• Tidak ada hasil yang ditemukan

Maudhui ya Rara Kipindi cha Uhuru 1961 hadi 1967

MAUDHUI NA FANI YA RARA ILIVYOBADILIKA KATIKA KILA AWAMU YA MAENDELEO

5. Wimbo wa Ntonga

5.1.3 Maudhui ya Rara Kipindi cha Uhuru 1961 hadi 1967

Msingi wa sanaa ni maisha halisi ya mwanadamu, hili limejadiliwa katika mjadala wa nadharia tunazozitumia kubainisha maudhui ya rara katika awamu mbalimbali za maendeleo ya jamii. Wakati huu Tanzania ilikuwa ikiingia katika ujenzi wa jamii mpya. Jamii inayojitawala kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa. Baada ya mapambano ya muda mrefu dhidi ya ukoloni taifa la Tanzania (Tanganyika wakati huo) mwaka 1961 lilipata uhuru. Shangwe na shamrashamra zilihanikiza kila kona ya nchi kusherehekea uhuru.

Hata hivyo, uhuru uliopatikana ulipatikana baada ya kuwa mambo mengi yanayoitambulisha nchi yalikuwa yameharibiwa na wakoloni. Suala la msingi lililokuwa changamoto kubwa lilikuwa kujenga na kuimarisha utamaduni wa Mtanzania kama asemavyo Nyerere katika hotuba yake ya 12/09/1962; “Nchi isiyokuwa na utamaduni haina tofauti na mkusanyiko wa watu ambao hawana roho iwawezeshayo kuwa taifa”. Maelezo ya Mwalimu Nyerere yalikuwa yakiwalaani Wakoloni kwa kuharibu utamaduni wa Waafrika na vitendo vya kuwafanya Waafrika waamini kwamba hawana utamaduni wao wenyewe. Suala hili lilikuwa ni moja ya michakato iliyopewa kipaumbele katika kuelekea maendeleo ya taifa huru. Aidha, maudhui ya nyimbo zilizoimbwa zilisisitiza mtazamo huu na kama ulivyoainishwa katika miongozo ya chama cha TANU. Mfano mzuri ni wimbo ‘Mwongozo wa TANU’ uliokuwa ukiimbwa na vijana wa TANU YOUTH LEGUE.

Yeli: Hoyeeeee!

Mwongozo mpya umetangazwa Na uhuru siyo ule wa bendera pekee Wala wimbooo wa Taifa si uhuru wa kweli Bali kila kitu tumiliki sisi wenyewe wananchi x3

Mwongozo!

Yeli: Mwongozo mpya wa TANU Wazumi: Hoyeee twafurahia oooooh Yeli: Mwongozo mpya wa TANU Wazumi: Umma twaunga mkonoo Yeli: Tumenyonywa vya kutosha Wazumi: Hoyeee twafurahia oooh Yeli: Tumeonewa vya kutosha Wazumi: Umma twaunga mkonoo Yeli: Tumepuuzwa vya kutosha Wazumi: Hoyeee twafurahia ooooh Yeli: Sasa twataka mapinduzi Wazumi: Umma twaunga mkono Yeli: Oooooh! Oooooh! Oooooh! Wazumi: Hoyeee twafurahia ooooh! (Muziki wa ala)

Yeli: Mwongozo mpya wa TANU Wazumi: Umma twaunga mkono Yeli: Kuzikwa kwa mabepari Wazumi: Hoyee twafurahia ooooh! Yeli: Kuzikwa kwa wanyonyaji Wazumi: Umma twaunga mkono Yeli: Oooooh! Ooooh! Ooooh! Wazumi: Hoyeee twafurahia eeeeeeh!

Katika wimbo huu maudhui yanayodai Tanzania kutambuliwa kama nchi iliyohuru na wala si nchi yenye uhuru wa bendera yanajitokeza. Hali hii inatokana na madai ya kufanya mambo ya nchi kama kupanga na kuamua masuala ya kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa na wananchi wenyewe na wala si kwa shinikizo kutoka kwa wakoloni. Masuala ya unyanyasaji, ukandamizaji na kupuuzwa yanalaaniwa na haya yalikuwa katika miongozo ya chama tawala TANU. Hili halikuwa bahati mbaya katika enzi hizo. Pamoja na uhuru uliokuwa umepatikana, lakini maamuzi ya kikoloni yalionekana kuendelea kujitokeza katika sehemu mbalimbali za utawala. Wananchi na serikali walikuwa katika vita ya kuondoa uhuru wa bendera na kupata nguvu kamili za maamuzi.

Hata hivyo, maudhui yanayojibainisha wakati huu yanajitokeza katika makundi mawili, kundi la kwanza likihusisha masuala ya kisiasa na kundi la pili likihusisha masuala ya kijamii. Jambo linaloonekana katika makundi yote haya ni suala la uchumi ambao nao bado ulikuwa katika hatua ya chini sana.

