4.5 Miktadha ya Majina ya Asili katika Koo za Ginantuzu
4.5.7 Muktadha wa Kudokeza Tabia na Matendo
Majina yanayotokana na muktadha wa tabia na matendo ya mtu kwa kawaida huakisi
mienendo ya wahusika. Mienendo hiyo hujumuisha ubishi, ukaidi, uasherati,
majivuno, usafi, hasira, upole, uchoyo, ukali, ubishi, ulevi na ukorofi. Watafitiwa
walibainisha kuwa muktadha wa tabia na matendo ya mtu hudokezwa katika majina
ya asili katika koo za Ginantuzu. Tabia na matendo hayo yalifanywa na waanzilishi
wa koo husika katika jamii. Matendo hayo katika jamii yalitofautiana kati ya mtu
mmoja na mwingine kama anavyodai Adrey (1970) kwamba, kila mtu katika jamii
ana tabia na matendo yanayoweza kumtofautisha na wengine. Madai haya yaliungwa
matendo yanayoweza kumtofautiasha na wengine. Utafiti umebaini kuwa katika koo
za Ginantuzu, kuna majina ya asili yenye maana yatokanayo na tabia na matendo ya
watu. Baadhi ya majina yanayotokana na tabia na matendo ya mtu ni pamoja na
Mabiti/Mbiti, Ng’homi, Salisali, Magulyati, Shayayi, Mbogo, Pilipili, Mashimba/ Shimba, Kitalumba, Ngokolo, Kuyela, Masemba, Nkwabi, Lombiha, Kuyela,
Ng’walali na Long’we. Katika majina haya yaliyoorodheshwa hapa juu, majina kama Mabiti/ Mbiti, Ng’homi, Salisali, Magulyati, Shayayi, Mbogo, Pilipili, Mashimba/Shimba, Kuyela, Walwa, Mahela, Ngokolo, Nkwabi na Masemba
yalionekana kutumiwa sana katika koo za Ginantuzu kwa sababu kila kata iliyofikiwa
na mtafiti kulikuwepo na uwepo wa majin haya. Majina haya yana maana fulani
katika jamii. Lengo kuu la kupewa majina hayo katika jamii ni kuwafanya wanajamii
waendelee na tabia na matendo yao yanayokubalika katika jamii au wajirekebishe na
tabia na matendo yasiyokubalika katika jamii husika.
Kwa mujibu wa watafitiwa walisema kuwa majina hayo yalitolewa kwa watoto wao
kwa ajili ya kuhimiza au kupinga tabia na matendo mabovu pindi watakapokuwa
wakubwa. Hapa chini ni ufafanuzi wa maadhi ya majina yaliyotokana na muktadha
wa tabia na matendo ya watu.
1. Mabiti (fisi) Hili ni jina analopewa mwanaume ambaye alikuwa na tabia na
matendo kama ya mnyama fisi. Jina hili linadokeza muktadha ya mtu aliye
na tamaa kupita kiasi. Jina hili wakati mwingine hujulikana kama Mbiti.
Vilevile kupatikana kwa wingi kwa mnyama huyu au mnyama huyu kuwa
na athari fulani katika maeneo husika katika jamii ni muktadha mwingine
2. Ng’homi (nge) Jina hili hupewa mwanaume ambaye ana tabia na matendo ya
ukali wa kupindukia kama alivyo mdudu nge. Hivyo jina hili hudokeza
mtu mkali na kaidi kuliko kawaida ya watu wengine. Tena watu wengine
mtu mwenye jina hili humwoona hatari sana katika jamii husika.
3. Salisali (panzi) Salisali ni panzi ambaye hachoki kuruka na panzi huyu pia ni
mjanja kuliko panzi wengine. Hivyo jamii katika koo za Ginantuzu
huamua kumpatia jina hili mwanaume ambaye ni mjanjamjanja katika
jamii. Wakati mwingine mtu mwenye tabia na matendo ya namna hiyo
humwiita mapepe ambaye hashikiki wala kukamatika.
