• Tidak ada hasil yang ditemukan

2.5.2 Hitimishi

Ili mtafiti aweze kufanikiwa katika kufanya utafiti, ni lazima awe na nadharia ambazo zitakuwa kama kurunzi yake katika kumwongoza ni kipi akifanye wapi na kwa kufuata misingi gani. Kwa hali hiyo mtafiti katika utafiti huu alitumia nadharia mbili kuu katika kazi hii. Nadharia ya kwanza ni ile ya Kila Jamii ina Ujumi Wake na ya pili ni ile ya Taalimu ina kwao na Fasihi ina kwao.

2.6 Nadharia ya Ndani-Nje

Nadharia ya Ndani Nje inaonekana kuwa ni moja ya nadharia kongwe za sanaajadiiya. Pamoja na kuwa na mapisi ya muda mrefu, kumekuwa na mfululizo wa mabadiliko ya matumizi ya nadharia hii. Jambo la msingi katika nadharia hii ni kuimanya jamii hisika Ndani Nje, mapisi, ada, kazi, maadili na ulimbe wa kazi katika jamii husika kama mzee Prof. Dkt. Sheikh Sengo alivyoanza kutoa mwelekeo mpya wa nadharia hii tangu katikati ya miaka ya 1970.

2.6.1 Chimbuko la Nadharia ya Ndani Nje

Yuri Long, (2010) katika makumbusho ya Taifa ya Marekani anabainisha chimbuko la nadharia ya Ndani Nje kuwa ni katika karne ya 13. Wanataalimu wa sayansi inayohusu mwili wa binadamu wakishirikiana na wanataalimu wa sanaa za maonesho, walitumia taalimu hiyo kutengeneza jukwaa la maonesho. Katika karne

ya 17 Ndaki nyingi Ulaya zilikuwa zimeshaanza ushirikiano wa kimasomo kati ya wanafunzi wa sayansi na wale wa sanaa. Mwaka 1315 huko Bologna nchini Italia, ndiko kulikorekodiwa ukumbi wa kwanza wa aina hii. Mchakato huu unatufikisha katika karne ya 18 ambapo mwanataaalimu Sir Charles Bell alipoandika kitabu kilichoitwa “Essays on the Anatomy of Expression in Painting” mwaka 1806. Katika kitabu hiki mwandishi alionesha imani yake kuhusu umuhimu wa sayansi inayohusu mwili na viungo vyake jinsi vilivyo, vinavyohusiyana na namna mwanadamu anavyoelezeya hisia zake.

Miaka mingi imepita na mawazo mengi yamepita pia. Wanataalimu wengi wametumiya nadharia hii katika mambo mengi kama, sheria, biashara na hata katika kuulinda na kuuelezeya uhayawani wa binadamu walioumbwa na Mwenyezi Mungu wanapojiona wao ni bora na wanajuwa kuliko Muumba wao, wakaona ushoga ndiyo jibu kwa maisha yao.

Katika karne ya 20, mwanasanaajadiiya na mtafiti mkongwe katika fani ya sanaajadiiya Afrika, Mzee Prof Dkt Sheikh Sengo T.Y S M, akaja na nadharia iliyo bora katika mazingira ya Kiafrika na inayokidhi mahitaji ya jamii za Kiafrika kwa sasa. Nadharia ya Ndani Nje mwanataalimu Mzee, Prof, Dkt Sengo anasema kuwa mwalimu na mhakiki wa fasihi ya jamii fulani ili aweze kuitafiti, kuifundisha au kuihakiki ni shuruti aimanye vizuri. Kuijuwa fasihi ya watu, ni muhimu kwanza kuwajuwa watu wenyewe, utamaduni wao, mila zao, ada na desturi zao, bahari yao ambayo ndiyo chemchemi ya ishara na dhana zao. Mawazo hayo yanaungwa mkono na (Bathawab na Sengo, 2007; Sengo, 2009; Sengo, 1978).

2.6.2 Wazo kuu la Nadharia ya Ndani Nje

Mtafiti anakubaliana na maneno ya (Sengo, 2009) ambayo yanashadidiwa na wanataalimu wengine kama (Wamitila, 2008; Mtesigwa, 1989; Mulokozi, 1989; Balisidya, 1982). Kila jamii ya watu ni tafauti. Kwa hali hiyo, ili kuihakiki au kuuelewa ukweli uliyomo katika semi za miiko ya jamii ni lazima msemaji na msikilizaji wawe na hisia za aina moja.

