• Tidak ada hasil yang ditemukan

KATEGORIA ZA RARA KATIKA AWAMU NNE ZA MAENDELEO

4.2 Chimbuko la Sanaa

Kuna wataalamu wengi wameeleza juu ya chimbuko la sanaa kinadharia wakiwemo Nkwera (h.t); Jahn, (1961); Levine, (1977); Senkoro, (1987); Okpewho, (1992); na Mulokozi, (1996). Jahn, (1961) anasema kwamba; “kwa kuwa sanaa haitengani na mwanadamu, ni dhahiri kuwa fasihi ilianza na mwanadamu”. Maelezo haya yanatueleza kuwa sanaa kwa ujumla ilikuwa sahemu ya maisha na utamaduni wa mwanadamu. Hata hivyo, Jahn hatuelezi kinagaubaga sanaa hii na mwanadamu walikutana nayo wapi.

Aidha, wataalamu wengi wanakubaliana kuwepo kwa mitazamo miwili inayofafanua suala la chimbuko au chanzo cha fasihi. Mitazamo hiyo ni ule wa kidhanifu na ule wa kiyakinifu Williams, (1977); Senkoro, (1987) na Mulokozi (1996). Kwa kuanza na mtazamo wa kidhanifu; mtazamo huu unaiona sanaa au fasihi kama zao toka kwa Mungu. Mwanasanaa anachukuliwa kama apokeae fasihi ikiwa imekwishapikwa na kuivishwa na Mungu. Kujitokeza kwa mtazamo huu kunaanza tangu katika mawazo

ya wanafalsafa wa Kigiriki na Kirumi mathalani Socrates, Plato na Aristotle katika mijadala yao ya kuitazama sanaa kinadharia (Harrison-Barbet, 1990). Kwa upande wa fasihi ya Kiswahili, wahakiki wanaojitokeza na mtazamo huu ni kama Nkwera (1976) na Ramadhan (Mulika 3:5). Mtazamo huu unakubaliana sanaa kuwepo tangu kuwepo mwanadamu katika uso wa dunia. Haya yanasisitiza kuwa fasihi haikugunduliwa katika kipindi fulani cha maendeleo ya mwanadamu, bali ilikuwa zawadi ya Mungu kwa mwanadamu.

Aidha, mtazamo huu kama unavyotolewa kasoro na baadhi ya wataalamu wakiwemo Williams, (1977); Okpewho, (1992) na Mulokozi, (1996) wanaona kwamba unajadili taaluma kwa kuichanganya na imani suala ambalo ni gumu kulithibitishwa kisayansi; pili ni kuwa, mtazamo wa namna hii unatafuta chimbuko la vitu vya kitamaduni nje ya maisha halisi ya mwanadamu na nje ya dunia. Jambo hili linakanusha masuala ya kimazingira na mapambano ya mwanadamu katika kumlea mtu na kumfanya akubalike na aendane na utamaduni wake. Pamoja na hayo, mtazamo wa namna hii unamtenganisha msanii na jamii yake na kumfanya kuwa juu zaidi ya watu wengine kwa kumuweka karibu na Mungu (Williams, 1977 na Mulokozi, 1996).

Plato, (1935) katika kupunguza nguvu za vuguvugu hili la wanaudhanifu anasema; “A man is a master of everything ….. man is the measure of all things”. Mwanadamu ndiye mjuzi wa kila kitu……mwanadamu ni mwamuzi kwa kila kitu (Tafsiri yetu). Plato anachotuambia ni kuwa hakuna kilicho juu ya mwanadamu na kila kitu hupimwa na kuamuliwa na mwanadamu ambaye nje ya uumbaji ana mamlaka ya chochote kiishicho juu ya dunia. Haya kwa namna nyingine yanadhihirika katika maandiko matakatifu Biblia Mwanzo (1:28) wakisema; “Mungu

akawabariki akawaambia, zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi”. Hali hii inatuaminisha kuwa kila kilichopo juu ya dunia kinatawaliwa na huyu mwanadamu. Aidha, kwa maelezo kama haya sanaa ambayo ni matokeo ya mkono wa mwanadamu haitoki nje ya mwanadamu. Hata hivyo, mwelekeo wa wanaudhanifu haupaswi kubezwa moja kwa moja kana kwamba hakuna kitu cha kuzingatia katika kuitazama sanaa na chimbuko lake.

Mtazamo wa pili unaiangalia fasihi na sanaa kwa ujumla kama inayotokana na mazingira halisi ya jamii hapa duniani na si kwingineko. Kwa hakika mtazamo huu unaiona fasihi hasa fasihi ya mwanzo kama zao la mazingira na fasihi hii ilifungamana na kazi na uzalishaji mali (Senkoro, 1987). Nadharia hii inadai kuwa mwanadamu alianza kubadilika alipoanza kuwa mfanyakazi, kuzalisha mali, na hivyo kubadili mazingira ya kimaumbile aliyoyakuta. (Williams, 1977; Senkoro, 1987; na Mulokozi, 1996), wanakubaliana kuwa baada ya mwanadamu kuwepo duniani (Kutoka katika uumbaji wa Mungu au akitokea mtini kama baadhi ya wataalamu wanavyodai) ilimlazimu ashirikiane na wenzake. Hali ya kushiriki ilimulazimu mwanadamu huyu kuwa na chombo cha mawasiliano. Lugha ilianza kama njia tu ya mawasiliano na baadaye lugha ikawa chombo cha sanaa, yaani fasihi ingawaje neno hilo ‘fasihi’ bado lilikuwa halijaanza kutumika.

Mwanadamu wa wakati huu yaani katika ujima wa awali, hakuwa na uwezo mkubwa wa kuyatawala mazingira yake. Mazingira nayo yalikuwa na changamoto nyingi zilizomlazimisha kuanza matumizi ya zana. Kihistoria, tunaelezwa juu ya mabadiliko mbalimbali aliyopitia mwanadamu katika utengenezaji wa zana tangu zana ya jiwe

hadi zana ya chuma na mashine tutumiazo sasa. Mabadiliko haya ya matumizi ya zana yalikuwa ni matokeo ya mwanadamu kuongezeka uwezo wa kufikiri na njia za kibunifu. Kadri muda ulivyopita sanaa ilipanuka kutoka katika matumizi ya kawaida na kuingia katika mikitadha mingine kama ya burudani. Kupanuka na kukua kwa sanaa katika mikitadha ya kazi na burudani ndiko kunakochipua fasihi ya mwanzo.

Hatua hizo hapo juu zinatuchorea mstari wa kategoria ya mwanzo ya rara. Aidha, matumizi ya lugha ya mwanadamu wa kipindi hiki hayakupiga hatua kubwa kutokana na ugunduzi wa dhana mbalimbali kuwa katika hatua za mwanzo. Hali hii ilimfanya mwanadamu kuwa na uwezo mdogo wa kibunifu na matumizi ya hali ya chini ya lugha. Ala za muziki ambazo tunaelezwa kwamba zilikuwa ni sauti zilizotokana na zana za kazi haikujaa ubunifu wa kisanaa kama tunaouona hivi sasa. Masuala yote haya yaliifanya rara iliyojitokeza kuwa kwa ajili ya kuchapua kazi. Senkoro, (1987) katika hili anasema;

Hatua ya kuwa na uwezo wa kufikiri na kupambanua mambo kwa usahihi, upambanuzi uliobeba dhana za uzuri na ubaya, ilikuwa ni hatua ya mbele na ya maendeleo kwani sasa mtu hakuwa mtumiaji tu wa silaha, bali alikuwa mtengenezaji wa silaha bora zaidi. Hisia za kisanaa zilianza sasa kutumiwa katika kutekeleza kazi kwa nyenzo bora zaidi. Sanaa inayoelezewa hapa ni sanaa tumizi, sanaa iliyokuwa imeelekezwa moja kwa moja katika matumizi ya mtu ya kujihami na mazingira. Ni sanaa ambayo ilikuwa imefungamana na kazi.