4. Shayayi (sungura) Jina hili hupewa mwanaume ambaye anatabia na matendo ya
ujanjaujanja kama sungura alivyo. Mtu mwenye matendo haya katika
jamii ya Ginantuzu huwa hapendwi na jamii nzima. Hivyo mtu hupewa
jina hilo ili ajirekebishe na tabia ya ujanja ujanja.
5. Mbogo (nyati) Jina hili hupewa mtu wa kiume ambaye ni mpole katika jamii
lakini ni hatari sana ukimkorofisha. Tabia na matendo ya mnyama huyu
hupendwa sana na jamii katika koo za Ginantuzu. Jina hili katika jamii ya
Ginantuzu linatawala sana na kila mmoja anajivunia kuwa nalo katika
jamii.
6. Pilipili (pilipili) Kama lilivyo jina lenyewe pilipili kuwa ni kali. Hivyo jina hili
hupewa mtoto wa kiume ambaye anaonekana kuwa hapendi matani katika
jamii. Hivyo basi, jina hili hudokeza muktadha wa ukali na mtu
anayepewa jina hili husadifu jina lenyewe. Majina mengine
7. Kuyela (kuzurula) Hili ni jina analopewa mwanaume ambaye alionekana kuwa
na tabia na matendo ya uzururaji. Tabia ya uzururaji katika koo za
Ginantuzu ilipigwa vita sana hapo zamani kwani mtu wa namna hiyo
hakuwa na maendeleo yoyote kwake na hata katika jamii yake.
8. Masemba (vituko/utani) Hili ni jina alilopewa mtoto wa kiume na wazazi wake. Mtu ambaye alikuwa na vituko sana au mwazilishi wa jina hilo
alikuwa na vituko vingi vyenye kushangaza na kuchekesha katika maisha
yake, alistahiri jina hilo. Watu wenye vituko katika jamii ya Ginantuzu
kwa kiasi kikubwa walipendwa sana na walitakiwa sana kuwepo katika
shughuli yoyote iliyokuwa inafanywa kwa jumuia. Hivyo mtoto aliweza
kupewa jina hili kama ukumbusho wa mwanzilishi huyo.
9 Nkwabi (mtafutaji mali) Jina hili alipewa mtoto wa kiume akirithi kutoka kwa
wazazi/waanzilishi. Mwanzilishi wa jina hili alipewa kutokana na tabia ya
utafutaji mali kwa njia halali. Katika jamii ya Ginantuzu mtu kama huyu
alipendwa na kila mtu mwenye moyo wa utafutaji mali. Utafutaji mali
ulikuwa ni msingi wa maisha katika koo za Ginantuzu hivyo jina kama
hili lilipendwa na jamii na linapatikana kwa wingi katika koo za
Ginantuzu mpaka sasa.
10 Mayumila (kutoa kitu bila kipimo maalum) Jina hili lilitolewa kwa mtoto wa
kiume akirithi kutoka kwa mwanzilishi aliyekuwa na matendo na tabia
nzuri iliyokubalika kwa jamii kiasi kwamba alikuwa anatoa kitu chochote
kwa watu wengine bila kutumia kipimo maalum. Tabia kama hii ilikuwa
inamilikiwa na wachache sana. Wachache hawa walipewa jina hili kama
hulifupisha na kuliita Mayuma. Hivyo jina hili hudokeza muktadha wa
ukarimu kwa watu wengine.
Kutokana na ufafanuzi wa majina hayo hapa juu, utafiti umebaini kuwa tabia na
matendo ya mtu unadokeza muktadha wa majina katika koo za Ginantuzu na
muktadha huo wa majina huwa na maana tu kwa jamii husika. Mtoto anayepewa jina
la aina hiyo kutambuliwa kuwa yeye ni Mnyantuzu kutokana na jina la Ginantuzu
linalomtambulisha kwa jamii yake.
Ningependa ifahamike kuwa miktadha iliyoelezwa na watafitiwa ni baadhi tu kwani
ipo miktadha mingi kulingana na sehemu ambako mtoto alipewa hilo jina. Wakati
mwingine athari fulani ya jina halisi katika mazingira ya mtoto yaliweza kuchangia
kumaanisha maana ya jina husika. Hivyo basi jamii katika koo za Ginantuzu ziliweza
kutoa jina kulingana na miktadha mbalimbali.