• Tidak ada hasil yang ditemukan

Wimbo Katonzi Nkasyala neka katonzi x2

KATEGORIA ZA RARA KATIKA AWAMU NNE ZA MAENDELEO

9. Wimbo Katonzi Nkasyala neka katonzi x2

Nene katonzi, eh wee katonzi x2 Nkasyala nkuyimba x2

Nkasyala nkuyimba kakwale, Nasova umayi,

Nasova umwana. Avalozi mhuu!

Nitakuwa kama ndege wa porini x2 Mimi ndege, eh wee ndege wa pori x2 Nimeachwa kwenye mihangaiko x2

Nimebaki najilea kama kifaranga cha kwale, Nimemkosa mama,

Nimemkosa mtoto, Wachawi mhuu! Chanzo. Msanii Kalugwanje kutoka Mbozi – Mbeya

Huu ni wimbo unaoimbwa wakati wa msiba. Umebeba maudhui ya huzuni kwa jamaa wa marehemu. Mfiwa anajiuliza namna gani ataishi baada ya kupoteza mtu wa muhimu katika maisha yake. Aidha, ugonjwa au sababu ya kifo hiki kinahusishwa na mila za uchawi na ushirikina. Katika hali ya kawaida, magonjwa ya malaria na magonjwa ya maambikizi hayafikiriwi katika jamii hizi kutokana na mazingira ya wanajamii wenyewe. Mazingira ambayo huduma za afya, elimu, na nyingine hazipatikani kwa urahisi; uchawi na ushirikina huchukua nafasi kubwa.

Mfumo wa ughatuaji wa madaraka ulioanzishwa kama imani na njia ya kuleta maendeleo miaka ya 1960 hadi 1970 ulipunguzwa nguvu na mfumo wa serikali kuu. Kuanzishwa kwa serikali kuu mwaka 1972 kulifungua njia ya kumaliza mfumo wa awali wa serikali za mitaa na nchi ikawa haina viongozi wa vijiji na mitaa mpaka ilipoanzishwa tena mwaka 1982 na kufanywa kama mawakala wa serikali kuu. Kuyumba yumba kwa utawala katika serikali, kuliifanya serikali na wananchi wake kuwa katika hali ngumu kiutawala.

Aidha, matokeo ya maamuzi haya yalizidi kuushusha uchumi wa taifa na wananchi wake, huduma za jamii zikawa duni na kuacha ombwe la utawala kwa wananchi kama asemavyo Nyerere akinukuliwa na Mkandala na Weanzie, (2000) “Kuna

jambo nisingelifanya kama ningetakiwa kuanza upya. Moja wapo ni kuvunjwa kwa serikali za mitaa na kuharibu vyama vya ushirika”. Kuvunjwa kwa vyama vya ushirika kuliondoa ushiriki wa wananchi katika maendeleo yao na taifa. Hali hii ndiyo iliyoleta matatizo ya kiuchumi katika taifa la Tanzania miongoni mwa wananchi. Serikali ikashindwa kuwahudumia wananchi na kukifanya chama tawala kutoa matamko mbalimbali ambayo nayo hayakutekelezwa kabisa.

Aidha, matokeo ya kipindi hiki yanaweza kujadiliwa kwa kuegemea katika mwainisho wa mwanaathropojia Edward Taylor (1832-1917) akijadili suala la utamaduni na kusema kuwa; "Utamaduni" ulihusisha mambo yote yaliyomhusu binadamu ambayo hayakufungamana na matokeo ya kimaumbile. Dhana ya utamaduni katika Anthropolojia ya Kimarekani ilikuwa na maana mbili: (1) Uwezo wa kibinadamu wa kuainisha na kuwasilisha tajriba za kibinadamu kiishara na kutenda mambo kiubunifu; na (2) Namna mbalimbali watu wanaoishi katika sehemu mbalimbali ulimwenguni huainisha na kuwasilisha tajriba zao za maisha na kutenda mambo kiubunifu.

