesha utu wetu. Nadharia ya Kila Jamii ina Ujumi Wake inatualika Wabungu, Watanzania, Watu wa Afrika ya Mashariki na Waafrika

wote kwa ujumla wake, kuupenda, kuuenzi, kuulinda na kuuendeleza Utu wetu kama Waafrika. Nadharia hii inatutaka kuandika, kusimulia / kulumba, kutunga nyimbo, mashairi, kutega vitendawili, kutumia Methali na Miiko inayolenga kusifu na kutangaza uzuri wa watu weusi. Uzuri wa Wabungu.

Nadharia ya Kila Jamii ina Ujumi Wake inatoa wito wa maendeleo ya mtu mweusi. Maendeleo imarishi yatatokana na Wabungu kufanya kazi kwa bidii. Kutunza miiko yao ambayo inalinda uoto wa asili. Kutumia miiko amboyo inamkinga Mbungu dhidi ya maradhi na kifo. (Wafula, 2007; Sengo, 2009) wanabainisha matumizi ya sanaajadiiya kulingana na jamii husika ambayo hapa ni jamii ya Wabungu. Uzuri wa miiko katika malezi na maadili ya watoto na watu wazima katika jamii ya Wabungu.

Kila Jamii ina Ujumi Wake ni nadharia inayoshadidia kuwa Wabungu wana miiko. Wabungu wana maadili. Wabungu wanafanya kazi si wavivu na kwamba uvivu ni zao la wageni kufifisha maadili ya Wabungu ili waweze kupenyeza kafaulaya na kuchukua dhahabu kutoka Chunya. Wazungu wameacha alama za kudumu Ubunguni. Mlima wenye dhahabu nyingi Chunya ukapewa jina la mlima Elizabeti. Mwene wa Wabungu akashindwa kustahimili na kusalimu amri mbele ya madhabahu ya wakatoliki na kupewa jina la Simoni, na kuacha majina ya asili ya Wabungu Ilonga, Wangu, Njalaleiko nk. Huu ni mwanzo wa miiko ya Wabungu kupigwa mweleka. Kila Jamii ina Ujumi Wake unatuamsha, tufunguke macho ya ndani ya mtima na kuanza kutumia vilivyo vyetu. Wabungu watumie miiko yao, nyimbo zao na majina yao huu ndio utu wao.

Mawazo ya wanasayansi na falsafa wanasema kuwa, utambuzi wetu ndio unaojenga duniya. Imani yetu ndiyo inayotafsiri na kujenga vitu vinavyoonekana. Hakuna

ukweli unaokuwapo bila akili inayotafsiri ukweli huo, hivyo ukweli huelezewa na akili inayouona ukweli. Kila Jamii ina Ujumi Wake ni zao la Mwafrika Mtanzania, Mbungu anayeuona ukweli huo katika mazingira ya Ubunguni.

Mtafiti anaona kuwa nadharia nyingi alizozisoma katika utafiti huu, zinaonesha namna ya kuchanganua na kupambanua sanaajadiiya kwa mtazamo wa kimapokeo kutoka Uzunguni au Ughaibuni. Thamani ya miiko katika jamii ya Wabungu, inapaswa kumrejesha Mbungu katika kuuona, kuutambua, kuuthamini na kuugeukia Ubungu wake na kuishi kama Mbungu na si Mzungu. Mbungu anapaswa kutambua kuwa utu wake ulioporwa unarejeshwa. Hapa ni Mbungu tu ambaye anaweza kuurejesha utu wa Mbungu. Mbungu asitegemee hata siku moja kwa Mzungu kumsaidia ajitambue, aijue miiko yake, kwani anajua wazi kuwa huo utakuwa mwisho wa ukoloni wake mamboleo.

Kwa hali hiyo mtafiti anaona kuwa nadharia ya Kila Jamii in Ujumi Wake ni nadharia iliyoasisiwa na watu weusi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya sanaajaadiya ya mtu mweusi. Nadharia ya Kila Jamii ina Ujumi Wake haijaasisiwa Uzunguni. Nadharia hii inaziba pengo la nadharia kutoka Uzunguni ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikitumiwa na waandishi, wasomi, na watafiti wa sanaajaadiya katika mazingira ya Kiafrika na kwa uhalisia hazikuweza kukidhi, kuendana na mahitaji kwa kuzingatia thamani ya ulimbe na mapisi ya Mwafrika.

Aidha nadharia hii ya Kila Jamii ina Ujumi Wake ina nguzo zake nyingi. Katika utafiti huu, matafiti alishughulika na nguzo moja tu ambayo ni miiko inayomfanya Mbungu awe na maadili mema. Maadili yanayoshadidia uzuri wa mila, desturi, kazi,

uongozi, na makuzi ya vijana wa Kibungu wake kwa waume. Ujumi utakaobainisha kukengeuka kwa maadili ya jamii ya Wabungu na kutabii maadili ya Uzunguni (Sengo, 1981; P’Bitek, 1972). Miiko itakayoonesha staha na thamani ya Mbungu mahalia popote atakapokuwepo.

2.5.2 Hitimishi

Ili mtafiti aweze kufanikiwa katika kufanya utafiti, ni lazima awe na nadharia ambazo zitakuwa kama kurunzi yake katika kumwongoza ni kipi akifanye wapi na kwa kufuata misingi gani. Kwa hali hiyo mtafiti katika utafiti huu alitumia nadharia mbili kuu katika kazi hii. Nadharia ya kwanza ni ile ya Kila Jamii ina Ujumi Wake na ya pili ni ile ya Taalimu ina kwao na Fasihi ina kwao.