Kujua jamii fulani si kutabii vitu wanavyovifanya. Mtu inampasa abadilike kwa kujua kuwa jamii ni ya watu wa namna gani na wana imani ipi kwa Muumba wao. Kuna msemo usemao, “Ukienda Roma fanya kama Warumi”, na Wabungu wana msemo unaosema “Ukifika katika nchi ya watu wenye jicho moja na wewe toboa jicho lako moja”. Misemo yote hii inabainisha kuwa ni muhimu kwa mtu awaye yeyote kuheshimu mila na utamaduni wa wenyeji anapofika katika mazingira yao. Kwani kila jamii ina Ujumi wake.

Katika kila jamii mna miiko ambayo, si kila mja anaweza kutenda atakacho. Kabla ya kuuangalia mwiko huo, inampasa mtafiti kwenda ndani zaidi katika kuijuwa jamii hiyo kama daktari bingwa wa upasuaji aujuwavyo mwili wa binadamu kabla ya kufanya upasuwaji. Na Roma, muungwana hatakubali aige ya Waziri Mkuu fulani aliyewataka Waafrika wajiunge na kuteketezwa kwa Sodoma na Gomora ati, kwa sababu ya misaada. Afrika itowe mali na vyakula, mlaji ageuke aseme yeye anatoa msaada. Huu ni mwiko mkubwa kwa Mwafrika.

2.6.3 Umuhimu wa Nadharia ya Ndani Nje

Ngoma ya Makala inapopigwa basi kuna jambo. Labda isiche lyakumbuka, Kisiki kimeng’oka. Mtu mkubwa anapofariki katika jamii ya Wabungu, basi ngoma hiyo

maalumu hupigwa. Ngoma hii huchezwa na Ilombwe. Ilombwe ni watu maalumu waliofundwa na kuwa na sifa maalumu za kuweza kuingia na kuicheza ngoma hiyo. Ni mwiko kwa mtu asiyehusika kuingia ndani na kucheza ngoma hiyo. Ni mwiko kwa Mwafrika mwanaume kuwa msenge (shoga) au basha na mwanamama kusagana na mwingine. Kama kwa kufanya hayo ndizo haki za binadamu, ambazo hata haziwafai mahayawani, sembuse Waafrika, wazazi wa watu wote (Bathawab na Sengo, 2007).

Nadharia ya Ndani Nje inamlazimisha mtafiti na mwanasanaajadiiya, kabla ya kufanya au kutoa hitimisho la aina yoyote linalohusu jamii, jambo la msingi kwake ni kuijua jamii hiyo Ndani Nje. Mtafiti wa aina hii atakuwa na papasi za kupapasa, pua za kunusa ngozi ya kuhisi masikio ya kusikia, macho ya kuona na ubongo wa kuelewa miiko inayotumika katika jamii ya Wabungu na kuihusisha na Wabungu na si kuihusisha na Wazungu. Katika utafiti huu Nadharia ya Ndani Nje ni muhimu sana katika kufikia hitimishi sahihi la tatizo la utafiti linalosema kuhusu matatizo ya kufuwawa kwa miiko na kupotoka kwa maadili katika jamii ya Wabungu.

Tatizo la nadharia ya ndani nnje ni kwamba, kama mtafiti ni kutoka ughaibuni, ni rahisi kwake kupotosha ukweli wa maana ya miiko ya jamii anayoitafiti. Hii ni kwa sababu mtafiti hatakuwa na hisia za kuoanisha lugha ya picha inayotumika katika jamii, ulimbe na miiko yenyewe. Mtafiti wa ughaibuni hawezi kuona kufuwawa wala kupotoka kwa maadili kwani atakuwa na hisia za kwao ughaibuni na si Ubunguni. Mtu yeyote anayefanya utafiti wa Wabungu anapaswa kujua na kuheshimu mila na utamaduni wa Wabungu. Atakuwa ni mtovu wa nidhamu na mtu asiyefundwa kwao kama atajitia anajua zaidi ya Wabungu kuhusu mila na utamaduni wa wenye nao.