Maelezo ya Senkoro yanatufikisha katika kuiona rara ya mwanzo na mabadiliko yaliyochochewa na mazingira halisi. Mazingira haya ni mazingira ya uzalishaji mali, tena uzalishaji mali wa kijima kwa maana ya uzalishaji uliotegemea zana za hali ya chini. Kwa hakika maelezo haya yanaendelea kutujuza kuwa hatua za mwanzo za

mwanadamu zilikuwa kwa ajili ya kutimiza mahitaji yake ya muhimu, kama vile kula, na mengine; lakini baada ya mahitaji haya mtu alianza kupambana ili kupata mahitaji mengine, mahitaji ya kutimiza hisia zake za kisanaa na hili linajitokeza katika michoro mbalimbali katika makumbusho ya mtu wa mwanzo, kwa mfano michoro ya mapangoni Kondoa na Isimila hapa Tanzania.

4.2.1 Rara Katika Kipindi cha Ujima

Mfumo wa kimajumui katika utafiti huu unachukuliwa kama mfumo unaojitokeza katika kipindi cha ujima wa awali. Aidha, mfumo huu unatazamwa kwa kumtazama mwanadamu wa mwanzo; yaani mwanadamu aliyeishi maisha ya kuhamahama na ambaye alikuwa bado hajawa na makazi maalumu ya uzalishaji.

Kama wasemavyo, (Eaton, 1966; John, 1979; Juhani, 1988; na Helge, 1996) kwamba miaka 10,000 iliyopita Afrika na Tanzania kwa upekee ilikaliwa na wawindaji na wakusanyaji. Jamii hizi kutokana na kuishi maisha ya mapangoni na ya kuhamahama katika kutafuta riziki zao, hazikuwa na lugha iliyokuwa imeendelea kama tuliyonayo sasa. Jamii hizi kadri zilivyoishi zilizaliana na kuongezeka, mazingira nayo yalibadilika kwa maana ya kupungua chakula kama mizizi, matunda na wanyama ambavyo vilikuwa tegemeo kwa maisha yao. Hali hii iliwalazimisha wanajamii hizi kuishi pamoja ili kupambana na mazingira hayo. Kuishi pamoja kulichochea ushirikiano baina ya wanajamii hizi. Mashirikiano haya yalihitaji chombo cha mawasiliano hivyo, lugha ikaibuka. Lugha ya mwanzo kama asemavyo Senkoro, (1987) ilikuwa imefungamana na mwigo wa sauti za zana za kazi, milio ya wanyama, ndege na viumbe vingine. Ushahidi katika hilo unatolewa pia na wanaisimu mbalimbali kama (Hymes, 1964; na Parret, 1976). Lugha hii iliyofuatia

sauti hizi za zana za kazi ikazalisha wimbo ambao ulimhamasisha mwanadamu wakati wa kazi na hii ndiyo hasa inayoibua rara ya kwanza ambayo iliambatana na kazi. Maelezo haya yanapewa nguvu na wimbo ulioimbwa na mababu wa Kinyamwanga katika Sherehe zao za Kingwengwi kama ulivyoimbwa na Bi Songa wakati wa ukusanyaji wa data. Wanasema kuwa wimbo huu uliwakumbusha wanawake kutunza mifugo yao kutokana na kuwa bila wale ng’ombe mahari aliyolipiwa ingeweza kurudishwa. Hata hivyo, kuna suala la ukosefu wa uaminifu katika maisha ya ndoa ambalo nalo ni jukumu la wanafamilia kulizingatia (Maelezo ya Bi. Songa wakati wa ukusanyaji wa data).