• Tidak ada hasil yang ditemukan

Katika kila jamii kuna mgawanyo wa kazi na wajibu wa kila mtu kufuata jinsi. Ujumi wa jamii nyingi sasa unawekwa rehani kwa visingizio vya usasa, uvivu na kutokuwajibika kwa wanajamii. Sheria za jamii zilizotawala mienendo na maadili zilikuwa na nguvu kabla ya kuyeyushwa na maingilio ya wageni na sasa Wabungu wanaona kuwa hali ya kujisasa ndiyo hali yao ya asili. Ulinzi na usalama ilikuwa ni kazi mojawapo ya wanaume. Sasa ni kinyume vitu vyote vilivyowaunganisha Wabungu vimeondoka.

5.26.1 Ni Mwiko kwa Mwanaume Aliyeoa Kuingia au Kupika Jikoni, Atakuwa Ameolewa na Mwanamke

Katika jamii ya Wabungu, kazi ziligawanywa kwa kufuata jinsia. Ilikuwa ni kitendo cha aibu kwa mwanaume kufanya kazi za wanawake au kukaa mahali ambapo wanawake wanafanyia kazi. Basi jikoni ni sehemu muhimu sana kwa kazi za mwanamke. Kwa mwanaume kwenda kukaa au kupika jikoni wakati ameowa, kulionesha ni kwa kiasi gani mwanaume unatawaliwa na mkewe. Mwanaume yeyote hangependa huambiwa kuwa anatawaliwa mke wake, hali kadhalika mwanamke hangependa na ingakuwa jambo la aibu kuambiwa kuwa anamtawala au amemkalia mume wake. Suala zima ni la kuaminiana katika maisha na kupeana nafasi ya kuonesha umahiri katika kutimiza wajibu kama mke.

Taalimu ina kwao na fasihi ina kwao, Ulimbe wa taalimu unapatikana katika jamii husika, hii ni jamii ya Wabungu. Licha ya mgawanyo wa kazi za nyumbani, na

wajibu wa kila mwanandoa kutimiza wajibu wake, mwanamke anahitaji faragha. Faragha ya mavazi hadi ya maongezi. Wanawake walipaswa kukaa peke yao na kutumia nafasi hiya kuwafundisha wasichana wao mambo yanayowahusu kama wanawake. Hali kadhalika wavulana walikaa na wanaume wakifundishwa kazi za kiume katika jamii. Tabiya mwanamume kukaa jikoni kungemnyima mkewe uhuru wake wa kuchanganyika na wanawake wenzake. Thomas, alimweleza mtafiti kuwa kama mwanamke yupo katika siku zake basi mume alipika na chakula kiliandaliwa bila kujua kama ni mume aliyepika chakula hicho. Mwiko huu ulimlazimisha mume kumpa nafasi mke kushirikiana na wanawake wenzake na si kujifungia ndani na mumewe wakati wote.

5.26.2 Ni Mwiko kwa Mwanaume Kukalia Kinu Ataota Majipu Makalioni Kinu ni chombo muhimu ambacho kinahitajika kuwa kisafi wakati wote. Kinu kilitumika kuandalia chakula. Ni muhimu kuheshimu mahali pa kuandalia chakula kwa ajili ya kuepuka maradhi. Kwa kawaida kinu kiliwekwa jikoni au uwani. Wanaume mahali pao pa kuzungumzia palikuwa Barazani mbele ya nyumba chini ya mti. Kwa hali hii hapakuwa na sababu ya mwanamume kwenda kuchukua kinu na kukitumiya kama kiti.

Pia kwa heshima chakula kiliandaliwa kila mgeni anapofika. Kwa mila na ada za Wabungu, ilikuwa si heshima kwa mwanamke kumtoa mwanamume mahali alipokalia. Hili lingalikuwa tatizo kubwa. Kila kitu kilikuwa kwa ajili ya matumizi maalumu, hivyo wanaume walipaswa kujiandalia mahali pao pa kuongelea na kujitosheleza kwa vifaa vya kukalia.

5.26.3 Ni Mwiko kwa Mwanaume Kukalia Kinu Akikijambia, Atakapoowa Kila Mke Atakuwa Anakufa

Kinu ni chombo muhimu ambacho kinahitajika kuwa kisafi wakati wote. Ni muhimu kuheshimu mahali pa kuandalia chakula kwa ajili ya kuepusha maradhi. Hofu ya kujambia ndani ya kinu ina maana ya ndani zaidi, kama kusotea, huenda mtu alikwenda haja na hajafanya usafi vizuri. Hili lilikuwa na tatizo la kiafya na kimgawanyo wa kazi. Kama mwanaume atakuwa amekalia kinu inaweza kuwa ni vigumu kwa mwanamke kumwomba kuondoka na kukaa mahali pengine. Aidha maelezo ya mwiko wa “ni mwiko kwa mwanaume kukalia kinu ataota majipu makalioni” yanahusika.

5.26.4 Ni Mwiko Kumpiga Mwanaume kwa Ufagio, Atapooza

Wabungu wanaamini kuwa ufagio ni mchafu. Kwa mfano, ufagio husafishia maeneo mbalimbali kama vile chooni. Hivyo huchukuwa uchafu mtafiti alielezwa.

Bado maelezo ya kitaalimu zaidi yanahitajika kufafanua athari iliyopo iwapo mwanaume atapigwa na ufagio. Ni wazi kuwa, athari inayohofiwa ni kutokana na kuwa ufagio una ncha ambazo zinaweza kumchoma mtu kama atapigiwa. Vile vile, kwa vile ufagio husafishiwa maeneo machafu kwa hiyo unaweza kuchukuwa vijidudu vya maradhi na kumwingiya mtu mwilini.

Mwiko huu una mantiki ndani yake lakini tunaweza kujiuliza kuwa kwa vipi unasababisha madhara ya kupooza. Vile vile kutokana na ufafanuzi uliotolewa kabla ni wazi kuwa madhara yanaweza kumpata hata mwanamke. Ukweli ni kwamba hakuna mwanamke, mama yeyote ambaye angependa mtoto wake wa kiume apoteze uwezo wa uume wake.

5.26.5 Ni Mwiko Kukojowa Mtoni au Ndani ya Maji Uume Wako Utavutika Tendo la kukojoa mtoni ni jambo ovu kwani husababisha maji kuchafuka. Mwiko huu unahimiza kutunza vianzio vya maji ili kujikinga na maradhi, kama kichocho ambacho huenezwa kwa kuoga maji yenye vijidudu vya kichocho. Kama mtu mwenye ugonjwa atakojoa majini basi anaweza kueneza vijidudu. Vile vile katika miiko iliyotangulia ilielezewa kuwa nguo za mtoto zenye kinyesi zisifuliwe mtoni. Lengo la mwiko huu ni moja la kutoyaharibu maji ambayo yanatumika kwa shughuli mbalimbali sanjali na kulinda afya na maisha ya Wabungu. Erick na Paza walieleza.

5.26.6 Ni Mwiko Kuingia Kaburini na Viatu

Kaburi ni mahali pa kuheshimiwa kama mahali patakatifu pa kutolea sadaka. Viatu ni vitu vinavyokanyaga uchafu wa aina mbalimbali. Ingawa maiti hulazwa udongoni, lakini mahali hapa panapaswa kuwa safi na kutokutiwa najisi. Kukanyaga kaburini na viatu ni sawa na kupanda kitandani na viatu. Kiimani hapa ni mahali pa tambiko na kutolea sadaka, panapaswa kuhesimiwa. Mzee Mahella na Federiko walimweleza mtafiti. Utakatifu wa mahala na namna ya kupaingia unashadidiwa na vitabu vyote vitakatifu Biblia na Quruan Takatifu.