• Tidak ada hasil yang ditemukan

Rara Katika kipindi cha Ukoloni wa Wazungu

KATEGORIA ZA RARA KATIKA AWAMU NNE ZA MAENDELEO

5. Utenzi wa Mwanakupona

4.2.3 Rara Katika kipindi cha Ukoloni wa Wazungu

Mifumo ya kitumwa na kimwinyi ilijitokeza wakati wa utawala wa Waarabu. Ujio wa wakoloni kutoka bara la Ulaya haukumaliza mfumo wa kimwinyi ghafla, hii ilikuwa mwanzoni mwa karne ya kumi na tisa (19) wakoloni kutoka bara la Ulaya walipoanza kuingia kwa nguvu barani Afrika. Watumwa ambao tayari walishakuwa katika makoloni ya Kizungu kama vile makoloni ya Kifaransa yaliendelea na utamaduni wao nje ya bara lao na mifano ya sanaa hii ni Voodoo, Lucumi, Orisha, na Rumba. Jambo la msingi ni kwamba sanaa hii ilichipuka kutokana na mila na deturi za Kiafrika. Sanaa yote hii ilikuwa kwa ajili ya burudani, sehemu ya kutunza mila na desturi zao, kama kuomba miungu yao, matambiko, na kichocheo cha ujasiri miongoni mwa watumwa hao Jahn, (1961).

Kutokana na sanaa hii kuenea sana katika mataifa ya Ulaya na msisimko wake kwa watumwa na wenyeji wa hali za kati na chini kiuchumi, ilipigwa marufuku na kupewa majina yaliyokatisha tamaa kama vile kuhusishwa na uchawi. Matokeo haya yaliifanya sanaa iliyotoka Afrika kutazamwa kwa jicho la kubeza na hata matamshi ya sanaa hii yalionesha chuki dhidi yake.

Katika mjadala huu Levine (1977) anasema; “Katika jamii nyingi za Kiafrika sanaa ya rara na nyimbo ziliweka mpaka kati ya mzimu na mzima lakini wote waliwakilishwa na mhusika mzima. Katika sanaa hii wahusika walivaa vinyago, ingawa ilikuwa kwa ajili ya burudani. Kwa mfano, kuna vinyago vilivyokejeli maasikari na vingine makahaba, sanaa hii ilifanyika mahali pa kuabudia” (Tafsiri na msisitizo wetu). Mtaalamu huyu anaeleza juu ya vionjo vya kisanaa vilivyotumiwa na wasanii katika kazi zao za sanaa, ambavyo kwa hakika ndivyo vinavyoipachika

sanaa hii kuwa sanaa ya kichawi. Aidha, Jahn, (1961) akizungumzia sanaa za Rumba, Lucumi, na Voodoo anasema;

Since the postures and movement of this dance are highly obscene, decent masters forbid their slaves to practice it and watch out to see they give it up. Because it was the part and parcel of their culture, yet the slaves love it so that even children who can hardly toddle try to imitate their parents when they see them dancing and spend whole days practicing.

Sanaa hii ya watumwa ilipozidisha upujufu katika msimamo na muondoko wake, mabwana waliipiga marufuku. Kwa kuwa ilikuwa sehemu ya utamaduni wa mtumwa, watumwa waliipenda na hata watoto waliojifunza kusimama walijaribu kuigiza wazazi wao walipowaona wakicheza na kutumia siku zote wakifanya mazoezi. (Tafsiri yetu).

Mtazamo huu ulijaa chuki juu ya sanaa ya watumwa kutoka Afrika na ilikuwa mbinu ya kuitokomeza kabisa na kujaribu kupandikiza utamaduni wao kwa Waafrika. Hii haikuwa bahati mabaya, bali ulikuwa mpango wao mahususi wa kujenga ngome imara ya utawala wao katika bara la Afrika na kwa watumwa nje ya bara lao. Aidha, kuna jambo la mapenzi ya dhati katika sanaa, mapenzi ambayo ni ya asili kama ilivyokuwa vigumu kuifuta tabia (utamaduni) na kipengele cha watoto kama sehemu ya kurithisha utamaduni huu kwa kizazi kipya. Hali hii ndiyo inayoleta ugumu kwa watawala kuitokomeza kabisa sanaa ya rara na kuhitimisha kwa kuipachika majina ya kashifa. Mawazo haya yanatolewa pia na Gubik, (1977).

