4.5 Miktadha ya Majina ya Asili katika Koo za Ginantuzu
4.5.5 Muktadha wa Kudokeza Mahusiano katika Familia
Kama ilivyoelezwa hapo mwanzo kuwa, mahusiano ni hali ya kushirikiana au
kutoshirikiana katika mambo mbalimbali katika jamii ya watu. Mahusiano hayo
yanaweza kuwa mazuri (kushirikiana) au mabaya (kutoshirikiana). Mahusiano katika
familia ni muktadha unaotumika kuelezea majina ya asili katika koo za Ginantuzu.
Katika utafiti huu imebainika kuwa majina yaliyo mengi katika koo za Ginantuzu
yamedokeza muktadha wa mahusiano yaliyopo ndani ya familia na jamii kwa ujumla.
Majina ya aina hii yanaeleza mahusiano halisi yaliyo katika jamii husika. Majina hayo
mengine yanaonesha muktadha wa upendo, amani, furaha na mengine yamedokeza
chuki, ugomvi, mgogoro na migongano katika jamii husika. Kwa mujibu wa
watafitiwa hao waliendelea kusema kuwa mahusiano katika jamii yanaweza kuwa
mazuri na kwa upande mwingine yasiwe mazuri. Mahusiano yote hayo hujibainisha
katika majina wanayowapa watoto wao. Majina yanayopatikana kutokana na
mahusiano mazuri huwa yako wazi na ya kueleweka katika jamii lakini majina
yanayopatikana kutokana na mahusiano mabaya mara nyingi huwa na mafumbo ndani
yake. Baadhi tu ya majina yanayodokeza muktadha wa mahusiano katika familia ni
pamoja Mayombo, Mlekwa, Masanja, Buyegi, Lusangija, Mpejiwa, Oleng’wa,
Mihayo, Buki, Mpelwa, Matulanya, Mababza na Maseko.
Katika majina hayo, watafitiwa walifafanua kwa kueleza kuwa majina kama
yanadokeza muktadha wa mahusiano mazuri katika familia husika. Kwa mfano jina
Maseko ni jina analopewa mtoto wa kiume na wazazi wake wakiashiria kuwa mtoto
huyo amezaliwa kipindi cha amani katika familia hiyo. Hata wazazi wa mtoto huyo
wanaamini kuwa mtoto, huyo naye atakuwa ni mtu mwenye amani tele katika maisha
yake. Jina Oleng’wa lenye maana ya kukataliwa ni jina alilopewa mtoto wa kiume na wazazi wake baada ya muda mfupi kuzaliwa na mmojawapo ya wanandoa hao hasa
baba au familia anakoishi mama wa mtoto huyo kumkataa mtoto huyo. Jina hilo
hudokeza muktadha wa mahusiano mabaya. Majina mengine ambayo yanatawala sana
katika koo za Ginantuzu yenye kuonesha uhusiano mbaya ni Mlekwa lenye maana ya
aliyeachwa, Mpelwa lenye maana ya aliyekimbiwa na Masolwa lenye maana ya
aliyeokotwa. Majina haya ni baadhi tu ya majina ambayo yanadokeza muktadha wa
mahususiano mabaya katika familia mpaka ikafikia mmojawapo wa wazazi kuamua
kumwacha, kumkimbia au kumtupa kabisa mtoto. Matendo hayo yanapotokea katika
jamii watu wenye jukumu la kutoa majina kwa mtoto kumpatia mtoto jina hilo la
Masolwa kama alitupwa, Mlekwa au Mpelwa kama aliachwa au alikimbiwa na mzazi
wake. Hapa tunapenda kukufahamisha kuwa si kila mwenye majina hayo alitokea
katika muktadha huo hasha, majina haya wengine hupewa kutokana na kurithi kama
kumbukumbu kutoka kwa wanzilishi wake ambao asili yake alitokana na muktadha
huo. Hapa chini ni ufafanuzi wa baadhi ya majina hayo majina hayo.
1. Mayombo (vurugu) Jina hili alipewa mtoto wa kiume na wazazi wake ambaye
alizaliwa kipindi cha vurugu ya kijamii au kifamilia au muda mfupi baada
ya kipindi hicho cha vurugu. Watafitiwa pia walisema kuwa jina hili
linaweza kuwa Kayombo kama vurugu iliyotokea katika familia husika
2. Lusangija/Masanja (unganisha) Hili ni jina analopewa mtoto wa kiume na
wazazi wake baada ya kuzaliwa au kabla ya kuzaliwa kulikuwa na
vurugu kati ya mme na mke kiasi kwamba walikuwa wametengana.
Mara nyingi utenano huo ulisababishwa na kutopata mtoto. Katika koo
za Ginantuzu mtoto ni kiungo kikubwa cha kudumisha ndoa. Hali ya
kutopata mtoto kwa wanandoa husababisha vurugu isiyo na kikomo.
Baada ya kupata mtoto, mtoto huyo huwafanya waliotengana wawe
pamoja na jina la mtoto huyo aliyewaunganisha mtoto wazazi hao
hupewa jina la hujulikana kwa kwa jina la Lusangija/Sangija/Masanja
lenye kudokeza muktadha wa kurejea kwa mahusiano mazuri
yaliyopotea.
3. Mpejiwa (aliyefukuzwa) Jina hili alipewa mtoto ambaye mama yake
alifukuzwa na mme au familia mara tu baada ya kuzaliwa mtoto huyo.
Jina hili lilitolewa na wazazi wa mtoto huyo kutokana na vurugu
iliyotokea katika familia hiyo kama kumbukumbu ya baadaye kwa ajili
ya tukio hilo alilofanyiwa. Kwa hiyo basi jina hili linadokeza muktadha
wa kuwepo na mfarakano baina ya wanafamilia husika. Jina hili pia
liliweza kurithiwa kutoa kwa mwanzilishi ambaye ilimtokea hali hiyo.
Hivyo si kila mwenye jina hili kuna muktadha wa mfarakano bali
wengine hupewa jina hilo kwa ajili ya kumbukumbu tu.
4. Buyegi (furaha) Hili ni jina analopewa mtoto wa kike na wazazi wake au
jamii yake hasa baada ya mtoto huyo kuzaliwa na kuikuta familia ya
mtto huyo ikiwa katika kipindi cha furaha. Kama mtoto wa kiume
furaha pia. Hivyo jina hilo linadokeza muktadha wa amani katika familia
ya huyo mtoto kwani jina Buyegi linaweza kudokeza furaha kwa mtoto
ama furaha kwa familia. Wakati mwingine jina hilo hupatiwa mtoto na
wazazi wake wakimtabiria mtoto huyo kuwa na furaha katika maisha
yake.
5. Mihayo (maneno) Jina hili hupewa mtoto wa kiume au wa kike na watoa jina
wakiashiria kuwa aidha kipindi mama yake akiwa na ujauzito wa mtoto
huyo alikumbana na msukosuko wa vita vya maneno toka ama kwa
mme, ndugu, jamaa, jamii au hata familia yake kiasi kwamba mama
huyo alipata wakati mgumu sana kwa kipindi chote cha ujauzito. Hivyo
basi, baada ya kujifungua mtoto huyo watoa jina ikabidi wampatie jina
hilo ili kusadifu yaliyompata kipindi cha ujauzito kama kumbukumbu.
Wakati mwingine jina hilo lilitolewa kwa mtoto ikiwa mama wa mtoto
huyo alikuwa mwongeaji kupita kiasi yaani alikuwa haishiwi na maneno
kipindi cha ujauzito wake mpaka ikawalazimu watoa jina kumpatia jina
hilo kama kumbukumbu. Kwa maana hiyo jina hilo linadokeza pia
muktadha wa kutokuwa na amani katika familia husika.
6. Matulanya (mchonganishi) Hili ni jina ambalo hupewa mtoto wa kiume na
wazazi wake kukiwa na vurugu ya uchonganishi katika familia husika.
Vurugu hiyo itakuwa imesababishwa na mtoto huyo aliyezaliwa kwa njia
moja au nyingine. Wakati mwingine vurugu ya uchonganishi huo huwa
kwa mmojawapo wa wazazi wake. Kutokana na vurugu hiyo mtoto
hupewa jina hilo ili kutunza kumbukumbu ya tukio hilo la vurugu
mzima. Mara nyingi mtu huyo aliyepewa jina hilo huwa na tabia ta
uchonganishi miongoni mwa wanajamii.
7. Maseko (kicheko) Jina hili hupewa mtoto wa kiume aliyezaliwa kipindi cha
amani na furaha kiasi kwamba kuzaliwa kwa mtoto huyo kulileta
kicheko ndani ya familia na jamii kwa ujumla. Jina hili hubadilika na
kuwa Nsekela kama mtoto atazaliwa wa kike katika kipindi hicho likiwa
na maana hiyo hiyo. Hivyo basi jina hili nalo hudokeza muktadha wa
amani na furaha katika familia husika.
8. Mapambano (mapambano) Hili ni jina analopewa mtoto wa kiume ambaye
amezaliwa kipindi cha mapambano fulani. Mapambano hayo yanaweza
yakawa ya kifamilia, kiukoo au kijamii Jina jingine katika koo za
Ginantuzu linalofanana na hilo ni Bulugu. Hivyo basi jina hili la
Mapambano hudokeza mukiadha wa kutokuwa na amani wakati mtoto
huyo anazaliwa aidha katika familia hiyo au katika jamii hiyo.
9. Mabanza (mashitaka) Hili ni jina ambalo anapewa mtoto wa kiume ambaye
alizaliwa kipindi cha mashitaka baina ya wanadoa au wanajamii husika.
Wakati mwingine jina hili hupewa mtoto ambapo mmoja wapo wa
wazazi wake kama baba au mama alikuwa na tabia ya kupenda sana kesi.
Hivyo basi jina hili hudokeza pia muktadha wa kutokuwa na amani
katika jamii ya mtoto huyo.
Kutokana na majina hayo, utafiti umebaini kuwa majina ya watu katika koo za
Ginantuzu hudokeza muktadha wa mahusiano yaliyopo katika familia na jamii kwa