Hii ni kumaanisha kwamba watu walitumia sanaa zao kueleza mandhila ya kipindi chao kupitia kazi za kibunifu. Na kwa kuwa nyimbo zilikuwa ni utanzu uliojitokeza sana katika jamii hasa jamii za watu waliokuwa na uwezo mdogo katika elimu ya Kizungu, rara zilitumika kutoa kilio chao. Mfano mzuri umetolewa katika wimbo ‘Ajali ya Ntokela’ kama ulivyonukuliwa (Uk. 271), ambao pamoja na kuzungumzia tukio la ajali iliyowaua watoto, bado kuna hali ngumu ya maisha hasa katika ubeti wa saba. Katika jamii nyingi za kiafrika mwanajamii anahesabika kuwa hana njaa kwa kuwa na hazina ya nafaka. Msanii anatuonesha mama anaetegemea viazi

kuwalisha watoto wake, jambo linaloashiria umasikini wa chakula. “Watoto wale nini, wale nini jamani”, anaimba. Kwa kawaida katika jamii za Kisafwa kula viazi ni dalili ya umasikini na njaa kali katika jamii hiyo.

Kama sehemu ya sera isiyoweza kusahaulika kwa Watanzania na Mataifa ya Kiafrika, Tanzania iliendeleza harakati za ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika zikiwemo Msumbiji na Afrika ya Kusini. Hizo ni mfano wa nchi ambazo moja kwa moja zilipokea msaada wa harakati hizo kati ya nyingi zilizopata misaada ya kujikomboa kutoka kwa wakoloni. Harakati hizo ziliungwa mkono na wananchi na baadhi ya wasanii walijitokeza kuunga mkono na kuwatia moyo wananchi kupambana kwa dhati. Mfano wa wimbo ‘Ukombozi wa Afrika’ kama unavyoimbwa na vikundi mbalimbali vya rara wakiwemo Kilwa Jazz, Moro Jazz, na Kiko Kids.

Sisi Watanzania hatutabadili ahadi yetu ya Afrika, Tutaitetea Afrika yote mpaka iwe huru,

Tumesimama imara

Hatutakubali kuchezewa na yeyote

Tupo tayari kufa Watanzania kuliko kuonewa x3 Maghani: Eeeeh heeee

Ooooh! Ooooh! Wazumi: Afrika tutayari kufa Afrika kuliko kuonewa Yeli: Na Tanzania iko tayari kufa Mpaka ione Afrika nzima iko huru Wazumi: Afrika tutayari kufa

Afrika kuliko kuonewa Yeli: Hii Zambia iko tayari kufa Mpaka ione Afrika yetu iko huru Wazumi: Afrika tutayari kufa

Yeli: Guine na Mali, Ghana tayari kufa Mpaka ione Afrika yote iko huru Wazumi: Afrika tutayari kufa

Afrika kuliko kuonewa

Yeli: Kongo Kishansa na Braza tayari kufa Mpaka ione Afrika nzima iko huru Wazumi: Afrika tutayari kufa

Afrika kuliko kuonewa

Yeli: Kenya Burundi Rwanda tayari kufa Mpaka ione afrika yetu iko huru Wazumi: Afrika tutayari kufa

Afrika kuliko kuonewa

Yeli: Ethiopia, Sudani, Somali tayari kufa Mpaka ione afrika yetu iko huru Wazumi: Afrika tutayari kufa

Afrika kuliko kuonewa

Miaka ya mwishoni mwa 1970 na mwanzoni mwa 1980 nchi ilipata mtikisiko mkubwa wa kiuchumi. Mtikisiko huu ulisababishwa na mambo kadhaa; kubwa ilikuwa ni vita kati ya Tanzania na Uganda mwaka 1978. Uhaba wa vitu vingi muhimu kwa maisha ya binadamu kati ya mwaka 1980 na 1984, huu ulikuwa ndiyo wakati ambapo serikali ilianza kupunguza idadi ya wafanyakazi katika mashirika ya umma na serikalini ili kukidhi masharti ya mashirika ya fedha ya dunia—yaani Shirika la Fedha la Dunia na Benki ya Dunia. Viwanda vilikuwa vikizalisha chini ya uwezo kiasi kwamba vingi vyake vilitumia uwezo kati ya asilimia 30 na 50, na mchango wa viwanda katika uchumi wa taifa ulikuwa umeteremka kutoka asilimia 10.4 mwaka 1977 hadi asilimia 5.8 mwaka 1980. Kadhalika, licha ya mfumuko wa bei, ambao mwishoni mwa miaka ya 1980 ulikuwa umefikia hadi asilimia 30, deni la taifa kutokana na kukopa nje lilikuwa likipanda kila kunapokucha kwa mamilioni ya

