• Tidak ada hasil yang ditemukan

Mkanganyiko wa Rara na Nyimbo Nyingine

Kama asemavyo mwanahistoria Ranger, (1970), alipata mshangao alipowaona watu wa Ziwa Nyasa wakicheza rara aina ya Mganda mnamo mwanzoni mwa miaka ya 1970. Kilichomshangaza ni ule uvaaji wa wachezaji wa rara hiyo: yaani shati jeupe, suruali/kaptura nyeupe na tai. Aliarifiwa kwamba ngoma hiyo ya asili imekuwa ikitumia mavazi hayo kwa vizazi vingi, na ndivyo ngoma ilivyokuwa ikichezwa kimila.

Katika utafiti wake kuanzia pwani ya Afrika ya Mashariki hadi Afrika ya Kati, kilichojidhihirisha ni kwamba chimbuko la Mganda lilikuwa ni aina ya ngoma ambayo ilianzia pwani mwa Afrika ya Mashariki mara baada ya kuingia kwa wakoloni, mnamo miaka 1890. Nayo ilikuwa ikiitwa Beni Ngoma. Ngoma hii ilianzia Mombasa na hapa Tanzania, ilianzia Tanga na Pangani. Hadi mwaka 1914, ngoma hii ilikuwa imeenea nchi nzima, na lugha kuu iliyokuwa ikitumika katika

ngoma hii ilikuwa ni Kiswahili na kidogo sana lugha za makabila ya kando kando ya ziwa Nyasa. Ngoma hii ilikuwa pia ndiyo chimbuko la ngoma nyingine kama Kalela, Malipenga, Lelemama, Mbeta na hata huu muziki unaoitwa muziki wa dansi siku hizi. Kwa Wamwera kulizuka Chikosa, kwa Wanyamwezi kukawa na Dundo, huko Ulanga kukawa na Mlangimlangi, na kwa Wasukuma Wigashe. Hata Enanga miongoni mwa Wahaya na Wakerewe. Mitindo ya nyimbo hizi ilikaribiana kwa kiasi kikubwa na Beni Ngoma. Beni Ngoma ilienea katika jamii nyingi za Afrika ya Mashariki na ya Kati.

Ranger anaendelea kusema kuwa, kihistoria jina la ‘Beni Ngoma’ lilitokana na mfumo wake wa kimuziki ambao ulitokana na majaribio ya kufuatisha mvuto wa upigaji wa muziki wa kijeshi (military brass-band) wa wakoloni, wakati mwingine kufuatana na hali kwa kutumia matarumbeta, filimbi au ngoma moja au kadhaa. Ingawa kulikuwa na tofauti za hapa na pale kati ya jamii na jamii, kimsingi ulijikita katika mazoezi ya kijeshi. Muziki huu wakati mwingine ulichukua fani ya gwaride, maandamano, mwendo wa kutembea wa askari, au wakati mwingine mduara wa mazoezi ya kijeshi.

Uimbaji ulikuwa ni sehemu muhimu ya muziki huu. Nyimbo hizo zilihusu mambo yaliyokuwa yakitokea kila siku kama magonjwa, ukame, na masuala ya kishujaa. Beni ngoma ilijikita katika migawanyiko kati ya wanawake na wanaume, na katika vikundi hivyo kulikuwa na maofisa na vyeo (Wafalme, Mamalkia, Majemadari, Majenerali, Maluteni n.k.), kadhalika sare ambazo zilitambulisha makundi na vyeo hivyo. Kivyeo na kimakundi, walijipa majina kama Sultani, Kingi (mfalme), Malkia, Marini (wanamaji—askari wa hali ya juu), Arinoti (wale wa hali ya chini wenye

kunuka na kutoa jasho) Skotchi, Nidhamu, Ba Simba, Askari, Banu Saada, Keya (K.A.R.—Kings African Riffles) na kadhalika mambo ambayo yanaendelea hata katika rara ya hivi leo na muziki wa kisasa. Makundi haya yalienea kutoka Lindi hadi Bukoba. Kulikuwa na kawaida ya makundi mbalimbali kukusanyika katika mashindano na wakati mwingine yaligombana katika mashindano yao. Lakini baadaye yaliafikiana na hata kupatana.

Makundi haya yalikuwa na mawasiliano na ufuasi nchi nzima, na mamanju wao waliweza kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kushiriki katika matamasha ya makundi waliyohusiana (Chachage, 1999). Yalikuwa pia ni makundi ya kusaidiana. Wakoloni na wamisionari waliwachukia sana washiriki wa Beni Ngoma. Sababu kubwa ya kuwachukia ilikuwa ni umoja uliojibainisha kati yao, jambo lililoleta hofu ya kufanya kinyume na utawala wao.

Kwa msimamo wao, hawa walikuwa wakivuruga maadili ya Kiafrika na kutishia misingi ya Ukristo. Kihalisi, Beni Ngoma haikuwa uigaji wa muziki wa Kizungu, bali ubadilishaji wa muziki huo ili kukidhi matakwa ya umuhimu wa kushikamana katika mazingira ambayo yalikuwa yakiyabomoa mahusiano ya umoja wa kijumuia, ikiwa ni pamoja na kuuingiza muziki wa dansi. Wakoloni waliwapiga marufuku wafanyakazi wa serikalini kushiriki katika ngoma kama hizo, wakidai kwamba ni za “kishenzi”, japokuwa ngoma hizi nazo pia zilipinga “ushenzi” wa kikoloni. Kadhalika wakaanzisha utozaji wa kodi katika miji kila ngoma hizo zilipochezwa. Nyimbo nyingi zilizoimbwa katika ngoma hizi, ziliwakashfu na kuwadhihaki wakoloni. Kufikia miaka ya 1940, Beni Ngoma ilikuwa tofauti kabisa na Fox Trot au miziki mingine ya Kizungu. Ilikuwa imekwisha kuwa ainisho la utamaduni wa

watu waliokuwa wamehamia mijini na kwenye mashamba ya Wazungu kama manamba.

