5.1 Utangulizi
Katika sura hii mtafiti amewasilisha na kufanyia uchambuzi data za awali na taarifa alizozikusanya kutoka kwenye eneo la utafiti. Data alizoziwasilisha hapa ni zile tu alizoziona kuwa ni muhimu katika utafiti huu. Eneo hili ni vijiji vya Mwambani na Udinde wilayani Chunya mkoa wa Mbeya. Kwanza mtafiti amewasilisha data za mazungumzo na Wabungu ambao aliweza kuzungumza nao. Mtafiti ameyagawanya mazungumzo haya kwa kufuata mtiririko wa maswali ya utafiti. Katika sehemu ya pili mtafiti amejadili miiko aliyoikusanya kutoka kwa watafitiwa katika eneo la utafiti pamoja na maelezo ya mtafiti akirejelea sura ya pili na sura ya tatu ya utafiti huu. Pia mtafiti amejadili miiko ambayo watafitiwa wanaiona kuwa imefuwawa au sasa haifuatwi au imeachwa na sababu za hali hiyo.
Licha ya mtiririko huo, mtafiti alianza kwa kuwahoji watafitiwa kuhusu maana ya maneno ya msingi katika utafiti. Maneno haya hayajaulizwa katika maswali ya usaili wa utafiti huu. Maneno hayo ni maana ya Miiko na maana ya Maadili. Lengo la maswali haya ni kumsaidia mtafiti na watafitiwa katika kuchanganua maswali ya usaili na kujiridhisha katika usaili kama kinachosailiwa na majibu ya maswali ya usaili yalimpa mtafiti ufafanuzi uliotarajiwa kubainisha, Kufuwawa kwa Miiko na Kupotoka kwa Maadili katika Jamii ya Wabungu.
Katika uwasilishaji na uchambuzi wa data hizi, maswali muhimu ya kujiuliza na kuyazingatiya ni; Je, katika sanaajadiiya ya Mbungu kuna kitu gani cha asili ya
Wabungu cha kuringia au kujivuniya? Je, kuna uwezekano wowote wa kuenzi utamaduni wao, mapisi yao, lugha yao, miiko yao dhidi ya kukengeuka kwa maadili ya Wabungu? Je, ni lazima kutabii kila kitu bila kujali uzuri wa maadili ya Kiafrika kama mavazi, miondoko, lugha, mitindo ya kujiremba hata kujikandika madini ya mekyuli ili kukoboa rangi ya ngozi kwa sababu ya ati urembo? (P’Bitek, 1972; Sengo, 2008 na Mulokozi, 2002) wanashadidia hali hii.
Kitu cha msingi tunachotakiwa kukifanya ni kuirejelea Miiko. Miiko ina Kwao, Elimu ina kwao na kila jamii ina ujumi wake. Dhana hizi zote zinasisitiza kuhusu kuurudia utu wa Mwafrika, kuuthamini, kuuheshimu na kuupenda Utu wa Mbungu na vikumbo vyake vyote vya sanaajadiiya. Kuirejelea miiko iliyopotea, au kufuwawa na kusababisha kukengeuka kwa maadili ya Wabungu.
Vijiji vya Mwambani na Udinde vimo ukingoni, ndani ya bonde la ufa Mashariki ya Ziwa Rukwa. Kijiji cha Mwambani sasa kina umeme, na wanakijiji wachache wameshaingiza umeme nyumbani mwao. Wanakijiji wachache sana wana runinga, ingawa kuna mabanda ya kuoneshea picha za runinga ambamo mnauza pombe na soda kwa watu wanaokwenda kuangalia picha. Watu wengi wanatumia redio kupata habari. Katika kijiji cha Udinde hakuna umeme wa umma lakini kuna watu wachache wana mashine ndogo za kufuwa umeme unaowawezesha kutumia runinga kuangalia video.
Hapa mtafiti anawasilisha data zote kwa maswali ya usaili. Maswali ya usaili ya watu wazima, maswali ya usaili ya viongozi na maswali ya usaili ya watoto. Maswali yote ya usaili yalitumiwa na mtafiti kuwahoji watafitiwa.
5.2 Maana ya Miiko
Awali ya yote mtafiti alijadili na watafitiwa kuhusu maana ya miiko katika jamii ya Wabungu. Wote walionesha uelewa mkubwa juu ya miiko kuwa ni makatazo ya kufanya, kusema, kuangalia, au kula kitu kilichokatazwa. Mtafiti alihoji kama kuna uhusiano wowote kati ya miiko na ushirikina. Majibu yalikuwa mwiko hauna uhusiano wowote na ushirikina au uchawi.
Bibi mmoja alisita kidogo na kueleza kuwa, kama mtu anafuata miiko ya zamani basi anaoneka kama ni mchawi. Wazo hili halikukubaliwa na watafitiwa wengine kwani walieleza kuwa tabia ya watu sasa ni kutaka mambo ya kisasa na kutaka kuulinda usasa huo kwa kutoa sababu wanazofikiri kuwa ni sahihi. Mkataa asili ni mtumwa na Kila Jamii ina Ujumi Wake.
Mzee mmoja alisema kuwa hali hii inasababishwa na dini. Katika mafundisho ya dini, watu wanakatazwa kufuata mila za wenyeji Wabungu kwa madai kuwa huo ni upagani. Mjadala huu ulikuwa na haja ya kuleta sababu za kufuwawa kwa matumizi ya miiko katika jamii ya Wabungu.
Kitu cha mwiko ni katazo ambalo mtu akifanya atapata madhara yeye aliyefanya au jamii yote bila ya mchawi kuweka nguvu zake. Wachawi wapo lakini hawana sehemu katika miiko ya maadili ya jamii ya Wabungu. Hata wachawi wanaogopa kuvunja miiko hii. Miiko haijawekwa na wachawi. Mzee huyu alisisitiza kuwa, miiko waliikuta, japokuwa alikiri kuwa, siku hizi watu wengi hawaifuati. Wanaivunja kila uchao na ndiyo maana kuna matatizo mengi. Kwa mfano, zamani
mtu akiwa porini, ilikuwa ni mwiko kukanyaga maua ya mmea unaoitwa kafauongo (eindouwalouwa). Endapo mtu anakanyaga maua haya porini basi akili ya mtu aliyekanyaga mmea huo itafungwa na atapotea njia hawezi kurudi nyumbani. Je kuna uhusiano wowote kati ya mchawi na kafauongo? Mtafitiwa alihoji.
Dhana hii iliwafundisha Wabungu kutotembea peke yao porini. Kama mtu atakanyaga mmea huu, mwenzake ataweza kumsaidia, kumwongoza na mwishowe kurudi nyumbani salama. Pia ilikuwa ni njia ya kuwaonya watu waendao msituni kwa kutafuta kuni au mahitaji mengine kuwa waangalifu.
Licha ya hayo, umoja wa wanajamii ni muhimu sana katika maisha ya kila siku ya Wabungu. Mwiko huu ulimfanya mtu kila wakati kufikiria kuhusu umoja na si ubinafsi. Msituni kuna hatari nyingi. Pia mwiko huu unasisitiza uangalifu wakati mtu au watu wanapokuwa msituni. Kutembea bila kuangalia chini unaweza kukanyaga nyoka ambao wengi ni hatari sana kwani wana sumu kali ya kufisha kwa haraka. Hadi sasa mwanamke haendi peke yake mwituni kusenya kuni, lazima aandamane na wenzake wengi.