Pamoja na hayo Chachage, (2009) akimnukuu Mwalimu Nyerere katika hotuba ya tarehe 09/12/1962 anasema:

Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na masuala mengine, aliongelea kuhusu historia ya utamaduni wa

Tanganyika. Naye alitamka kwamba nchi isiyokuwa na utamaduni wake haina tofauti na mkusanyiko wa watu ambao hawana roho iwawezeshayo kuwa taifa. Alivilaani vitendo vya wakoloni vya au kuwafanya Waafrika waamini kwamba hawana utamaduni wao wenyewe; ama kuufanya utamaduni wa Kiafrika uonekane kitu cha ovyo. Kutokana na hili, wengi wa waliokuwa wamesoma na kupata elimu ya Kizungu waliojiona kuwa ni “wastaarabu” walijifunza kuwaiga Wazungu kiasi kwamba, kuwa Mwafrika msomi kulimaanisha kuwa Mzungu Mweusi. Suala la muziki, kama nyanja muhimu ya utamaduni katika historia ya Tanzania, limekuwa ainisho muhimu la migogoro ya kitamaduni, na Mwalimu Nyerere katika hotuba hii alizunguumzia juu ya muziki.

Kwa maelezo yake, waliokubuhu katika elimu ya kikoloni walifunzwa kuimba nyimbo za Kizungu, lakini siyo za Wahehe, Wasukuma, Wahaya, Wanyakyusa, Wamakonde, Wanyiramba, Wagogo, Wanyamwezi n.k. Walifunzwa kucheza rumba, chachacha, rock ‘n’roll, twist, waltz na Foxtrot na mitindo mingine ya kizungu. Lakini, wengi walikuwa hawajawahi kucheza au hawakujua chochote kuhusu Gombe Sugu, Mangala, Wigashe, Ndili, Enanga, Nyangumumi, Kiduo, Lele Mama, Babatoni, Kingwengwi, au Mganda. Wengi wa waliosoma wakati wa ukoloni walijua kupiga gitaa au piano na kuimba Tenzi za Rohoni (waumini wa Kikristo), lakini walikuwa hawajui kupiga ngoma, zeze, malimba, wala filimbi ya mwanzi au pembe ya mnyama.

Haya yalitamkwa mwaka 1962, wakati ambapo kulikuwa hakuna mitandao ya kimawasiliano, video wala televisheni, kama ilivyo leo hii! Japokuwa hivi havikuwepo, “twist” ilikuwa inavuma Afrika nzima, hadi kukawa na wimbo uliodai kuwa: “Afrika yote inapenda twist, hata wanyama wa msituni wanaicheza na kuiimba”. Hali hii siyo ya kubezwa kamwe, bali ni sehemu ya kuanzia kuangalia

mabadiliko yanayojibainisha katika sanaa ya rara. Pamoja na athari hizo, nyimbo nyingi zilizokuwa zikiimbwa na wanajamii zilitumia lugha za kikabila. Aidha, lugha ya Kiswahili ilijitokeza mara chache hasa katika jamii zilizokuwa pembezoni mwa miji. Wakati mwingine lugha ya Kiswahili iliyotumika katika nyimbo hizo iliathiriwa na lahaja za maeneo watambaji husika walikotokea.

Kihistoria wakati huu ulitawaliwa na dhuluma ambayo ilivuka mipaka ya uchumi na siasa ikafikia hadi kwenye hali ya kumteka Mwafrika kimawazo asiweze kuonea ufahari nyimbo zake. Hapa ndipo baadhi ya Waafrika walipojiona kwamba wao hawakuwa na uwezo wa kufanya chochote na hata nyimbo zao hazikuwa na maana yoyote. Nyimbo za kutoka nje kama vile Twist, Foxtrot na nyingine zilizochukuliwa kama nyimbo zenye fahari dhidi ya nyimbo za Waafrika.Watu walianza kwenda katika majumba ya starehe ili kucheza na kudensi. Lugha iliyopendelewa sana ilikuwa ni Kingereza. Kipindi hiki kiliwaathiri sana vijana waliokuwa mijini na baadhi ya waafrika waliobahatika kupata elimu ya kigeni. Aidha, athari hizi zilipenya mpaka katika rara zilizoimbwa na kuchezwa maeneo ya wakoloni hawa wa Kizungu. Kwa mfano, katika vipengele vya uchezaji na mavazi kama inavyojadiliwa katika sura ya sita.

Hata hivyo, waimbaji na wachezaji wa rara wachache waliendelea kutumia lugha ya Kiswahili na wengine lugha za makabila yao katika muziki. Watambaji kama anavyowataja Mulokozi (1996), Kabishwa na Chocho na rara zao za Omwalimu owa Nyakato, iliyosimulia kisa cha mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Nyakato alimpenda mwanamke wa nje na hatimaye kuuwawa. Ngugi (2000), anawataja Waimbaji kama vile Fadhili William, Daudi Kabaka, John Mwale na wengineo

kwamba walikuwa baadhi ya wanamuziki ambao bado walisifika sana katika kuimba kwa kutumia Kiswahili. Katika Tanzania waimbaji kama Mbaraka Mwishehe, vikundi kama vya Kiko Kids, Moro Jazz band na Kilwa Jazz viliendelea kuimba kwa Kiswahili. Ufuatao ni mfano wa rara inayoimbwa na kikundi cha Moro Jazz ‘Mshenga’;

Kupita pita kunanipa wazimu, Hii ni wiki ya pili ninamuona,

Kila mara akipita nyumbani kwangu kuelekea dukani, Sura yake ya kijapani na umbo lake kweli lanisitua! Hiyeeee! Hiyeeeee! Hiyeeee!