Kwa upande wa kisiasa, kuna nyimbo zilizohamasisha ujenzi wa nchi na chama cha TANU kwa ujumla wake. Aidha, nyimbo hizi zilikuwa katika mwelekeo wa kujenga jamii inayoipenda na kuiheshimu nchi yake. Mfano mzuri unatolewa katika wimbo ufuatao kama ulivyokusanywa kutoka TBC, ‘Heko U.W.T’

Tunawapa heko Umoja wa kina mama Kwa kudumisha chama

Chama cha kina mama Tanzania Tunawatakieni mzidi kuendelea

Muwashinde adui watatu zetu wanaotupa tabu ooh! Oooooh! Tunawapa heko

Heee!

Umoja wa kina mama oyeee! Mwenyekiti Sophia Kawawa hoyee! Umoja wa kina mama hoyeee! Katibu mkuu Tekra Mchalu hoyeee! Umoja wa kina mama hoyeee! Makamu wake Salome kisusi hoyee! Umoja wa kina mama hoyeee! Wakidumishe chama hoyee! Hoyee! Kwa nguvu moja bila kusita hoyeee!

Umoja wa kina mama Tanzania (U.W.T) uliundwa muda mfupi baada ya uhuru wa Tanganyika kupatikana ikiwa ni mkakati wa kujenga chama katika ngazi zote za wananchi miaka ya 1960. Wimbo huu umebeba maudhui ya kuwatia moyo viongozi waasisi wa umoja huu kufanya kazi ya kujenga chama cha TANU; na kuhamasisha wananchi kufanya kazi ili kuondoa maadui watatu kama ilivyoainishwa na chama wakati huo, yaani Ujinga, Umasikini na magonjwa.

Aidha, kuna nyimbo zilizisherehekea uhuru na kuwatukuza watawala. Nyimbo hasa ngonjera za Mnyampala na mashairi ya Saadan Kandoro ni mifano mizuri katika eneo hili. Nyimbo hizi na mashairi pamoja na kuandikwa miaka ya 1970, yalianza kughanwa na kuimbwa mbele ya hadhara miaka ya mwanzoni mwa 1960 na nyingine zilitumika katika kudai uhuru (Tuli, 1985). Kwa mfano, ngonjera za Mnyampala (1971) ambazo zilifundishwa hadi mashuleni na kuimbwa wakati wa matamasha ya Chama na Serikali. Mfano wa ngonjera ya Wakati Wetu ni Huu

Salam Baba Taifa, Nyerere wa kusifika Tunafuraha taifa, mambo ya nje kushika Yafaa tukupe sifa, na uzidi kutukuka Wakati wetu ni huu, kuwajua viongozi

Salam baba Karume, Makamu wetu wa kwanza Ulivyofanya kiume, juhudi tena ongeza

Yafaa uungurume, kila mara ni wa kwanza Wakati wetu ni huu, kuwajua viongozi Salam Baba Kawawa, makamu wetu wa pili Ulivyosema ni sawa, tutumie Kiswahili Twatumia sawa sawa, kusoma na kwa akili Wakati wetu ni huu, kuwajua viongozi Pongezi Bryceson, kilimo na ushirika Si bwawani si mtoni, mote humu umeshika Kwenye siku za usoni, Tanzania ‘tasifika Wakati wetu ni huu, kuwajua viongozi Pongezi bwana Jamali, Waziri wetu wa fedha Tutunzie zetu mali, mioyo ipate ladha

Pesa zile za asili, zile tena si faradha Wakati wetu ni huu, kuwajua viongozi Pongezi bwana Bomani, mipango maendeleo Upige kila pulani, tunatega masikio

Twakuomba kwa hisani, twataka maendeleo Wakati wetu ni huu, kuwajua viongozi

Ngonjera za Mnyampala zinaingia hapa kutokana na historia yake. Kabla ya kuandikwa, hasa kipindi chote cha baada ya Uhuru ziliimbwa mbele ya hadhira na

vijana wa TANU na wanafunzi kutoka shule mbalimbali Tanganyika. Haya yalifanyika katika matamasha mbalimbali ya viongozi wa chama na serikali. Mnyampala anawataja viongozi waasisi wa Chama cha TANU na waasisi wa Muungano ambao ulipatikana miaka mitatu baada ya uhuru wa Tanganyika. Hata hivyo, kinachoonekana ni kuwapongeza na kuwasifia kwa kupewa dhamana hizo. Masuala ya utamaduni, ulinzi na matumizi bora ya rasilimali za taifa yanajitokeza kama sehemu ya kuwakumbusha majukumu yao kwa jamii.