dola. Kwa ujumla, hali ya wafanyakazi na wakulima ilikuwa inazidi kuwa duni siku hadi siku, kiasi kwamba hadi kufikia mwaka 1984, mshahara wa chini ulikuwa unatosheleza mahitaji muhimu ya siku tatu tu kwa mwezi (Chachage, 1999). Wananchi walikosa chakula na mahitaji mengine ya msingi. Tatizo lingine liliingia miaka ya 1980 UKIMWI. Mambo yote haya yaliongeza machungu kwa mwananchi wa kawaida. Sanaa ya wanajamii na hasa vijana ambao wengi wao walikuwa wamehamia mijini kukimbia hali ngumu zaidi huko vijijini ilisawiri maisha hayo.

4.5 Rara Katika Kipindi cha Soko Huria 1988 - 2010

Kufikia miaka ya 1984 hadi 1987 kulikuwa na ongezeko la wasomi katika nchi ya Tanzania ukilinganisha na miaka ya 1960 hadi 1980. Wasomi hawa walikuwa na changamoto mbalimbali dhidi ya serikali na mipango ya kiuongozi. Miongoni mwa changamoto hizi zilikuwa za kiuchumi, kiuongozi na kisera katika siasa ya Tanzania. Kwa namna moja na nyingine harakati za wasomi hawa ziliwafumbua macho watawala na baadhi ya mambo ilibidi yarekebishwe. Kwa mfano, Rais wa Kwanza Mwalimu Juliua Kambarage Nyerere aliamua kumwachia Uraisi Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi. Pamoja na hayo tukashuhudia vuguvugu la kuelekea mchakato wa uanzishwaji wa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Kipindi hicho cha miaka ya 1980 kilishuhudia mfumo wa Ujamaa na kujitegemea kuanza kupoteza umaarufu wake. Kupotea huku kwa umaarufu wa sera ya Ujamaa na kujitegemea yalikuwa ni matokeo ya kuongezeka kwa watu waliokuwa na uwezo wa kuhoji hasa mantiki na faida ya mfumo wenyewe kwa wananchi. Kufifia kwa ujamaa na kujitegemea kulipisha mfumo wa soko huria ambao ulianza kujipenyeza tangu katikati ya miaka ya 1980 na kushamiri baada ya Mwalimu Nyerere kuachia

madaraka. Pamoja na Azimio la Zanzibar kubariki mfumo wa kibepari, mfumo wa Ujamaa na kujitegemea haukutangazwa rasmi na mpaka leo hii hakuna kiongozi yeyote aliyekwishatangaza kuachana na Ujamaa na Kujitegemea. Kuingia katika mfumo wa kibepari kulileta mabadiliko makubwa kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Masuala haya yalibadilisha hata mtazamo na sura nzima ya sanaa kama anavyosema Lenin, (1970) akinukuliwa na Senkoro, (1987) anasema; “Hadithi zisizokuwa na mantiki, bali zilizo na mahusiano mithili ya ndoto; mashairi yenye sauti tamu na yenye maneno yanayosikilika vizuri masikioni, hata hivyo yasiyo na maana wala mantiki huwa sanaa ya wakati huu”. Hii humaanisha kuwa katika mfumo wa kibepari kila kitu kinachofaa kufanywa biashara, hufanywa hivyo. Kwa hali hiyo, watu wenye sauti nzuri huziuza sauti hizo jukwaani na katika santuri, wenye misuli mikubwa huziuza nguvu zao kwenye michezo ya masumbwi, na wale wasio na chochote wakilazimika kuiuza miili katika ukahaba ili mradi wapate fedha. Mfano katika eneo hili ni Rara kutoka jamii ya Wagogo kutoka Dodoma;