Nitamtuma mshenga akaulize, Wazazi wake!

Nimempenda msichana akikubali Tufunge ndoa!x2

(Marudio ya beti zote)

Sherehe kubwa sana nitaifanya nyumbani, Majibu mazuri nikipata x2

Nadhiri niliyoiweka ikawa iko wazi moyoni, Hapo nitapokubaliwa x2

(Ala na maghani)

Yeleleee! Hoyeeee! Afrika hoyeeee! Yeleleeee! Hoyeeee! Afrika hoyeeee! X2

Mfano wa rara hii pamoja na kuimbwa katika Kiswahili na kutumia beti chache bado inakidhi vigezo vyote vya kuwa rara kama ilivyofafanuliwa katika sura ya kwanza. Aidha, wasanii hawa ndio waliosaidia kuendeleza lugha ya Kiswahili katika miaka ya sitini kwa kutumia nyimbo za rara. Hivi sasa kuna vikundi vingi vya mtu mmoja mmoja ambao hutamba rara kwa kutumia lugha za makabila na Kiswahili. Pamoja na hayo, Wakoloni kutoka Ulaya walipofika Afrika, hatua waliyoichukuwa ilikuwa kukomesha biashara ya watumwa hasa watumwa waliopelekwa Amerika ya

Kaskazini (Marekani), Amerika ya Kusini na Latin Amerika kama Haiti, Cuba, Columbia na kwingine. Hiki kilikuwa kipindi cha mapinduzi ya kiuchumi huko Ulaya. Viwanda vilichukua nafasi ya watumwa na watwana hivyo, watumwa walilazimika kubaki huku ili kuzalisha mali ghafi zilizohitajika huko Ulaya. Kwa mfano, nchini Tanzania yalifunguliwa mashamba ya mazao ya biashara kama mkonge Mkoani Tanga na Morogoro. Mashamba haya yalitegemea wafanyakazi kutoka kila kona ya Tanzania kama vile Waha kutoka Kigoma, Wagogo kutoka Dodoma, Wanyaturu na Wanyiramba kutoka Singida, Wanyamwezi kutoka Tabora, Wasukuma kutoka Mikoa ya Shinyanga na Mwanza, Wamakonde na Wandengereko kutoka Mikoa ya Pwani, Lindi na Ruvuma na makabila mengine ambayo yalikwenda kukutana na makabila ya Kikaguru na Kiruguru kutoka Morogoro kwa wale waliopelekwa Morogoro. Na wale waliopelekwa Mkoani Tanga walikwenda kukutana na makabila ya Wabondei na Walangi wakazi wa Mkoa wa Tanga. Aidha, wengine walichukuliwa kutoka nchi jirani kama Burundi, Rwanda, Kongo, Zambia na Malawi. Kama Tuli, (1985) anavyosema;

Wajerumani walianzisha mashamba makubwa ya mazao ya biashara ya mkonge, kahawa na mpira na wakawalazimisha Watanganyika kutoka bara na pwani (na wengine kutoka nchi za jirani) kuja kufanya kazi katika mashamba hayo. Watumishi wengi walitoka katika makabila ya Unyamwezini, Usukumani, Kasulu na Kigoma. Baadhi yao wamesalia huko na kuoana na makabila ya huko na wengine waliorudi makwao walirudi na utamaduni wa huko walikokua na lugha ya Kiswahili ambayo ilipata mwanya wa kukua na kuenea (Msisitizo wetu).

Kuhamishwa kwa makundi ya watu hawa kutoka sehemu moja na nyingine kulisababisha msambao wa rara na mwingiliano kutoka jamii mbalimbali. Rara ya wakati huu ilipinga unyanyasaji mahali pa kazi uliofanywa na watawala. Hata hivyo,

baadhi ya wasanii wa rara ambao misimamo yao haikuwa dhahiri au ilikumbwa na kasumba ya uwoga iliwasifia wakoloni. Aidha, kulitokea baadhi ya vuguvugu za upinzani ambazo zilipinga hali hii, ingawaje zilianzishwa na baadhi ya makabila yaliyochukia unyonyaji huu, Jahn, (1968) anayabainisha haya katika rara zilizoimbwa kipindi hicho katika jamii ya Waswahili: