• Tidak ada hasil yang ditemukan

Rara Katika Kipindi cha Uhuru 1960 hadi 1967

KATEGORIA ZA RARA KATIKA AWAMU NNE ZA MAENDELEO

6. Wimbo wa Mgeni (Mkoloni)

4.3 Rara Katika Kipindi cha Uhuru 1960 hadi 1967

Baada ya uhuru Tanzania ilipitia hatua mbalimbali za maendeleo kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Kiuchumi hali haikuwa nzuri, ndiyo Tanganyika, kama ilivyojulikana ilikuwa ndiyo kwanza imekabidhiwa kwa viongozi wachanga. Hakukuwa na bajeti ya kutosha kuendesha shughuli za kiserikali na kijamii na hata msaada mdogo uliopatikana ulitoka kwa haohao wakoloni na mataifa mengine ya Ulaya. Hali hii isingemaliza matatizo ya kijamii na kiutawala bila kuacha athari za kikoloni katika Tanganyika kiurahisi. Masuala kama ya huduma za jamii, shule, hospitali, huduma za afya ambazo wanajamii walitegemea kuwa baada ya uhuru zitakuwa mikononi mwao yalidumaa. Hii iliongeza matatizo makubwa kwa wanajamii, maisha bora waliyoyategemea yakawa ndoto na baadhi wakaanza kudhani bora kumrudisha mkoloni.

Kwa upande wa pili ilikuwa kisiasa na kiutamaduni. Kama sehemu ya kurudisha utamaduni wa Mtanzania uliokua umetetereka kipindi chote cha Ukoloni, Mwalimu Nyerere alitimiza Malengo yaliyokuwa yamewekwa na mkutano wa TAA (Tanganyika African Association) mwaka 1947. Mkutano huu uliofanyika mjini Unguja, ambao ulifuatiwa na mkutano wa TANU wa mwaka 1954 na yote kuweka maazimio ya kutumia lugha ya Kiswahili katika shughuli zake. Pamoja na kupendekeza Kiswahili kutumika kuwa lugha ya mawasiliano katika shughuli mbalimbali za kiserikali na kitamaduni, Mtanzania alijengwa kujitambua kama raia

huru na mwenye maamuzi katika rasilimali za nchi yake. Haya yanabainika katika wimbo wa rara inayoimbwa na wasanii mbalimbali kipindi cha baada ya uhuru wakiwemo, Moro jazz, Kilwa jazz na wanasanaa mbalimbali wa enzi hizo ‘Mwongozo wa TANU’;

Yeli: Hoyeeeee!

Mwongozo mpya umetangazwa Na uhuru siyo ule wa bendera pekee Wala wimbooo wa Taifa si uhuru wa kweli Bali kila kitu tumiliki sisi wananchi x3 Mwongozo!

Yeli: Mwongozo mpya wa TANU Wazumi: Hoyeee twafurahia oooooh Yeli: Mwongozo mpya wa TANU Wazumi: Umma twaunga mkonoo Yeli: Tumenyonywa vya kutosha Wazumi: Hoyeee twafurahia oooh Yeli: Tumeonewa vya kutosha Wazumi: Umma twaunga mkonoo Yeli: Tumepuuzwa vya kutosha Wazumi: Hoyeee twafurahia ooooh Yeli: Sasa twataka mapinduzi Wazumi: Umma twaunga mkono Yeli: Oooooh! Oooooh! Oooooh! Wazumi: Hoyeee twafurahia ooooh! (Muziki wa ala)

Yeli: Mwongozo mpya wa TANU Wazumi: Umma twaunga mkono Yeli: Kuzikwa kwa mabepari Wazumi: Hoyee twafurahia ooooh! Yeli: Kuzikwa kwa wanyonyaji Wazumi: Umma twaunga mkono Yeli: Oooooh! Ooooh! Ooooh! Wazumi: Hoyeee twafurahia eeeeeeh!

