• Tidak ada hasil yang ditemukan

Kuvaa nguo ni lazima kwa watu wote. Hata zamani za kale watu walivaa magome ili kusetiri maungo yao. Ubora wa nguo unaweza kutafautiana lakini suala la mavazi ya kusetiri maungo si jambo la mjadala ni jambo la lazima. Watafitiwa wote waliosailiwa walibainisha jambo hili.

Watafitiwa wote walikereheshwa na mtindo wa sasa wa uvaaji, hasa mavazi ya wanawake. Uvaaji wa suruali kwa wanawake watafitiwa waliona kama ni kumwingilia Mungu shughuli za uumbaji. Kwa dhamiri kuu waliona kuwa mavazi ya kubana na kuonesha maumbile ya mtu au kuvaa suruali na kuacha makalio nusu nje au sehemu za mapaja ama matiti yao yakiwa wazi. Hii si tabia njema. Siku hizi tunashuhudiya wanaume watu wazima wanaweka rangi nywele zao kuficha mvi. Ili wasionekane kuwa wamepitwa na wakati. Pia wanaume wanatoga na kuvaa vipuri puani na masikioni, huku suruali zao zikiwacha makalio wazi au wakionesha nguo zao za ndani. Huu ni usasa, huu ni , haya si malezi ya Kila Jamii ina Ujumi Wake.

Hii si elimu iliyo na kwao Ubunguni. Uvaaji huu hauna mapisi yake Ubunguni, Ubunguni taalimu hii si kwao.

Hali hii ilionekana kuwa haikubaliki hata kidini. Wakristo, Waislamu, na madhehebu mengine mengi. Walitoa mfano wa wachungaji kuweka sheria za mavazi kanisani kuwa huku kote ni kukataa aina hiyo ya mavazi. Swali lililoulizwa ni kuwa wanamvalia nani mavazi haya? Haya ni mavazi ya mjini ambako watu hawapo na wazazi au ndugu zao bibi Wakunyala alisisitiza.

Mtafitiwa mmoja alisema yeye anaona aibu anapomwona mwanamke amevaa suruali. Anajisikia kama yeye yupo uchi. Alimkumbusha mtafiti kuhusu habari ya oparesheni mavazi nchini Tanzania miaka ya mwanzoni mwa sabini. Watu wote wake kwa waume walipaswa kushona na kuvaa nguo zenye urefu wa kufunika magoti. Pia hata kaptula za shule ilipasa ziwe na urefu wa kufunika magoti. Hii ilikuwa sera bora ya mavazi haijulikani baada ya hapo ilikwenda wapi?

Shida ni kuwa maamuzi mengine mazuri yanayotolewa na Serikala yanatolewa na kushika kasi kama moto wa mabua ya mahindi kisha unazimika mara moja hakuna hata mtu mmoja anayekumbuka kama kuna jambo lilitokea hapa duniani. Mavazi yanayositiri maungo ndiyo utu wa mtu. Wanyama wanatembea uchi kwa sababu hawana akili, wao ni hayawani. Je, watu hawa nao hawana akili? Je, wamerukwa na akili? Wamekuwa hayawani! Haya basi kama umependa kuivaa hiyo suruali basi shona yenye ukubwa wa kutosha na si kama uliyomnyang’anya mdogo wako au umeazima baada ya kuunguliwa na nyumba. Katika hali ya dharula mtu huyu atapewa kitenge au kanga ili ajisitiri na hiyo iwe kama nguo ya ndani.

Mzee Federiko alikumbuka visa vya mjini kuwa kuna wanawake siku moja walifuatwa na kundi la wauzaji wa sokoni wakizomewa na kupigiwa miluzi na mwishowe walichaniwa “vimini” walivyovaa ati kwa sababu walikuwa sawa na uchi wa mnyama hivyo hawakustahili kuvaa nguo. Hali hii watu wa mijini wanaileta huku Ubunguni, wanapokuja kutoka mjini. Hali hii ni hatari sana kwa watoto wetu kwani wanawaiga watu hawa bila kujua wanajikuta wametumbukia katika kilindi ambacho wanapata shida kutoka, au kuwatoa hao waliotumbukia.

Hali ya Mkwajuni na Mwambani ni mbaya zaidi kuliko Udinde na Maleza. Watu wa Mkwajuni wanawaharibia watoto wao wanapokuja huku na wao wanabadilika na kuanza kutabii kuvaa nguo za ajabu ajabu. Aidha wakati wa kujadili suala hili, liliambatana na miiko ya mavazi ya jamii ya Wabungu ambayo ilikuwa kama ifuatavyo;

1.16.1 Ni Mwiko kwa Wanawake Kuvaa Suruali

Mzee mmoja alieleza kuwa hapo zamani wanawake walivaa nguo nyingi za kuwasitiri mitetemo ya maungo yao. Nguo hizi zilikuwa madhubuti kwa upepo na mvua. Yumkini hata kama mwanamke huyu atapata dharura yoyote ya kimaumbile, basi alikuwa salama mbele za watu wote.

Tabia ya mtu ilipimwa kwa Mwenendo wake pamoja na mavazi yake. Kwa mwanamke kuvaa suruali kulifananishwa na kutabii tabia ya watu wa mjini, wahuni

au kutabii vitu visivyomhusu. Kama ilivyo aibu kwa mwanaume kuvaa gauni, ilikuwa ni aibu kubwa kwa mwanamke kuvaa suruali.

Jamii ilimwona mwanamke kama huyu kuwa, anataka mashindano ya kutafuta usawa ambao hauna msingi katika maumbile na kuleta matamanio kwa waume wakiwemo baba zake, wajomba, kina kaka, kwa kuonesha maungo yake ya mwili wazi wazi. Kuvaa suruali kulifananishwa na umalaya. Waliovaa suruali wengi wao walijisasa ndimi zao na kupata athari ya uhabithi, kupewa talaka katika ndoa kwa kukosa hisia za mambo. Kwa Mungu hawana nafasi nyingine ila motoni.

Watafitiwa walikiri kuzidiwa na ongezeko la wanawake wanaovaa suruali za kubana nchini hasa mijini. Katika jamii ya Wabungu katika kijiji cha Mkwajuni waliona kuwa ndilo chimbuko na mahali pa majaribio ya mavazi ya mjini.

5.16.2 Ni Mwiko Kuvaa Nguo za Kubana kwa Wanaume na Wanawake

Mavazi yalikuwa ni kielelezo kikubwa cha tabia ya mtu katika jamii ya Wabungu. Watafitiwa walisema kuwa watu wanavaa nguo kama wazungu, kama wapo katika nchi ya wazungu. Mzee Thomas Bangu alitoa mawazo yaliyolingana na (P’Bitek, 1972). Kwa kuangalia mavazi tu tunaweza kueleza tabia ya mtu kama ni mbaya au nzuri. Nguo za kubana zilihusishwa na uhuni au umalaya na mambo ya kutabii makundi mabaya ya mijini, wageni washenzi, wasokwao.

Katika jamii ya Wabungu hakuna nguo au mavazi ya kuogelea au mavazi maalumu ya kuchezea muziki wa kisasa. Kwa hali hiyo vazi ni vazi ambalo linaweza kuvaliwa mahali popote mbele ya watu. Nguo maalumu ni ile ya kuvaa wakati wa kwenda

Kanisani au Msikitini. Hii ni lazima iwe imefuliwa na kupigwa pasi vizuri. Hata wakati wa kucheza ngoma, wachezaji walivaa nguo zilizo sitiri maungo na wanawake walivaa demu ili kuacha mabega wazi wakati wa kucheza makala au simba kaleinde.

5.16.3 Ni Mwiko kwa Wanawake Kuvaa Nguo Fupi

Mavazi yanatafautiana kutoka jamii moja hadi nyingine. Hilo halitoshi, na kila jamii ilikuwa na aina yake ya uvaaji kutegemeana na shughuli za jamii hiyo. Aidha, tafauti ya mavazi tu si hoja bali uvaaji pia ulitafautiana sana. Wabungu si kama Wamasai. Jamii hizi mbili zinatafautiana kwa shughuli na mila ingawa sisi sote ni Waafrika.

Katika jamii ya Wabungu, mavazi ni kielezeo cha tabia njema ya utu uliokamilika kwa mwanaume au mwanamke. Vazi ni nguo yoyote inayovaliwa kusitiri mwili. Kusitiri ni kitendo cha kuficha jambo la aibu ili lisijulikane au kitendo anachofanya mtu kumkinga na fedheha. Nguo za kubana au fupi zilikuwa zinaashiria usasa na maisha ya mjini ya uhuni. Wabungu walikuwa na desturi ya kuvaa nguo zilizofunika mwili hadi chini ya magoti. Kwa mujibu wa bibi Ilonga na mzee Fredrick Bangu, (P’Bitek, 1972) wao walisema nguo fupi na za kubana ni matokeo ya kutabii mavazi ya wageni wa mijini.

Msichana aliyeonekana kukengeuka kimavazi, alikuwa hafai kuolewa kwani ni muhuni. Mifano hai ilitolewa kwa kuwataja watu majina ambao waume wao walipokuwa katika hatua ya uchumba waliwaonya kuwa msichana huyo au yule ni mhuni na kuhoji kama mtafiti alikuwa haoni hali hiyo. Mtu hawezi kuishi naye wataachana lakini kwa kuwa waume na wao walikuwa wamekaa mijini walikataa na

kung’ang’ania ndoa. Ama kweli “ndoa ndoana” kwa msemo wa kisasa, ya wahenga yalitimiya. “Asiyesikia la mkuu ama kweli huvunjika guu”. Ndoa zote hizo zilivunjika. Majuto yakawa mjukuu.

Hali hii inatuonesha kuwa dalili za mvua ni mawingu. Miiko ipo ili kutuongoza na kutukumbusha sehemu ambazo tunakengeuka au kuwaeleza wenzetu athari ya jambo kabla halijatokea ingawa mara nyingine wahenga walisema; “sikio la kufa halisikii dawa”.