Katika nyanja nyingine, ufuasi wa Marini na Arinoti ulijitokeza kwa njia ya mchezo wa mpira wa miguu, kukiwa na wafuasi wa Sunderland na Young Africans. Ngoma hizi mwishoni mwa ukoloni zilichukua majina mbali mbali na tofauti kufuatana na mahali zilipokuwa zimejikita. Baadhi yake, kama vile Lele Mama, Gombe Sugu na Hiari ya Moyo zilijipatia umaarufu wa kipekee katika harakati za kampeni za kupigania uhuru. Umaarufu wake ulianza kufifia miaka ya 1960.

Kwa upande wa nyimbo, Mulokozi, (1996) anafafanua nyimbo kama kila kinachoimbwa. Ufafanuzi wa Mulokozi unaipa dhana ya nyimbo upana mkubwa kiasi ambacho hata tanzu za kinathari kama hadithi kuweza kuingia katika kundi la nyimbo pindi zitolewapo kwa kuimbwa. Naye Nkwere (h.t) anasema kuwa nyimbo ni maneno yanayotamkwa kwa sauti ya muziki, yaani maneno yanayoambatana na uimbaji. Mambo haya mawili yaani maneno na uimbaji, yamepangwa kwa namna inayogusa na kumwathiri binadamu kwa namna fulani kupitia hisi zake na akili yake. Uimbaji wenyewe waweza kuwa pamoja na sauti za ala au bila sauti za ala. Ufafanuzi huu unasisitiza mambo mawili ambayo sharti yawepo, yaani maneno na uimbaji ijapokuwa sauti za ala na miondoko ya uchezaji vyaweza kuwepo au kukosekana na wimbo ukabaki kuwa wimbo.

Akifafanua dhana ya nyimbo Freuchen (1962) anaunganisha mawazo ya Nkwera (h.t) na Mulokozi (1996) kwa kusema kuwa;

Nyimbo ni mawazo yanayoimbwa na watu baada ya kusukumwa na nguvu maalumu. Mawazo hayo

hayawezi kutolewa kwa hadhira katika mazungumzo ya kawaida yakaeleweka ama kuleta athari

iliyokusudiwa…..mawazo ya mwanadamu

yanasukumwa na nguvu maalum iliyozingirwa wakati huo kama vile furaha, hofu, uchungu, simanzi, ….. Mawazo yaweza kumfurika mtu kichwani na kumfanya apumue kwa mashaka na moyo kumdunda. Mwanadamu awapo katika hali hii hujikuta katika athari fulani inayoyasukuma maneno yenyewe yanayohitajika kulieleza tukio hilo. Maneno hayo ndiyo yaundayo wimbo mpya.

Freuchen anasisitiza dhana kuwa, kazi ya sanaa hasa nyimbo haina budi kutokana na mazingira. Mazingira ndiyo yanachochea hisia na hatimae mawazo kwa msanii wa nyimbo ili aweze kufanya kazi yake ya usanii wa nyimbo. Pengine Matteru (1987) anatusogeza mbele zaidi kwa kusema kuwa; nyimbo ni tungo za kishairi zenye kutumia mahadhi, melodia, mkong’osio, mapigo na muwala. Nyimbo huweza kuimbwa na mtu mmoja pekee ama na wazumi wake wakiitikia mkarara.

Maelezo ya Freuchen, (1962); Matteru (1987), Mulokozi (1996) na Nkwera (h.t) yanabainisha sifa za nyimbo kwa ujumla wake kuwa lazima kuwepo na muziki wa sauti ya mwimbaji au waimbaji, muziki wa ala kama zimejumuishwa, maneno yanayoimbwa, hadhira inayoimbiwa na muktadha unaofungamana na wimbo huo kama vile sherehe, ibada, kilio au tukio lingine lolote. Nyimbo zinapoimbwa hutumia vipengele vingi katika kuwasilisha ujumbe kama ulivyokusudiwa, vipengele hivyo huwa si maneno tu wala mazungumzo bali vidokezo, miguno, miliolio, toni, vituo, kiimbo, vijisauti na ishara nyingine.

Utanzu wa fasihi simulizi wa ushairi simulizi ndio wenye vipera vya nyimbo, maghani, na Semi. Katika maghani kuna maghani ya kawaida na maghani simulizi

(Matteru 1987; Mulokozi 1989 na Wafura na Ndungo 1993). Rara zinapatikana katika maghani simulizi pamoja na ngano, sifo na tenzi. Rara pamoja na kusimulia mambo ya kubuni ingawa nyingine husimulia matukio ya kweli, zinajibainisha na sifa za kuwa tungo za kishairi, zinasimulia hadithi kamili au tukio kwa kirefu (ni hadithi kamili), zinatungwa papo hapo wakati wa utongoaji, zinaambatana na muziki wa ala na mtambaji huwa ni fundi wa kupiga ala fulani ya muziki. Utafiti huu unazitazama rara kama zinazoambatana na sifa hizo. Hata hivyo, rara nyingi katika makabila mbalimbali zinapata majina yake ya kikabila kutokana na ala kuu itumikayo katika utambaji wake. Kwa mfano, Babatoni, Ndili, Mbeta, Kingwengwi, Mbeni ngoma, na nyingine.