Chanzo, TBC (Mwimbaji Mbaraka Mwishehe)

Maudhui ya wimbo huu pamoja na kushangilia uhuru, yanaweka msisitizo kwa wananchi kutekeleza kwa pamoja mwongozo wa TANU chama tawala. Kwa upande wa kisiasa, Waafrika na Watanganyika kwa upekee waliokuwa na uwezo wa kusimamia masuala yao ya kiutwala nayo yalikuwa na changamoto. Waliokuwa

wamebahatika kupata elimu ya Kizungu walikuwa wachache ukilinganisha na nafasi zilizokuwepo za kiutawala katika Taifa lao. Hapa mkoloni alipata mwanya wa kuendelea kupandikiza misingi ya kisiasa na kitamaduni katika nchi changa ya Tanganyika na mahali kwingine walipopata uhuru. Mwanya huu ulipatikana kutokana na kwamba nchi hizi hazikuwa na uwezo wa kibajeti na kitaalamu kuendesha mambo yake. Mataifa mengi yaliyopata uhuru yaliendelea kutegemea misaada kutoka kwa wakoloni. Na misaada hiyo kidogo na ambayo haikutolewa kwa wakati ilikuwa na masharti mengi. Maisha ya wananchi katika familia yaliendelea kuwa magumu na rara zilizoimbwa kipindi hiki zilikuwa zikiomboleza machungu ya maisha duni, ingawaje nyingine ziliendele kusifu utawala wa ndugu zao huku zikisisitiza kufanya kazi kwa bidii. Wimbo wa Mbaraka Mwishehe ambao ulitungwa kwa mara ya kwanza na Saadan Kandoro kwa lengo la kuimbwa na vijana wa TANU YOUTH LEGUE miaka ya 1962 ‘Kazi Ndiyo Msingi wa Maisha’ ni mfano mzuri;

Wito kwa raia wote tusiwe wavivu, Kwaajili ya maisha yetu!

Yawe bora tufanye nini? Tufanye kazi nguvu moja,

Tuinue uchumi kwa harakaaaa x4 Kazi ndiyo msingi wa maisha, Maendeleo yaletwa na kazi x2 Tusikalie eeehe he he!

Uchumi wetu eehe he he!

Tufanye kazi tusiwe wavivu oooh Kazi ndiyo msingi wa maisha, Maendeleo yaletwa na kazi x2 Bila kazi eehe he he!x2

Taifa lolote haliwezi kujengeka. Kazi ndiyo msingi wa maisha, Maendeleo yaletwa na kazi x2 Tusikalie eeehe he he!

Uchumi wetu eehe he he! Tufanye kazi tusiwe wavivu oo

Kazi ndiyo msingi wa maisha, Maendeleo yaletwa na kazi x2 Bila kazi eehe he he!x2

Taifa lolote haliwezi kujengeka Chanzo, TBC (Mbaraka Mwishehe)

Uhuru uliokuwa umepatikana haukuzuia harakati za kisiasa katika nchi hizo. Kama Senyamanza, (2011) anavyosema katika mjadala wa nyimbo katika kampeni za kisiasa anasema;

Baada ya uhuru kampeni za kisiasa ziliendelea kushika kasi nchini Tanzania. Chama Tawala TANU’ kilieneza siasa yake na misingi ya utawala wake kwa wananchi… wasanii na wananchi wa kawaida waliitikia kwa dhati siasa ya TANU; jukwaa la kisiasa likawa sehemu ya sanaa. Wasanii mashuhuri kama Mathias Mnyampala, Saadan Kandoro, na wengine walihubiri katika jukwaa kupitia sanaa zao. Vikundi mbalimbali vya ngoma na nyimbo vilitumika katika majukwaa mbalimbali ya kisiasa. Kwa mfano, vikundi vya vijana vilivyojulikana kwa jina la TANU YOUTH LEAGUE vilitumbuiza, sambamba na watoto wa shule kote nchini.

Kipindi hiki kwa upande wa Tanzania kilishuhudia sanaa iliyokuwa haitofautiani sana na sanaa iliyokuwepo katika kipindi cha ukoloni. Tunasema hivi kutokana na kuwa sanaa ya kikoloni iliyokuwepo ndiyo iliyoendelea kugezwa kwa upande wa fani. Hakukuwa na kigeni katika sanaa hususani ya nyimbo, jamii ya kipindi hiki ilibadilisha kidogo upande wa maudhui, kwa maana kwamba nyimbo zilizokemea na kutuhumu utawala wa mkoloni zilibadilishwa maudhui yake na kushangilia uhuru ambao ulisubiriwa kwa muda mrefu. Maudhui ya kuwatukuza viongozi wa Kiafrika na wapigania uhuru zilishamiri, mfano wa sanaa ya kipindi hiki ni wimbo wa Kisukuma wa kipindi kifupi baada ya ukoloni.

7. Wimbo Bazungu Bhashetani