Aidha, nyimbo nyingine ziliendelea kutumia maneno ya kejeli na kuyakumbuka mateso yaliyofanywa na Wazungu wakati wa utawala wao. Hata hivyo, msingi mkubwa wakati huu haikuwa lawama, bali kuwahimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii kama inavyojibainisha katika wimbo, ‘Kazi Ndiyo Msingi wa Maisha’ Kutoka TBC;

Wito kwa raia wote tusiwe wavivu, Kwaajili ya maisha yetu!

Yawe bora tufanye nini? Tufanye kazi nguvu moja,

Tuinue uchumi kwa harakaaaa x4 Kazi ndiyo msingi wa maisha, Maendeleo yaletwa na kazi x2 Tusikalie eeehe he he!

Uchumi wetu eehe he he!

Tufanye kazi tusiwe wavivu oooh Kazi ndiyo msingi wa maisha, Maendeleo yaletwa na kazi x2 Bila kazi eehe he he!x2

Taifa lolote haliwezi kujengeka. Kazi ndiyo msingi wa maisha, Maendeleo yaletwa na kazi x2 Tusikalie eeehe he he!

Uchumi wetu eehe he he!

Kazi ndiyo msingi wa maisha, Maendeleo yaletwa na kazi x2 Bila kazi eehe he he!x2

Taifa lolote haliwezi kujengeka

Wimbo huu pamoja na kuimbwa na wanamuziki wa mwanzo, zikiwemo bandi za Moro Jazz, Kilwa Jazz, Kiko Kids na wengine bado uliimbwa na wanamuziki mbalimbali katika mikutano ya hadhara kama sehemu ya kuhimiza wananchi kufanya kazi. Wimbo huu ulisaidia kueneza sera ya chama cha TANU ya ‘Kazi ndiyo msingi wa maisha’. Mtu alihesabika kuwa na heshima, utu na thamani kutokana na kazi. Uvivu ulikuwa adui wa taifa na jumii kwa ujumla, hivyo maudhui ya wimbo huu yalisadifu matakwa ya mtazamo wa nchi katika kujenga taifa imara.

Pamoja na maudhui ya kuhimiza wananchi kufanya kazi kwa bidii katika kujenga uchumi wao wenyewe na taifa kwa ujumla wake, bado wananchi walihimizwa kulinda uhuru wa nchi zao. Masuala ya kulinda na kuendeleza nchi yalihimizwa kwa vijana na wananchi wote. Mfano wa wimbo katika eneo hili unaimbwa na msanii Mawazo kutoka Mbeya. Wimbo huu ni ulikwisha kuwepo tangu miaka ya 1960. “Vijana”;

Eeeeh vijanaa, Waafrikaaa

Tuzilinde nchi zetu na mapinduzi ya Afrikax2

Vijana wa Afrika tuwalaani wapinga mapinduzi yetuuu! Vibaraka utumwa kuja kuchafua amani ya Afrikaaa!

Vijana ndiyo roho ya Afrika tuwe macho na vijibwa hivyoo! Vijana wa Afrika tuwalaani wapinga mapinduzi yetuuu! Vibaraka utumwa kuja kuchafua amani ya Afrikaaa!

Vijana ndiyo ngao ya Afrika tuwe macho na vijibwa hivyoo! (Muziki wa ala)

Vanavuli eeeee! Hoyeeeee!

Aidha, maudhui ya wimbo huu yanayokumbukiza machungu ya mkoloni na vitendo walivyokuwa wakiwafanyia Waafrika katika ardhi yao wenyewe. Msanii anawahimiza vijana kuwa macho na ukoloni na kila aina ya vitendo vya kuvuruga amani ya nchi. Maudhui haya yanarandana na wimbo wa Mbaraka Mwishehe ‘Vijana’ na kwa kuwa fasihi simulizi si mali ya mtu mmoja ni dhahiri kuwa nyimbo hizi ziliimbwa na wananchi wote.

Maudhui ya umasikini na hali ngumu ya uchumi katika jamii, yamejitokeza katika rara ya baada ya uhuru. Eaton, (1966) anabainisha kwamba, kigezo kikubwa cha kuubaini umasikini katika jamii ni aina ya chakula, ujinga, na maradhi. Suala hili linaungwa mkono na ufafanuzi wa Nyerere, (1977). Hali hii ilitokana na mfumo mzima wa uchumi uliorithiwa kutoka kwa wakoloni. Mfumo ambao ulitegemea vyanzo vya kibajeti kutoka mataifa ya nje (kwa wakoloni wenyewe) walioachia nchi katika hali ambayo haikuwa kwa mapenzi mema. Nyimbo nyingi zilizotungwa zilichukuwa mwelekeo wa kulalamikia maisha magumu yaliyotokana na mfumo wa uchumi uliorithiwa. Mfano wa wimbo wa rara unaoimbwa na Bwana Machezo kutoka Mbeya akilalamikia chakula kilichokuwa kikiliwa katika jamii yake: