• Tidak ada hasil yang ditemukan

MBINU NA NJIA ZA UTAFITI

3.5 Eneo la Utafiti

Utafiti huu ulifanyika katika Mikoa ya Mbeya na Dar es salaam. Kwa upande wa Mkoa wa Mbeya wilaya za Mbozi, Momba, Mbeya Vijijini na Mbeya Jijini ilihusika.

Aidha, katika wilaya ya Mbozi mtafiti na watafiti wasaidizi walitembelea kata tano za Mlowo, Vwawa, Myovizi, Isansa, na kata ya Nambinzo. Uteuzi wa kata hizi ulitokana na taarifa za kupatikana kwa watambaji wa rara ambazo tulizipata kutoka kwa Afisa utamaduni wilaya Ndugu, Godfrey Msokwa. Wenyeji wa Wilaya ya Mbozi na kata zake tulizozizungukia ni wa makabila ya Wanyiha na kidogo Wandali kutoka Wilaya ya Ileje. Kwa kuwa mwingiliano wa makabila ya Wanyiha na Wandali ni mkubwa na kutokana na jamii hizi kufanana misingi ya kiuchumi na kimazingira lugha zao na tamaduni zao pia hufanana.

Kwa upande wa Wilaya ya Momba; Wilaya hii ilikuwa ilikuwa sehemu ya Wilaya ya Mbozi kabla ya kugawanywa mwaka 2012. Wakazi wake ni mchanganyiko wa makabila ya Wanyamwanga, Wanyiha, Wandali na Wafipa kutoka Mkoa wa Sumbawanga. Wanyamwanga ambao ndio wenyeji hasa wa wilaya hii wanakurubiana kwa karibu sana na Wanajamii kutoka nchi jirani ya Zambia. Inasemekana kuwa jamii hii ilihama kutoka Zambia miaka mingi iliyopita. Ushahidi wa suala hili unabainishwa na mfanano wa majina ya wakazi wa Tanzania (Wanyamwanga) na wenyeji wa Zambia. Aidha, kata za Msangano na Kamsamba zilitembelewa na watafiti kutokana na sababu ile ile iliyotusababisha kuteua kata za Mbozi. Hata hivyo, katika Wilaya ya Mbeya vijijini kata mbili za Mbalizi na Iwindi zilitembelewa. Wenyeji wa eneo hili ni Wasafwa, Wandali na Wanyakyusa. Katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya tulikamilisha utafiti wetu kwa kuhudhuria kongamano la Safari Lager Traditional Dance Competition lililofanyika tarehe 22/09/2013. Mashindano haya yalitanguliwa na kuonana na watambaji wa rara vilabuni na katika mikusanyiko ya watu kama ilivyofafanuliwa katika sura ya tano na sita.

Mkoa wa Dar es salaam tulikusanya data kutoka kituo cha utangazaji cha taifa (TBC). Hapa tulikusanya data iliyorekodiwa kwa kipindi kirefu na kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya nchi. Taarifa zilizopatikana TBC zilitusaidia kulinganisha na kutathmini mabadiliko ya rara kulingana na vipindi mbalimbali vya maendeleo jamii ilivyopitia. Hii ni kusema kwamba, utafiti wetu pamoja na kuteua Mkoa wa Mbeya kama eneo kifani, umechambua na kutathmini mabadiliko ya rara kutoka maeneo mengine ya Tanzania.

3.6 Sampuli

Sampuli ni sehemu ndogo ya jamii ya watafitiwa ambayo huteuliwa na mtafiti kwa lengo la kupata taarifa juu ya tatizo linalotafitiwa. Kiwango cha ukubwa wa sampuli huamuliwa na mtafiti mwenyewe kutokana na sababu kadhaa. Miongoni mwa sababu hizo ni aina ya utafiti, asili ya mada husika, pamoja na kiasi cha rasilimali alizonazo mtafiti. Rasilimali hizo ni kama vile muda, vifaa na fedha za kuendesha utafiti wake. Cohen na Lawrence (2000) na Bryman (2004).

3.6.1 Sampuli ya Watafitiwa na Upatikanaji Wake

Sampuli ya utafiti huu ilipatikana kwa kutumia mbinu ya sampuli lengwa. Sampuli lengwa ni sehemu ndogo ya jamii ya watafitiwa ambayo huchaguliwa na mtafiti itumike katika utafiti wake kwa sababu ya kuwa na sifa za kukidhi mahitaji ya utafiti. Kwa kutumia msingi wa sifa hizo, mtafiti huwa huru kuchagua kadri aonavyo kuwa watafitiwa wanaweza kutoa taarifa za kutosheleza (Smith, 1997). Sampuli lengwa hufaa sana kutumiwa katika utafiti wa kifafanuzi kama huu wetu na hii ndiyo sababu ya kuteua mbinu hii. Pamoja na kwamba mbinu hii ya utafiti huhitaji umakini wa ziada katika kufanya majumuisho kutokana na mara nyingi kutumia idadi ndogo

ya sampuli lengwa; tuliamua kuitumia kwa sababu ndiyo inayoendana na mada ya utafiti wetu. Pia, utafiti wa kifafanuzi hutoa fursa kwa mtafiti kupata taarifa za kina kwa sababu taarifa hizo hutolewa na watu wenye sifa na upeo wa kutosha juu ya mada husika. Hata hivyo, ni kutokana na taarifa hizo kuweza kupatikana katika mazingira asilia ya mada husika (Shulman, 1988). Kwa kuwa, katika jamii wasanii huwa ni wachache ukilinganisha na wakazi katika jamii, watafitiwa walichaguliwa kiholela kulingana na jinsi walivyokuwa na sifa zinazokidhi haja na malengo ya utafiti huu. Sampuli hii iliundwa na makundi yafuatayo;

(i) Wasanii na watambaji rara waliokuwa wamependekezwa walikuwa wanane. Aidha ilipendekezwa kujumuisha jinsi zote, jambo ambalo limetekelezwa. Hata hivyo idadi ya watambaji rara wanane imeongezwa mpaka kufikia idadi ya watambaji kumi na wanane (18). Hali hii inaonesha mafanikio makubwa ya utafiti wetu na kati ya hao watambaji wa jinsi ya kike ni saba na wa kiume kumi na mmoja. Kwa kawaida wasanii katika jamii ni wachache. Pamoja na uchache wao, idadi ya wasanii wa kike pia inapungua ukilinganisha na wasanii wa kiume. Hii ni sababu kubwa ya kupatikana wasanii wa kike saba dhidi ya wasanii wa kiume kumi na mmoja.

(ii) Katika utafiti huu ilipendekezwa kuhudhuria maonesho manne na kila onesho tulipendekeza kuhojiana na watazamaji wanne. Utafiti wetu ulifanikiwa kuhojiana na watazamaji wawili katika kila onesho na hawa waliteuliwa kutokana na hali halisi ya muktadha. Sababu za kupunguza idadi ya watu waliohojiwa ilitokana na wengi kuonekana kurudia kilichojibiwa na waliotangulia. Hii ilisaidia kufikia hitisho la kilichohitajika kujulikana kutoka kwao.

(iii) Kazi kutoka maktabani zilipatikana za kusikiliza na za kusikiliza na kuona. Hapa tulipata kazi za rara ya Kitanzania na kazi za rara kutoka ng’ambo kama vile nyimbo za Kanda Bongomani, Arusi Mabele, Yondo Sista na wasanii wengine. Hizi zilitusaidia kutathmini mabadiliko kifani na kimaudhui yaliyotokana na mwingiliano wa kitamaduni. Aidha, tulikumbana na changamoto ya kukosa maelezo ya kutosheleza juu ya kazi hizo kulingana na kwamba, watambaji walizirekodi katika vituo husika na hawakuacha maelezo yanayofafanua kwa kina kinachomaanishwa katika nyimbo husika.

Bwana Allen Chilewa mwendeshaji wa kipindi cha ‘nyimbo za makabila mbalimbali ya Tanzania’, Anna Mahimbo mwendeshaji wa kipindi cha ‘Afrika yetu’ na Aisha Datchi Mkuu wa TBC Taifa walishindwa kutoa taarifa zinazohusiana na nyimbo hizo kutokana na kuimbwa katika lugha za makabila ambazo hazifahamiki kwao. Hata hivyo, tulijitahidi kutafuta uwezekano wa kupata wenyeji wa lugha hizo ili kuzitolea ufafanuzi nyimbo zilizoteuliwa na hili lilitatuliwa kwa kiasi fulani.